Acheni waje! Pablo amaliza kazi

Muktasari:

  • Azam na Simba watatoa jasho kwenye mechi ya kusaka heshima na kuonyeshana umwamba. Kwa jinsi zilivyopaniana kuna mashabiki watavurugwa baada ya dakika 90 na kupitiliza zao mbio kitandani.

Unguja. KWA namna yoyote ile kuna watu hawatakuwa na mudi ya kuangalia nusu fainali ya Liverpool na Arsenal usiku wa leo.

Leo usiku nchi itasimama. Tanzania Bara na Visiwani kote macho yao yatakuwa kwenye Uwanja wa Amaan Zanzibar kufuatilia fainali ya Kombe la Mapinduzi.

Wakubwa wawili, Azam na Simba watatoa jasho kwenye mechi ya kusaka heshima na kuonyeshana umwamba. Kwa jinsi zilivyopaniana kuna mashabiki watavurugwa baada ya dakika 90 na kupitiliza zao mbio kitandani.

Azam wanataka kuwaonyesha Simba kwamba hawakukosea kuifumua Yanga. Lakini Simba na wenyewe wamepania kuonyesha mkubwa ni mkubwa tu bila kujali rekodi za kwenye mafaili ya hivi karibuni.

Simba na Azam zimekutana mara tatu kwenye fainali ya Kombe la Mapinduzi zote Simba ilifungwa.

Azam waliwang’oa mabingwa watetezi Yanga kwa penalti 9-8 katika nusu fainali baada ya kumaliza dakika 90 pasipo kufungana wakati Simba waliitoa Namungo kwa ushindi wa bao 2-0 huku wakicheza soka lililosheheni kachumbari zilizopagawisha mashabiki.

Fainali ya Simba na Azam itapigwa kuanzia saa 2:15 usiku na itakapomalizika kuna kipute cha Arsenal na Liverpool cha nusu fainali ya Kombe la Carabao kitakachoanza saa 4:45, lakini kuna watu watakuwa wamevurugwa na hawataweza kuiangalia mechi hiyo wataenda zao kulala.

Lakini kabla ya mechi ya Liverpool na Arsenal tutashuhudia mengi. Mageti yatafunguliwa saa nane mchana kwa mashabiki kuanza kuingia huku viingilio vikibaki vile vile Sh 3000, 5000 na 10000.

Ili kuhakikisha wanatwaa ubingwa huo kocha wa Simba, Pablo Franco alisema hakuna mchezaji atakayemkosa kati ya waliopo kisiwani hapa kwa ajili ya mechi hiyo na wanatarajia kuwa na kikosi kizima ukiachana na wale waliokuwa na majeraha ya muda mrefu Taddeo Lwanga na Erasto Nyoni.

“Lengo letu la kwanza lilikuwa kufika fainali hilo tumefanikiwa na sasa ni kutwaa ubingwa, nawapongeza wapinzani wetu pia kufika hatua hii naamini itakuwa mechi ngumu pande zote mbili na yenye burudani, mabadiliko yatakuwepo kulingana na mchezo wenyewe hivyo tunatarajia lolote kwenye kikosi chetu.

“Tumejiandaa kupata ushindi ndani ya muda wa mchezo na hata tukiingia kwenye penalti nina vijana wazuri pia. Tutafanya mazoezi ya mwisho leo (jana) usiku ambayo yatatupa mwanga wa namna gani kikosi chetu kiwe kwa katika mchezo huo, tunawaheshimu Azam ni timu bora, mashindano haya yametusaidia pia katika maandalizi ya michuano ya kimataifa pamoja na Ligi Kuu,” alisema Pablo

Kocha aliyeanza na mguu mzuri pale Azam, Abdihamid Moallin amesema kuna baadhi ya nyota wake atakaowakosa kwenye kwenye hiyo akiwemo Shaban Chilunda ambaye aliumia wakati wa mechi ya makundi ya michuano hiyo huku akisema wengine watatu hawakuwa fiti kiafya ila ataangalia namna itakavyokuwa kwenye mazoezi ya mwisho na kutoa uamuzi.

Moallin alisema wapo tayari kwa mchezo huo ambao wanataka ushindi ndani ya dakika 90 na si kwenda kwenye penalti kama ilivyokuwa mechi ya nusu fainali ingawa kwenye mechi za mtoano lolote linaweza kutokea.

“Tulijiandaa kwa mechi zote na tunajiandaa kwa fainali, unapokuwa kwenye mashindano unapaswa kumheshimu mpinzani na si kumuogopa. Tunawaheshimu Simba kwani ni timu kubwa na imara ina wachezaji wazuri lakini hata kikosi changu kipo imara.

