Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Yassin: Mzize kaachiwa mikoba na Mayele

Muktasari:

  • “Ni mataifa mengi yamewashusha mastaa kibao ambao wanakuja kucheza soka la Tanzania. Wengi ni bora ukisema niwaorodheshe hatutamaliza leo, ila nakiri kuwa mimi nimeshuhudia vipaji vingi mno.”

“LIGI yetu (Kuu Bara) inakua msimu hadi msimu. Inatufanya tukutane na nyota wenye vipaji vikubwa na wanakuja na kutuacha, lakini uondokaji wao umekuwa ukiitangaza Tanzania kwa ubora.

“Ni mataifa mengi yamewashusha mastaa kibao ambao wanakuja kucheza soka la Tanzania. Wengi ni bora ukisema niwaorodheshe hatutamaliza leo, ila nakiri kuwa mimi nimeshuhudia vipaji vingi mno.”

Hayo ni maneno ya beki wa zamani wa Yanga ambaye kwa sasa anakipiga Tabora United, Yassin Mustapha alipokuwa akipiga stori na Mwanaspoti.

Beki huyo ameeleza mambo mbalimbali ikiwa ni pamoja na kumtaja aliyekuwa mshambuliaji wa zamani wa Yanga, Fiston Mayele kuwa ndiye staa wake bora aliyecheza muda mfupi Ligi Kuu Bara na kufanya mambo makubwa huku akiweka wazi kuwa kuna namna amemuongezea kasi Clement Mzize kupambania ufalme ndani ya Yanga.


MAYELE, MZIZE TISHIO

Tanzania imeshuhudia nyota wengi wa kigeni eneo la ushambuliaji ambao wameacha rekodi kama Emmanuel Okwi, Kipre Tchetche, Amis Tambwe na wengine wengi, lakini Yassin anamtaja Mayele kuwa ndiye bora kwake na itabaki hivyo kwa muda mrefu.

“Hajacheza muda mrefu Tanzania. Katumika kwa misimu miwili tu ameonekana, hii ni kutokana na kiwango bora alichoonyesha na kila mmoja amekiona na ameenda taifa ambalo hakuna mtu alitarajia atafanya makubwa kama anayoyafanya sasa,” anasema Yassin na kuongeza:

“Ubora wa mchezaji hauchagui taifa gani anacheza. Hicho amekithibitisha Mayele, alikuja Tanzania katutesa mabeki sasa yupo Pyramids anaendeleza ubora wake. Huyo ndio mshambuliaji hatari ambaye nimemshuhudia.”

Yassin haiishii hapo akimtaja nyota wa Kitanzania ambaye anafanya vizuri sasa ndani ya kikosi cha Yanga, Clement Mzize, kuwa ni mchezaji hatari kwa wachezaji wa ndani wanaocheza eneo hilo.

“Kwanza ukiwaangalia hao watu wawili (Mayele na Mzize) ambao nakiri kuwa ni hatari aina yao ya uchezaji ni moja. Wote wanapanda na kushuka na wana akili ndani ya 18, wana nguvu na kasi ukicheza vibaya wanasababisha hatari,” anasema.

“Mzize ni mchezaji hatari zaidi eneo la ushambuliaji licha ya uwezo wa mastaa wengi wa ndani na wa kigeni kwani namba zake zinamtambulisha.”

Yassin anasema huu ni wakati muhimu kwa Mzize kuutumia kuhakikisha anaweka rekodi baada ya misimu mingi kupita kwa wazawa kutotamba sana mbele ya wageni.

“Unajua Mzize kaanza kucheza na Mayele hakuwaka sana kaongezewa Keneddy Musonda, pia hakuwa na makali kama sasa ambavyo anacheza sambamba na Prince Dube,” anasema.

“Kuna kitu kilipandikizwa kwa Mzize kipindi wanacheza pamoja na Mayele. Ni kama alimpa hasira ya kupambana zaidi ukiangalia tangu kuondoka kwa Mkongomani huyo (Mzize) amekuwa akikuza ubora wake msimu hadi msimu, sasa anatafuta ufalme wake kwenye eneo hilo ndani ya Yanga kwa namna fulani amefanikiwa.”


