Yaliyobamba 2021: Simba na Chama, Yanga na Mayele

MWAKA 2021 unayoyoma hivyo kwani zimebaki siku 13 kabla ya kuuaga ili kuupisha 2022.
Ndani ya siku 352 zilizopita mwaka huu kumetokea mambo mbalimbali ikiwamo vilio na vicheko kwa vigogo wa soka Tanzania - Simba, Yanga na Azam FC kutokana na baadhi ya matukio yanayowahusu.
Kuuzwa kwa nyota wa Simba, Clatous Chama na Luis Miquissone na kuwapagawisha mashabiki wa timu hiyo waliowaimba hasa walipoona chama lao linachechemea katika mechi, huku watani wao - Yanga wakitamba na usajili wa kishindo wa kina Djuma Shaban, Jesus Moloko na Fiston Mayele.
Mwanaspoti linakuletea matukio yaliyozikumba timu hizo kubwa 2021 jinsi yalivyowaliza na kuwapa furaha mashabiki wao.
CHAMA NA LUIS
Kuuzwa kwa wachezaji hao walioipa mafanikio makubwa Simba msimu uliopita ikiwamo kuifikisha robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika kuliwavuruga wana Msimbazi. Chama na Luis ndio waliokuwa roho ya Simba katika mechi za ndani na kimataifa na kuirahisishia kubeba taji la Ligi Kuu kwa mara ya nne mfululizo na Kombe la ASFC mara mbili.
Kila Simba ilipokuwa ikiyumba mashabiki walielekeza vilio kwa uongozi na kuhoji ilikuwaje wakawauza wakati waliendelea kuhitajika, licha ya kwamba mabosi wao walisajili majembe mengine ya maana akiwamo Peter Banda, Sadio Kanoute, Duncan Nyoni na Ousmane Sakho.
LIGI YA MABINGWA
Simba ililia hapa baada ya matarajio ya kutinga robo fainali Ligi ya Mabingwa kushindwa kutimia kwa kuondoshwa na Jwaneng Galaxy ya Botswana kwa jumla ya mabao 3-3, Galaxy wakibebwa na bao la ugenini - Dar es Salaam.
Hata watani zao Yanga walilia baada ya kuondoshwa katika hatua ya awali ya michuano hiyo na Rivers United ya Nigeria na kujikuta wakiangukia pua baada ya kufungwa nyumbani na ugenini - bao 1-0.
FAINALI - FA (KIGOMA)
Mchezo huu Simba ilifurahi kama bingwa mtetezi huku Yanga iliyokuwa na matumaini kibao ikipoteza. Ilikuwa fainali ya aina yake ambayo Simba ilihitaji matokeo baada ya kutoka kupoteza mchezo wa watani kwa kufungwa 1-0 hivyo nyota wake walipambana kupata matokeo na walifanikiwa.
NYOTA AZAM
Uongozi wa Azam umeifanya timu kutaabika kutokana na matokeo inayovuna baada ya kuwasimamisha nyota wake Mudathir Yahya, Aggrey Morris na Salum Abubakar ‘Sure Boy’ kwa madai ya utovu wa nidhamu. Umuhimu wa nyota hao kikosi cha kwanza umeifanya timu hiyo itaabike kupata matoke kisi cha Kombe la Shirikisho kutolewa hatua ya awali.
DJUMA, MANYAMA
Djuma Shabani ni moja ya mastaa toka DR Congo katika klabu ya AS Vita aliyekuwa akitolewa macho na Simba ili kumnasa.
Hata hivyo ni Yanga waliocheka baada ya kunasa saini yake, huku Simba wakiachana naye kwa kuzidiwa kete na wapinzani wao.
Azam FC iliwapiga na kitu kizito Simba na Yanga kwa Edward Manyama waliyekuwa mawindoni kunasa saini yake akitokea Ruvu Shooting.
Simba ililizwa katika usajili huo kwani licha ya Azam FC kumtangaza hata Simba walipigwa changa la macho. Baada ya sintofahamu Yanga ilijiweka kando na kuachana naye licha ya kuwa kwenye rada.
NGAO YA JAMII
Yanga ilicheka vilivyo baada ya kuwapokonya Simba taji la kwanza kati ya matatu waliyokuwa wanayashikilia - Ligi Kuu, FA pamoja na Ngao ya Jamii.
Ni Fiston Mayele aliyewalaza mashabiki wa Simba na jezi zao kutokana na matumaini waliyokuwa nayo awali, huku wa Yanga wakitamba siku hiyo.
UBINGWA LIGI KUU
Simba ilicheka baada ya kuutetea ubingwa wa Ligi Kuu Bara mara nne mfululizo.
Simba imetamba miaka minne mfululizo ikitwaa taji hilo. Hata hivyo haijulikani nini kitafuata msimu huu kwani watani zao - Yanga wako njema.
MAJERAHA
Simba imepata pigo baada ya nyota wao muhimu kikosi cha kwanza Thadeo Lwanga na Chris Mugalu kuumia majeraha ambayo yatawaweka nje muda mrefu.
Mugalu anasumbuliwa na nyama za paja huku Lwanga aliumia goti - majeraha yanayowaweka nje kwa muda mrefu.
Hata Azam FC wameteseka juu ya mshambuliaji wao mahiri, Prince Dube ambaye aling’ara vilivyo msimu uliopita akiwania kitu cha dhahabu.
Lakini majeraha yalimuweka nje ya uwanja muda mrefu licha ya kurejea majuzi na kuupiga mwingi.
Yanga nao wamelia baada ya mshambuliaji Yacouba Sorgne kuumia goti na kufanyiwa upasuaji jeraha ambalo litamuweka nje ya uwanja kwa miezi mitano.
BASI LA AZAM
Basi aina ya Mercedes Irizar ambalo Azam FC imelinunua Afrika Kusini ndilo habari ya mjini katika medani ya soka nchini.
Thamani kubwa ya basi hilo na muundo wake wa kifahari ilizua gumzo kutokana na aina ya mapokezi iliyopata katika maeneo mbalimbali ilikopita.
Wakati Azam wakicheka na basi, Simba ilipata mabasi matatu ya timu ya vijana, wanawake na timu kubwa kutoka Africarriers.
KIPIGO YANGA
Mwaka huu uishe tu kwani umekuwa kilio kwa Azam FC baada ya kutembezewa kichapo na Yanga katika Uwanja wa Mkapa.
Yanga waliitumbua Azam FC mabao 2-0 katika mchezo wa Ligi Kuu mabao yakifungwa na Fiston Mayele na Feisal Salum ‘Feitoto’.
MATAMASHA
Katika matamasha wote Simba Yanga waliondoka na majonzi licha ya kuyaandaa wenyewe na kualika timu kutoka nje ya nchi.
Yanga ilicheza na Zanaco katika mchezo wa kujipima nguvu kwenye kilele cha wiki ya Wananchi na kujikuta ikiangukia pua baada ya kulizwa kwa kufungwa mabao 2-1.
Na watani zao - Simba walitoka kinyonge Simba Day baada ya kufungwa 1-0 na TP Mazembe.