ALI DIA: Aliigiza binamu wa Weah, akasajiliwa Southampton

Muktasari:
- Hili lilikuwa ni tukio la mchezaji Ali Dia ambaye alijiita kuwa mpwa wa mchezaji wa zamani wa AC Milan, George Weah na kwa kutumia jina hili aliweza kudanganya timu kadhaa na akafanikiwa kwa Southampton ambayo iliingia katika mtego wake na kumsajili.
SEPTEMBA 03, kila mwaka ni siku ya majonzi na ya kuchekesha kwa wapenzi wa mpira wa miguu duniani. Siku kama hiyo mwaka 1996, lilitokea tukio linaloendelea kuishi hadi sasa katika historia za mchezo huu.
Hili lilikuwa ni tukio la mchezaji Ali Dia ambaye alijiita kuwa mpwa wa mchezaji wa zamani wa AC Milan, George Weah na kwa kutumia jina hili aliweza kudanganya timu kadhaa na akafanikiwa kwa Southampton ambayo iliingia katika mtego wake na kumsajili.
Kocha wa Southampton kwa wakati huo Graeme Souness, ambaye kwa sasa ni mchambuzi, alipokea simu kutoka kwa mtu aliyejinasibu kuwa ni Weah na kumwambia kuna mchezaji mzuri anaitwa Dia ambaye amewahi kucheza timu ya taifa ya Senegal, hivyo ingefaa ikiwa angemsajili.
Souness, alishawishika na akaamua kumsajili Dia kwa mkataba wa mwezi mmoja ambao hadi leo umeweka historia yakuwa usajili mbovu zaidi kuwahi kutokea katika historia ya EPL. Fuatilia hapa visa na mikasa vya mchezaji huyu ambaye alidanganya kila kitu hadi kufanikiwa kusajiliwa na kucheza Ligi Kuu England licha ya kwamba aliwahi kucheza timu za madaraja ya chini ambako pia hakuwa anapata nafasi.

MAKOCHA WALIPONEA KUTAPELIWA
Souness hakuwa meneja pekee aliyepokea simu kutoka kwa mtu aliyedai kuwa George Weah. Harry Redknapp, ambaye wakati huo alikuwa kocha wa West Ham, amesimulia jinsi alivyopokea pendekezo kama hilo la kumsajili Dia kwa njia ya simu, ingawa hakuyapa uzito mkubwa.
"Alinipigia nikiwa kwenye uwanja wa mazoezi, alisema yeye ni George Weah, akasema, ‘Binamu yangu ni mchezaji mzuri, nimeiona timu yako, ni timu nzuri lakini mnahitaji mfungaji wa mabao’. Nikawa namjibu, ‘Aaah, sawa George, asante’. Nilidhani ilikuwa ni utani tu,"anasema Redknapp ambaye anadai hakuvutiwa na ofa hiyo.
Kocha wa Gillingham Tony Pulis naye alipokea simu kama hiyo na alidanganyika kiasi cha kumruhusu Dia kufanya majaribio, lakini baada ya kumuona akiwa kiwanjani Tony anasema alikuwa ni mchezaji wa hovyo kuwahi kumshuhudia.
Pulis anasema alishaanza kupata wasiwasi kwani alishangaa ni jinsi gani Weah angeweza kujua kuhusu klabu hiyo ndogo.
Mtu huyo aliyejiita Weah pia alipiga simu kwenye timu ya Port Vale, ambao nao pia wakampa Dia nafasi katika mechi ya kikosi cha akiba dhidi ya Middlesbrough. Hakufanya vizuri.
Souness, hata hivyo, alidai kuwa ilikuwa lazima asikilize mapendekezo yake kutokana na ukubwa wa mtu kama. Dia hakusainiwa kwa mkataba wa miaka mingi wala thamani kubwa, lakini alikubaliwa rasmi kama mchezaji wa Ligi Kuu ya England, na hata alipokea kiasi fulani cha malipo ya usajili.

UKWELI ULIVYO
Wakati Souness anaidhinisha usajili wa Dia, mtu aliyepiga simu kujitambulisha kama Weah alidai kuwa mchezaji huyo alicheza naye pamoja katika kikosi cha Paris Saint-Germain, jambo ambalo halikuwa na ukweli.
Timu aliyokuwa akiichezea kabla ya kujiunga na Southampton ilikuwa Blyth Spartans ambayo ilikuwa ikishiriki madaraja ya chini, katika timu hiyo aliweka historia kwa kuwa mchezaji wao mweusi wa kwanza kabisa, ingawa alicheza mechi moja tu, akiingia kama mchezaji wa akiba dhidi ya Boston United.
Ingawa Dia alikuwa amewahi kucheza kwenye ligi za chini za soka nchini Ufaransa, hakuwahi kuvalia jezi ya timu ya taifa wala kuchezea PSG, tofauti na madai ya 'Weah'.
Vyanzo mbalimbali vya utapeli huo vimeripotiwa; baadhi wanadai kwamba ilikuwa ni rafiki wa Dia aliyekuwa akijifanya kuwa Weah, wengine wanasema ilikuwa kazi ya wakala wake. Pia kuna taarifa zinazodai kwamba Dia mwenyewe ndiye aliyepiga simu, akiwa ameiga lafudhi na kujifanya kuwa Weah.