TSHABALALA HANA MBADALA

Ni Mohammed Hussen ‘Tshabalala’ ambaye amekuwa akitajwa na nyota wengi wanaocheza nafasi yake kutokana na ubora anaouonyesha, na kudumu muda mrefu ndani ya kikosi cha Simba kama anavyosema Yassin.

“Mabeki ni wengi wanaocheza nafasi yangu wanafanya vizuri, lakini kwa sasa bora ni Tshabalala. Hii ni kwa sababu ni mchezaji ambaye amecheza kwa ubora zaidi ya misimu 10 bila kuteteleka tofauti na wachezaji wengine mfano hata mimi nilikuwa bora, lakini nikapotea kwa muda kutokana na majeraha hadi narudi nafanya kujitafuta,” anasema mchezaji huyo na kuongeza:

“Tshabalala amecheza zaidi ya misimu 10 kwenye timu yenye ushindani mkubwa. Kaongezewa nguvu bado yeye ndio mchezaji wa kikosi cha kwanza. Anatakiwa kupewa heshima yake, anastahili.”

Yassin anasema ubora wa wachezaji unatokana na kucheza dakika au mechi nyingi kitu ambacho kimekuwa kikifanywa na Tshabalala kila msimu na anafurahia mafanikio ya beki huyo akimtaja kuwa chachu ya wachezaji wengi kutokata tamaa na kuamini katika kujitunza.


JABU ALIMVUTA LIGI KUU

Wakongwe wanatambua ubora wa Juma Jabu enzi hizo alipokuwa anakipiga Simba - ubora aliokuwa anauonyesha uliendeleza kipaji cha Yassin ambaye ndoto yake ilikuwa ni kuwa mwanasheria.

“Nilikuwa na kipaji cha kucheza tangu nikiwa na umri mdogo. Haikuwa rahisi  kuwekeza nguvu kwenye soka ukizingatia wazazi walikuwa wanatamani kuona nazingatia shule zaidi. Nakumbuka kipindi hicho nilikuwa namtazama zaidi Jabu.

“Alikuwa mchezaji wa Simba kipindi hicho na nilikuwa namfuatilia na kuvutiwa na uchezaji wake, nafikiri ndiye aliyenifanya nicheze nafasi ninayocheza sasa licha ya kuwa na uwezo wa kucheza winga zote mbili, na nimewahi kufanya hivyo nikiwa Polisi Tanzania timu ambayo ndio iliyonitambulisha kwenye soka la ushindani.

“Sasa wachezaji ni wengi na wengi wanafanya vizuri... nafikiri kujitunza na kuamini katika kujifunza ndio siri ya mafanikio ya wachezaji wengi wanaodumu kwenye soka,” anasema beki huyo ambaye aliwahi kuonyeshwa kadi nyekundu mara moja tu enzi hizo akiichezea Polisi Tanzania.”


SOKA LIMEMPA GETO

Licha ya changamoto ya kuzuiwa na wazazi wake wakiamini katika kumpa elimu ni jambo muhimu zaidi kwake, lakini mchezaji huyo anasema kuwa kwa sasa anapata sapoti kutoka kwa wazazi wake na hii ni kutokana na kujaribu maisha na kupata vijisenti ambavyo viliwafanya waone mpira ni ajira.

“Haikuwa rahisi, lakini sasa imewezekana. Nimesoma nimeishia kidato cha nne matokeo niliyoyapata yanaweza kunipeleka chuo, na nikasomea kitu chochote lakini sasa nimeamua kuwekeza kwenye mpira,” anasema beki huyo ambaye amecheza timu tano hadi sasa ikiwemo Yanga.

“Pesa yangu ya kwanza kuishika (katika soka) ilikuwa shilingi milioni na zaidi ambayo ilinihamisha nyumbani. Kiasi nilichokipata nilipanga geto na kununua baadhi ya mahitaji, hivyo nakiri kuwa soka ndio lilinitenganisha na wazazi na kunipa akili ya kujitegemea hadi sasa, lakini bado nalidai licha ya mambo mengi niliyoyafanya. Ndoto yangu bado haijatimia naendelea kujipambania.”