Prime
ZAKA: Usajili wa Mafisango Azam ulikuwa balaa –2

Muktasari:
- Wakati Azam FC inashinda Kombe la Mapinduzi na wakati inachukua ubingwa wa Ligi Kuu, bao lilifungwa na Bocco.
TUNAINGIA sehemu ya pili na ya mwisho kwenye mahojiano na Mkuu wa Idara ya Habari ya Azam FC, Thabit Zakaria ‘Zaka Zakazi’ akiendelea kufafanua mambo mbalimbali zikiwamo rekodi na matukio yaliyoshtua ndani ya klabu hiyo tajiri, akianza na kueleza hatma yao msimu huu.
KUHUSU MSIMU HUU
“Msimu huu tulikuwa tunataka tuongeze pointi za kumaliza nazo Ligi Kuu ziwe 79, bahati mbaya matarajio yetu hayajaenda kama tulivyotarajia, kwa sababu tumekuwa tukienda vizuri kwa misimu mitatu nyuma ukipata na msimu wa nne ni bahati, huwa haitokei mara kwa mara.
“Huu ni mchezo sio hadithi ya kufikirika, kwa hiyo kuna wakati mambo hayawezi kwenda sawa. Kwa msimu huu mipango yetu ilikuwa ni kuongeza alama 10, tumeshakwama. Sasa tunachohangaikia tubakishe alama kama za msimu uliopita. Kufikia sasa tuna pointi 48 na kuna mechi saba.”

MIPANGO IMEFELI MAPEMA
“Hizi mechi saba zilizobakia tukishinda zote tutapata alama 21 pamoja na zile 48 tutakuwa na alama 69 ambazo ni sawa na za msimu uliopita.
“Ikitokea hiyo tunasema hatujapiga hatua moja mbele, lakini angalau tumebaki pale pale kuliko kurudi nyuma tushikilie kwanza hapo.”
MCHEZAJI BORA WA MUDA WOTE
“Kumekuwa na wachezaji wengi sana wamepita, lakini sio dhambi kusema John Bocco ndiye mchezaji wetu bora wa muda wote kwa sababu ya kila kitu alichokifanya kwenye timu hii. Alifunga mabao ambayo yaliiwezesha Azam kupanda daraja.”

KOMBE LA KWANZA
Wakati Azam FC inashinda Kombe la Mapinduzi na wakati inachukua ubingwa wa Ligi Kuu, bao lilifungwa na Bocco.
Tunashinda Kagame Cup bao la ushindi anafunga Bocco, hadi sasa yeye ndio mfungaji bora wa muda wote Azam FC, ameifungia jumla ya mabao 86 kwa hiyo huwezi kukwepa hilo kuwa yeye ndio mchezaji bora.

AZAM VS BOCCO
“Kwasasa yeye ni mchezaji wa watu kwa hiyo na tunamuheshimu na hatuwezi kuwa na uhusiano naye, hata sisi hatupendi mchezaji wetu awe na uhusiano na watu wengine tunamuacha awe huru kuitumikia timu yake anayoifanyia kazi.
“Endapo akiacha mpira hapo sasa maisha mengine yataendelea, lakini tangu ametoka Azam FC hajawahi kuwa huru, kwa hiyo sisi hatuna uhusiano naye wowote ila heshima yake kwetu ipo kubwa sana.”
USAJILI WA MOTO
“Zipo sajili nyingi sana zilizotingisha. Vita ya usajili wa Mrisho Ngasa ilikuwa na changamoto kubwa 2010, ya Mafisango ilikuwa balaa na Simba.
“Unajua kushinda vita ya chini kwa chini haipo katika vyombo vya habari na bahati mbaya zaidi kipindi kile mitandao haikuwa ya moto kama sasa hivi, watu wanaweza wasijue lakini vita ilikuwa kubwa kati ya Azam FC na Simba kumgombania Mafisango.
“Pia Ramadhan Singano ‘Messi’, mwaka 2015 sakata lilikuwa kubwa sana kuna vita moja pia ilikuwa kubwa ya Ramadhan Chombo ‘Redondo’, alikuwa mchezaji wa Simba, Azam ikamsajili wala hakuwa na shida kwa sababu alikuwa anamalizia mkataba wake kule, alikuja kama mchezaji huru, alisaini mkataba wa miaka mitatu, lakini
baada ya miaka miwili akasema kamaliza mkataba anataka kurudi Simba, ile vita ilikuwa ni kubwa sana.
“Kwa sababu wakati anatoka kuja Simba walikuwa wawili yeye na Jabir Aziz ‘Stima’, mwenzake anamuuliza ‘Redondo tumekuja siku moja tumesaini miaka mitatu mimi na wewe bado mkataba haujaisha.’
‘Siku nikija kusema ilivyokuwa kwa namna ambavyo Redondo aliondoka Azam kwenda Simba, inaweza kutetemesha nchi. Ilikuwa vurugu kubwa, ilitumika nguvu ya nje ya mpira kufanikisha usajili huo.”

