Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Kumbe huyu Chove alibadili uraia wa Tanzania

UNAMKUMBUKA yule kipa wa zamani wa Yanga na Taifa Stars ya Marcio Maximo, Jackson Chove? Kama hujui tu, jamaa aliwahi kubadili uraia bwana.

Unajua ilikuaje? Twende pamoja kupitia mahojiano ambayo Mwanaspoti lilifanya na mlinda mlango huyu kwa sasa ni mchezaji huru na amedai atakapotimiza miaka 40 itakuwa mwisho wake wa kucheza soka na kuamua kufanya mambo mengine.

Anasema kwa sasa ana miaka 37 hivyo amesalia miaka mitatu na kwa miaka miwili mfululizo aliamua kujichimbia nchini Congo na sasa ameamua kurejea nyumbani.

MAISHA YAKE CONGO

Anasema alikaa miaka miwili 2018/2019 katika timu ya Ligi Kuu Bukabudawa akiwa na Mtanzania mwenzake Seleman Kassim Selembe ambaye wote walirejea pamoja baada ya mkataba kuisha.

“Mkataba ulikuwa wa miaka miwili tu, sasa ulipoisha kukawa na sintofahamu kwa viongozi hivyo, ikaonekana kuongezewa mkataba ni ngumu tukaamua kurudi nyumbani na kuangalia maisha mengine,” anasema huku akiongeza kiongozi aliyewapa mchongo Congo ameingia kwenye ishu za siasa kwa hiyo akaachana na timu.

KWA SASA ANAFANYA NINI

Chove anasema, kwa sasa yupo tu nyumbani kwake Mbande nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam.

“Baada ya gonjwa hili la covid 19, kuisha nitaendelea kucheza, maana yake mpaka sasahivi kuna ofa niliipata kwenda Zambia, lakini kutokana na hali iliyotokea sasa hivi sijajua itakuwaje ila kama kutakuwa na timu yoyote itakayojitokeza nitacheza haina shida,’’ anasema.

ISHU YA URAIA

Kwa sasa bado yeye ni Mtanzania. Lakini wakati fulani hapo kati alitoka Malindi ya Zanzibar akaenda Kiyovu ya Rwanda, kutokana na kumhitaji na kulazimisha akae muda mrefu walimpa uraia feki wa Rwanda ili na yeye aonekane mzawa wa Rwanda.

Anasema alikuwa akiitwa Shekimondo John Bosco jina ambalo anajulikana vilivyo kule, kwani la Chove lilipotea kabisa, hata yeye alilizoea jina hilo na maisha yalienda kwa vile alikuwa anaangalia mkwanja na damu ilikuwa inachemka.

Alicheza msimu mmoja wakati ligi imemalizika alilazimika kurejea nyumbani akapasha kidogo na Friends Rangers ikampa mchongo wa kusajiliwa JKT Ruvu, sasa JKT Tanzania.

Akiwa JKT, Kocha wa Taifa Stars, wakati huo Mbrazil Maxio Maximo akamwita kikosini na hapo ndipo ndoto za kurudi Rwanda zikafa kabisa, kwa kuwa alikuwa akitamani siku moja aitwe timu ya Taifa.

CHOVE NI NANI

Alianza soka pale Tukuyu Stars, alipoanza kucheza Ligi Kuu Bara mwaka 2004, baadae akaibukia Kahama United kisha Twiga FC, Kahonga United ya Malawi na Mzuzu Medical ya huko huko.

“Kocha wa Yanga, Mmalawi Jack Chamangwana (marehemu) alikuja kufanya usajili wa kiungo James Chilapondwa na beki Wisdom Ndlovu, akanifuata akaniambia nasikia wewe ni Mtanzania na nimekuona ni kipa mzuri, akajitambulisha na msimu wa 2007 hadi 2009 nikasaini Yanga.”

Baadae mwaka 2009 Chove aliibukia Prisons kabla ya kwenda Kiyovu ‘ile yenyewe’.

AZIMIA UWANJANI

Kuna wakati alirudi Bongo akacheza Moro United nusu msimu akapata matatizo akiwa uwanjani yaliyomfanya akae nje kwa muda.

