Bangala, Kaseke wapewa kazi maalum

Thursday September 16 2021
Bangala pic
By Imani Makongoro
By Thomas Ng'itu

LICHA ya Yanga kukubali kipigo cha bao 1-0 nyumbani dhidi ya Rivers United ya Nigeria wadau wa soka wametoa maoni yao kwa kuipa mbinu wakisisitiza wakizifuata watatinga hatua inayofuata kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika.

Wadau hao wameitaka Yanga eneo la kiungo kuwa na watu wanaoweza kumiliki mpira na kupandisha mashambulizi ya haraka kwa washambuliaji wao.

Kwa mujibu wao, kwenye eneo la kiungo kucheza kwa Zawadi Mauya na Tonombe Mukoko kuliwafanya viungo wa Rivers watawale na kuwashika viungo wa Yanga waliokuwa wanashindwa kutengeneza nafasi za mabao kwa washambuliaji wao.

Wamewapigia chapuo wachezaji Yannick Bangala eneo la kiungo kutokana na utulivu wake awapo na mpira, pia Deus Kaseke ambaye ni mpambanaji anapokuwa uwanjani huku silaha yake kubwa ikiwa ni umiliki wa mpira. Bangala ana uwezo wa kucheza kama beki wa kati, pia anacheza kama kiungo na hilo alilionyesha kwenye mchezo wa Wiki ya Mwananchi dhidi ya Zanaco.

Upande wa Kaseke licha ya kukosa nafasi ya kucheza mchezo wa kwanza bado anaaminiwa kwa uwezo wake mkubwa wa kuuficha mpira na kutengeneza mashambulizi.

Kocha na nyota wa zamani wa Yanga, Charles Mkwassa alisema; “Ukiangalia mechi ya awali, Yanga ilifika golini kwa Rivers mara nyingi lakini walikosa umakini wa kufunga, kama watatulia na kuhakikisha kila nafasi wanayoipata inazaa matunda, Yanga itashinda.”

Advertisement

Kocha huyo aliyewahi kucheza, kuongoza na kuinoa Yanga kwa vipindi tofauti alisema falsafa ya Nabi iwe ni kushambulia tu na ikiwezekana atumie mastraika wawili.

Hery Morris, mshambuliaji wa zamani wa Yanga ambaye aliwahi kuichezea Prisons alisema; “Kocha asimtegemee Makambo pale mbele, ikiwezekana Jumapili awaanzishe washambuliaji wawili, binafsi naamini tutafanya vizuri na kusonga.”

Nyota mwingie wa Yanga, Makumbi Juma alisema; “Kilichopo ni kocha kuimarisha zaidi eneo la mbele na kiungo, kwenye mechi iliyopita kulionekana kuwa na makosa, wachezaji watulie na kucheza kwa maelekezo na kila nafasi watakayoipata waone ni nafasi ya dhahabu kwao, hata mabao 3-0 tutapata wakitulia na kucheza kwa nidhamu na maelekezo,” alisema.

Yanga inahitaji ushindi wa kuanzia mabao 2-0 au zaidi katika mchezo wao wa Jumapili ikiwa ugenini Uwanja wa Adokiye Amiesimaka (Port Harcourt).

Msafara wa Yanga utaondoka kesho, Makamu mwenyekiti wa klabu hiyo, Fredrick Mwakalebela alisema japo Nigeria kuna fitina za soka, lakini wamejipanga kukabiliana nazo na wanaamini watafanya vizuri katika mchezo huo na kusonga mbele.


REKODI KUIBEBA YANGA

Licha ya Yanga kupewa asilimia chache za ushindi kwenye mechi ya marudiano, rekodi tatu zinaipa matumaini timu hiyo kupindua meza na kusonga mbele ya wenyeji.

Yanga itaikabili Rivers yenye rekodi ya kufungwa mara moja kati ya mechi zake tisa za kimataifa ilizocheza nyumbani, huku Yanga ikishuka uwanjani ikiwa na kumbukumbu ya mwaka 2019 ilipopindua meza ugenini na kuichapa Township Rollers nchini Botswana.

Yanga tangu mwaka 2006, ina histori ya kubanwa nyumbani kwenye mechi tatu tofauti za Ligi ya Mabingwa ikiwamo ya Township Rollers ya Agosti 10,2019 ambayo ililazimishwa sare ya bao 1-1 na kubadili upepo ugenini.

Katika mchezo huo, Township Rollers ndiyo walianza kupata bao dakika ya 8 kupitia kwa Phenyo Serameng na Patrick Sibomana akasawazisha dakika ya 86.

Siku 14 baadae, kwenye marudiano mji Gaborone, Yanga iliichapa Rollers bao 1-0 lililofungwa na Juma Balinya na kusonga kabla ya kutolewa na Zesco United baada ya sare ya bao 1-1 nyumbani na kipigo cha mabao 2-1 ugenini.

Miaka mitatu kabla ya mechi na Rollers, Yanga iliwahi kubebwa na matokeo ya ugenini Ligi ya Mabingwa katika mechi mbili ambazo ililazimishwa sare ya bao 1-1 na APR na Ngaya Club kwa nyakati tofauti nyumbani, lakini ushindi wa ugenini wa mabao 2-1 na mabao 5-1 uliiwezesha kusonga katika hatua za awali.

Kwenye mchezo wa Jumapili, Yanga kama itapata ushindi wa bao 1-0 itatafuta tiketi ya kusonga kwa penalti, ingawa matokeo ya mabao 2-0 au zaidi yataiwezesha kusonga moja kwa moja kwenye hatua inayofuata na itaweka rekodi ya kuwa timu ya pili kuifunga Rivers kwenye uwanja wao tangu Julai 2, 2017 ilipochapwa 2-0 kwa mara ya kwanza na Club Africain ya Tunisia kwenye mashindano ya kimataifa.

Advertisement