ILIKUWAJE BAADA YA KUSAJILIWA
Wakati anasajiliwa mambo hayakuwa yakienda vizuri kwa Southampton na ilikuwa karibu kushuka daraja msimu mmoja nyuma, wakinusurika tu kwa tofauti ya mabao ya kufunga na kufungwa, huku Manchester City wakishuka daraja badala yao.
Souness aliteuliwa kuwa kocha katika dirisha la majira ya kiangazi mwaka 1996, lakini alianza msimu kwa matokeo ya kusuasua ambapo Saints walishinda mechi tatu pekee kati ya 13 za mwanzo. Kisha, Novemba, Dia alisajiliwa na alikuwa amepangwa kucheza mechi ya kikosi cha akiba ili benchi la ufundi liweze kutathmini ubora wake. Hata hivyo, mvua kubwa ilisababisha uwanja kulowa sana, na mechi ikafutwa.
Licha ya kutovutia mazoezini, Dia alijumuishwa kwenye benchi kwa ajili ya mechi dhidi ya Leeds Novemba, 23, mwaka huo kwa sababu ya majeruhi waliokuwa wameathiri kikosi kikubwa cha wachezaji. Na wakati nyota wa timu, Matt Le Tissier, alipopata jeraha, Dia aliitwa kutoka benchi.
Aliingia na kucheza kwa dakika 53 kabla ya yeye mwenyewe kuomba kutoka na Le Tissier anakumbuka kuwa Dia alikuwa “mbovu kupita kiasi”, huku Souness akieleza kuwa kumuona akicheza vibaya kiasi hicho “ilikuwa kama mtu anampiga yeye teke sehemu nyeti.”

ALIVYOJITETEA
Hata hivyo, Dia alijitetea na kudai hana hatia. Baada ya tukio hilo, alisisitiza kwamba hakuwa “tapeli” na kudai kuwa ni wakala wake ndio aliyekuwa akijifanya kuwa George Weah alipokuwa akizungumza na timu mbalimbali. Kwa upande wake, Souness alisisitiza kwamba hakudanganywa, akidai Dia alikuwa mchezaji wa kimataifa, lakini ukweli ni kwamba hakuwa hivyo, na hakuna rekodi yoyote inayoonyesha kuwa aliwahi kuichezea timu ya taifa.
Alidumu kwa siku 14 katika mkataba wa mwezi mmoja aliosaini ambao na baad ya kiwango alichoonyesha katika mechi moja tu, Southampton ilivunja mkataba wake. Desemba mwaka huo huo, Dia alijiunga na timu ya madaraja ya chini ya Gateshead iliyoko England. Wakati huo, alieleza kuwa uhamisho wake kwenda Southampton ulikuwa ni “kutoelewana.”
Hata hivyo, alidai pia kuwa aliwahi kuichezea Senegal na kufunga bao katika mechi ya kufuzu Kombe la Dunia jambo ambalo halikuwahi kutokea. Inaripotiwa kuwa Dia alipata Pauni 2,000 kutokana na muda wake aliokuwa akiitumikia Southampton.
"Nachukuliwa kama tapeli na mchezaji asiye na kiwango, lakini mimi sipo hivyo, na ninakusudia kuthibitisha kuwa watu wamekosea. Ni wazi kuwa nimesikitishwa na kutofanikisha kucheza Ligi Kuu England kwa muda mrefu."

ALIPOTEA KWA MUDA
Ingawa ripoti zinadai kuwa Dia alijiandikisha kusoma katika Chuo Kikuu cha Northumbria baada ya kuondoka Gateshead, haijulikani kwa uhakika yuko wapi sasa. Mwaka 2016, alihojiwa na tovuti ya Bleacher Report na wakati huo alikuwa akiishi London, ingawa alikuwa na nia ya kuhamia Qatar.
Hata katika mahojiano hayo, uongo uliendelea kujitokeza, kwani Dia alidai kuwa alifanya mazoezi na Southampton kwa zaidi ya mwezi mmoja, akavutiwa na benchi la ufundi, ndipo akajumuishwa kwenye kikosi kilichocheza dhidi ya Leeds. Hata hivyo, sio Souness wala mchezaji yeyote wa Southampton wa wakati huo waliokubaliana na hilo.
Hata hivyo, Dia ameacha urithi katika soka kupitia kwa mwanawe, Simon, ambaye ameendeleza taaluma ya soka na kucheza katika nchi mbalimbali duniani. Kwa sasa anachezea klabu ya Bangkok katika Ligi Kuu ya Thailand, baada ya awali kuchezea Valenciennes na Amiens nchini Ufaransa, pamoja na timu za Bahrain, Ubelgiji na Qatar.
Simon hajawahi kudai kumfahamu George Weah ili kupata uhamisho kama ilivyokuwa kwa baba yake na kwa sasa akiwa na umri wa miaka 32, ameendelea kupambana katika soka.
MASOMO NA MAISHA BAADA YA SOKA
Dia ambaye ni raia wa Senegal aliyezaliwa jijini Dakar mwaka 1965 alihamia Ufaransa na kujiunga na timu ya Beauvais mwaka 1988, baada ya kucheza timu kadhaa nchini Senegal.
Baada ya soka alienda kusoma biashara katika Chuo Kikuu cha Northumbria kilichopo Newcastle, na alihitimu mwaka 2001. Baadaye alipata shahada ya Uzamili katika Utawala wa Biashara (MBA) kutoka Chuo Kikuu cha San Francisco State mwaka 2003. Baada ya kumaliza masomo, Dia alihamia Qatar ambako alifanya kazi katika sekta ya biashara. Hii inaonyesha kuwa, licha ya historia ya ajabu katika soka, Dia aliweza kujipanga upya na kujenga maisha mapya katika taaluma ya biashara.