“Tulikuwa uwanja wa Chamazi tunacheza dhidi ya Villa Squad, niligongana na Nsa Job, wakati huo Nsa Job wa Villa Squad nikapoteza fahamu kabisa pale uwanjani nikajikuta hospitali,” anasema alikaa nje kwa muda na baadaye akasajiliwa na Coastal Union ya Tanga, hakukaa sana akaibukia Ndanda ya Mtwara mwaka 2014-2016 baada ya hapo akatua Dodoma FC akacheza msimu mmoja 2017 na baadae akaenda Congo.

GOLINI CHANGAMOTO

“Kiukweli changamoto zinakuwa nyingi sana, kuna wakati unaweza kujua wewe mwenyewe upo fiti na nitacheza kwa kiwango changu mwenyewe, ila ukiwa uwanjani unajikuta unacheza nje ya kiwango. Ndio maana magolikipa tunapata shutuma nyingi sana.’’

Chove anasema katika hali hiyo unaweza kufungwa goli ambalo hata hukutegemea ila watu wanaanza kukufikiria vibaya wakati hata haujausika na ubaya wowote fikra zao tu.

MECHI ASIYOISAHAU

Anasema aliposajiliwa na Yanga, kuna mechi moja walicheza na Mzizima na ile ndio mechi ya kwanza akiwa amesajiliwa ilipigwa Uwanja wa Uhuru, ndani ya dakika 15 za mchezo, alifungwa bao mbili, kwenye dakika ya 18 akatolewa.

“Kwa kweli yalikuwa mabao ya kizembe na nikafikiria watu watanionaje nimesajiliwa na timu kubwa kama Yanga, lakini mabao yale yalikuwa ya kizembe kwa sababu ya presha ya mashabiki kuwa wengi, na kama ningekuwa na nia ya kukata tamaa nadhani ningeshaishia pale maana wale mashabiki sio poa.”

KUMBE ALIKUWA STRAIKA

Kabla ya kuwa kipa alicheza kama mshambuliaji kwani alikuwa akipenda kufunga na kushangilia, alikuja kubadili namba wakati akiwa darasa la tano shule ya msingi Kiloleli Dodoma, walikuwa na mechi na wanafunzi wenzao wa shule ya Uhuru.

“Nakumbuka alikuwepo pia Athman Idd Chuji, tukacheza ile mechi na ndani ya dakika 30 tukawa tumefungwa goli kama mbili hivi, baadae yule kipa wetu kuona amefungwa goli mbili za haraka haraka akaamua kususa na ndipo nikaamua kukaa kipa, nikadaka vizuri sana, mpaka mechi inaisha ikawa 2-2.”

“Siku hiyo nilidaka sana na watu walinisifia sana, mwalimu wangu wa michezo akasema kuanzia siku hiyo nitakuwa kipa wa shule, ila nikirudi timu yangu ya mtaani kocha wangu alikuwa ananipanga kama mshambuliaji nafasi za mbele.”

MALENGO

“Malengo yangu nisiseme uongo, japo sijaenda Ulaya ila nchi karibia tatu nimecheza kwa hiyo malengo yangu kwa kucheza nje ni heshima kubwa sana, kwa mfano mimi nikienda Congo, Rwanda ama Malawi, wakiniona tu wananipa heshima kubwa kwa kweli. Maana yake kuna wakati wakongo walikuwa wanasema mimi sio mtanzania kwasababu ya ujanja ujanja na lingala najua wakawa wanasema mimi ni mkongomani.”

KUHUSU WANAE

Kwa upande wake anasema hawezi kumzuia mwanae yoyote ambaye ataonyesha nia ya kuwa na kipaji kama chake au kipaji kingine chochote, kwani ana watoto wawili mmoja anaonekana kuwa msanii na mwingine mcheza mpira.

“Mwanangu wa kwanza kamaliza kidato cha nne anapenda sana muziki, huyu wa pili nimezaa na mwanamke Mnyarwanda anapenda sana kuwa mchezaji wa mpira na yeye anasoma kulekule Rwanda, lakini shule anayosoma inajihusisha pia na masuala ya vipaji.” Chove anawataka vijana ambao wanachipukia kuwa na nidhamu na kujitambua, ili waweze kuwa kama wao au akina Juma Kaseja, Aishi Manula na makipa wengine, kwani bila ya kujitambua na nidhamu ni kazi bure.

“Wasiwaze ulaya tu, kwani hata kutoka Tanzania kwenda Uganda, Kenya ni moja ya heshima kwa mchezaji wawaze mbali ila na karibu napo panalipa pia.”