“Tunatarajia utakuwa mchezo mzuri na wenye upinzani mkubwa kwani kila mmoja anapigania ubingwa huo naamini tutashinda ndani ya dakika 90 hata kama itatokea tofauti kwamba tunaingia kwenye penalti nako nyota wangu wameandaliwa vizuri kwani ni mechi ya kuhakikisha bingwa anapatikana,” alisema kocha huyo

Nyota wa Azam FC, Aggrey Morris ambaye ni nahodha mkuu na Mudathir Yahaya, nahodha msaidizi wao walitamba kuwa mechi hiyo itamalizika mapema tu kwani si mara ya kwanza timu hizo kukutana hivyo wanawajua vizuri wapinzani wao na wawili hao wamecheza fainali zote mbili za Mapinduzi Cup walizokutana na Simba, na Azam kutwaa ubingwa.

“Hakuna asiyefahamu kuwa Simba ni timu bora lakini ubora wao hauna tofauti na wetu, Simba hawawezi kutufikisha kwenye penalti tunajiamini kwenye mechi hii kuimaliza mapema tu, mechi yao ya nusu fainali pekee ndiyo walicheza vizuri na hiyo ni kwa vile walikutana na timu ambayo iliwaogopa mapema kwetu ni tofauti.

“Nimecheza dhidi ya Simba kwenye fainali hizi na tulishinda, iweje sasa tuwaogope wakati mbinu na uchezaji wao tunaufahamu, hatutashindwa na tutawatangulia kufunga na kuendelea kubeba kombe mbele yao hatufiki kwenye matuta,” alisema Morris.

Mudathir ambaye alipiga penalti ya mwisho katika mechi ya nusu fainali alisema; “Dakika 90 huamua nani mshindi lakini si kwa mechi hii dhidi ya Simba ingawa tunapaswa kuwaheshimu kwa ukubwa wao, ubingwa ni wetu maana mara zote tunazokutana kwenye mashindano haya na wao inakuwa rahisi kutwaa ubingwa na sasa itakuwa hivyo.

“Kucheza na Simba kwenye fainali za Mapinduzi Cup ni kama daraja la kubeba ubingwa tu na hatufiki kwenye penalti tena, hatuna hofu maana tumewaona Simba ni timu ya aina gani, haijalishi ilitufunga kwenye ligi ila wafahamu tu kwamba haya ni mashindano mengine na ni mtoano,” alisema Mudathir.

Beki wa Simba, Shomari Kapombe aliwahakikishia ushindi mashabiki wao na kutwaa ubingwa huo; “Tuko vizuri, yeyote na aje maana tulijipanga tangu mwanzo kuwa ubingwa ni wetu hivyo tutacheza kwa kuwaheshimu wapinzani wetu lakini tukiusaka ubingwa.”

Acheni waje! Pablo amaliza kazi

Mabosi Azam wakataa matuta

Ofisa Mtendaji Mkuu wa Azam FC Abdulkarim Amin ‘Popat’ alisema kuwa wamezungumza na benchi la ufundi pamoja na wachezaji kuwa hawataki kuona wanafikia hatua ya kupigiana matuta bali mechi imalizike ndani ya dakika 90.

“Binafsi sipendi kabisa kuona tunaingia kwenye matuta, na tumewaambia wote kuwa wahakikishe wanapata ushindi ndani ya muda wa mchezo. Penalti za nusu fainali sikuangalia hata moja iwe ya kupiga sisi ama kupigiwa maana zinatia presha sana na tunaamini haitakuwa hivyo.

“Kama viongozi tumewaandaa wachezaji wetu kiakili, kiafya na kisaikolojia wanapokwenda kukutana na Simba maana huwezi kumdharau mpinzani wako ila tumejipanga vizuri upande wetu,” alisema Popat.


Mabosi Simba wako poa

Mabosi wa Simba ambao wamekuwa wakitokea katika baadhi ya mechi zao nao wamesema wamejipanga huku Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi, Salim Abdallah ‘Try Again’ akisema ni wakati wa kubeba kombe hilo na kuanza safari ya kubeba makombe yote.

“Kama kawaida yetu timu inapofanya vizuri basi kuna jambo linafanyika hivyo tumejipanga kama viongozi kuhakikisha kikosi kinakuwa salama bila shida yoyote, mashabiki watarajie kuona mchezo mzuri baada ya wengine kutukimbia,” alisema Try Again.