Biashara kuifukuzia Simba

Biashara kuifukuzia Simba

Muktasari:

Ligi ilisimama kwa muda katikia kupisha michezo ya kimataifa.

Dar es Salaam. Kama itashinda mechi yake ya leo, Biashara United itafikisha pointi 20 sawa na Simba, huku Mbeya City, ambayo itakuwa ugenini kucheza na Ruvu Shooting ikipambana kujinasua mkiani.

Mbeya City iliyo nafasi ya pili kutoka mwisho itaikabili Ruvu Shooting, ambayo mechi ya mwisho imetoka sare ya bao 1-1 na Mwadui, matokeo kama iliyopata Mbeya City dhidi ya Polisi Tanzania katika mechi ya mwisho.

Biashara United itakuwa na kibarua ugenini dhidi ya Dodoma Jiji, mechi ambayo kama itashinda itafikisha pointi sawa na Simba, ambayo ni ya tatu kwenye msimamo, wakitofautiana idadi mabao, huku Simba akiwa na mechi moja mkononi.

Dodoma Jiji itashuka uwanjani ikiwa na kumbukumbu mbaya ya kipigo kizito cha mabao 3-0 katika mechi yake ya mwisho dhidi ya Azam FC, huku ikihitaji ushindi ili kurejesha matumaini mapya baada ya kufungwa mechi tatu mfululizo.

Biashara iliyo nafasi ya nne kwenye msimamo ikiwa na pointi 17, itashuka dimbani ikiwa imekusanya pointi nne katika mechi tatu za mwisho baada ya kufungwa na Yanga bao 1-0, kuichapa Polisi Tanzania kipigo kama hicho na kutoka sare ya bao 1-1 na KMC.

Mechi nyingine leo ni ya maafande wa Tanzania Prisons, ambao watakuwa nyumbani kuikaribisha Mtibwa Sugar, ambayo imetoka kupoteza pointi tatu nyumbani kwa kipigo cha bao 1-0 dhidi ya Coastal Union, huku Prisons ikipata ushindi kama huo mbele ya Ihefu.


Makocha wanena

Charles Mkwassa wa Ruvu Shooting alisema licha ya kuwakosa wachezaji wake, Juma Nyosso na Shaban Msala, ambao wanatumikia adhabu, lakini hana wasiwasi na mechi hiyo.

“Wachezaji wengine wote watakuwepo na kila mmoja anatambua jukumu lake, lengo ni kupata pointi tatu na kuendelea kuwa nafasi nzuri kwenye msimamo,” alisema Mkwassa.

Kocha Francis Baraza wa Biashara United alisema wataikabiri Dodoma Jiji kwa nidhamu ya hali ya juu, lakini kwa lengo la kupata matokeo.

“Matokeo ya mechi yao ya mwisho hayatufanyi kuamini kuwa tutashinda, ingawa lengo letu ni ushindi, tutapambana kwa nidhamu na kwa nguvu zote kuhakikisha tunashinda,” alisema Baraza.

Kocha wa Prisons, Salum Mayanga pia aliahidi ushindi katika mchezo huo wakipigia hesabu ya pointi tatu ili kufikisha 18, kauli sawa na iliyotolewa na kocha msaidizi wa Mbeya City, Joseph Wandiba, ambaye timu yake inapambana kujinasua mkiani ikiwa na pointi 7.

_______________________________________________________

 By Imani Makongoro