KUHUSU FEI TOTO
“Moja kati ya usajili mwepesi tulioufanikisha ni wa Feisal Salum kwa sababu alishamalizana na klabu yake kazi yetu ilikuwa ni kumsajili tu.
“Hayo mengine yalikuwa maneno tu ya mtandaoni, kwa sababu shida ilikuwa ni Fei na Yanga, baada ya matatizo yote Rais.Samia Suluhu, akatoa neno na sisi tukajaribu na tukampata ni siku moja tu.
KUHUSU DUBE
“Moja kati ya wachezaji waliotusumbua sana ni Prince Dube, alikuwa mtu mpole mwema wala hakuwa na shida, akapata majeraha akatulia benchi.
“Alikuja hapa 2020 akasaini mkataba wa miaka miwili, kabla haujaisha akaongeza tena mwili, 2023 akaongeza tena wakati huo alibaki na mwaka mmoja.
‘Baada ya raundi ya kwanza msimu uliopita, tukatakiwa kwenda kucheza na Prisons ila hakwenda kwa sababu ya majeraha ambayo aliyapata kwenye mchezo dhidi ya Simba.
“Ghafla akaomba kuondoka na sisi tukamruhusu alivyoomba, tukamwambia akafanye mkataba unavyotaka, lakini haya mengine ni kama kuruka kwa maharage tu.”
AMTAJA AHMEDY ALLY NA ALLY KAMWE
“Hawa ni kama ndugu zangu, kwani kabla ya hivi vyeo sisi tulikuwa marafiki na nilifanya nao kazi Azam Tv, kwa hiyo ni wadogo zangu.
“Ukweli tunasaidiana katika mambo mbali mbali ya kimaisha ushauri na kadhalika, hizi nyingine ni mbwembwe za kunogesha kazi ila tunaheshimiana sana.”

BATO LA YANGA
Wengi wanasema Azam inakaza dhidi ya Yanga, lakini inapocheza na Simba huwa unalegeza uzi. Hapa Zaka anafafanua akisema sio kweli, huku akitaja na rekodi za timu hizo mbili.
“Ni kati ya misemo na imani za hovyo, bahati mbaya mpira wa Tanzania wanawaza Simba na Yanga na kila mtu anakuweka anapopata.
“Simba ilipopanda ikakutana na Simba na kuwafunga 2-0, dhidi ya Yanga tukapiwa 3-0, raundi ya pili na Wekundu tukafungwa 3-0 mpaka kocha akafukuzwa.
“Msimu wa pili tulifungwa mechi zote mbili na Simba, unaofuata tukawafunga baada 2011/12 ikaja sare na uliofuata tukapoteza.
“Msimu wa 2012/13 Azam ikafungwa na Simba na ikafukuza kocha tena na kusimamisha wachezaji wa nne, kwa sababu ya hao hao Simba, halafu leo unasemaje inawalegezea, hayo ni maneno tu.
“2019 Yanga anatufunga 3-2 ilikuwa mechi ya kirafiki sana, haikuwa ngumu, nyingine 2015 Azam ilishinda 2-1 ulikuwa mchezo wa wazi, tuliwahi kucheza na Simba mpaka mchezaji akaumia na watu wakadhani amekufa kwa sababu ya ugumu.”