Yanga gari litakolea njiani

Tuesday September 28 2021
gari pic
By Khatimu Naheka

YANGA itaingia katika msimu wake wa tano wakitafuta namna ya kufuta ukame wa miaka minne bila taji la Ligi Kuu Bara wala lile la Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC) wakiwa chini ya Kocha Mkuu Nesreddine Nabi.

Raia huyu wa Tunisia aliichukua Yanga msimu uliopita akifanikiwa kuibakishia ubora wa ushindani akikuta angalau kombe moja la Mapinduzi aliloachiwa na mtangulizi wake, Cedric Kaze aliyerejea kama msaidizi wake na juzi wakibeba Ngao ya Jamii.

Sasa makocha hao wana safari mpya ya kuunganisha nguvu kuirudishia heshima Yanga.


10 WAPYA

Kuelekea msimu mpya wamesajili mastaa wapya 10 wanaoungana na wenzao kusaka mataji ya klabu yao. Nyota hao ni makipa Diarra Djigui, Erick Johola mabeki wakiwa Djuma Shaban, David Bryson na Yannick Bangala.

Advertisement

Viungo ni Khalid Aucho, Jesus Moloko na washambuliaji Heritier Makambo, Yusuf Athuman na Fiston Mayele.


MAANDALIZI CHANGAMOTO

Katika kuelekea kuanza kwa msimu ujao changamoto kubwa kwa Yanga ni maandalizi ya mwanzo wa msimu (pre season) kutokuwa yenye kiwango kilichotarajiwa.

Yanga iliweka kambi yake ya kwanza ya maandalizi nchini Morocco lakini hata hivyo hawakuweza kuimaliza na kurejea haraka nchini.

Sababu kubwa ya Yanga kurejea ilikuwa ni viongozi wao kunusa changamoto za mlipuko wa ugonjwa wa Covid 19 ambao kwa nyakati hizo ndani ya Jiji la Marrakech ambako Yanga iliweka kambi ulikuwa unazidi kutishia usalama wa timu yao.

Kambi hiyo ya Yanga badala ya kufanyika kwa siku 15 kama ambavyo walipanga walikuta ikiishia siku tisa pekee na kikosi kurejea


WAANGUKA CAF

Katika kuonyesha changamoto hiyo Yanga ambayo ilikuwa ndio inarejea katika mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu baada ya Tanzania kupata nafasi ya kuongeza idadi ya timu shiriki katika mashindano hayo ya Afrika wakajikuta wanaishia hatua ya awali ya mtoano. Yanga ilikutana na Rivers United ya Nigeria na kwa mshtuko wakapoteza nyumbani kwa 1-0 kisha kwenda kupoteza kama hivyo jijini Port Harcourt nchini Nigeria na kujikuta wakimaliza mbio zao kwa aibu.

Hata hivyo Yanga pia itakumbukwa walikutana na changamoto ya kuwakosa wachezaji wao watatu Aucho, Mayele na Djuma ambao kama isingekuwa hilo wangeweza kuisaidia timu yao.


NAFASI WANAYO

Ligi Yanga bado wana nafasi ya kufanya vizuri huku wakijua kwamba tayari wamewaangusha mashabiki wao lakini uzoefu wa wachezaji wao lakini pia ukongwe wa timu yao.

Kikosi ambacho Yanga wamekuwa nacho kama kitapata kuunganika haraka kinaweza kuleta ushindani mkubwa wa mataji kwa msimu ujao.


MSIKIE NABI

Akizingumzia malengo yao kwa msimu ujao, Nabi anasema kitu pekee kimewangusha kabla ya kuanza kwa msimu ni maandalizi yao ya mwanzo wa msimu.

Anasema anapambana na kuhakikisha muunganiko wa timu yake unapatikana haraka lakini anaimani msimu ujao Yanga inatimu imara itakayoleta mataji.

“Hatukupata muda mzuri wa maandalizi lakini kabla ya hilo hata wachezaji wetu hawakupatikana kwa pamoja tulikusanyika kwa makundi tofauti kitu ambacho kilizidi kutupotezea muda mrefu.

Hii ni timu kubwa haitakiwi kuwa na visingizio vikubwa kitu muhimu sasa tunachofanya ni kuhakikisha muunganiko wa timu unapatikana kwa haraka.

Narudia kusema msimu ujao Yanga ina timu kubwa ambayo mimi kama kocha naona kuna mengi tutayapata niwaombe mashabiki wetu wawe wavumilivu kuna mazuri yanakuja.” anasema


MSIKIE MUKOKO

Nahodha msaidizi wa timu hiyo, kiungo Mukoko Tomombe anasema wanatambua hawakufanya vizuri katika ligi ya mabingwa lakini wanaimani kubwa na kikosi chao kwa msimu ujao.

“Jukumu letu kama wachezaji ni kuendelea kupambana yaliyotokea ligi ya mabingwa huo ni ukurasa mbaya ambao unaweza kuusoma kwenye kitabu kizuri kitu muhimu tunarudi kwa umakini mkubwa katika ligi na kuhakikisha tunafanya vizuri,” anasema. Mukoko.

Advertisement