Prime
Staa Simba: Koti 'lilificha' pasipoti, chupuchupu niachwe Arabuni

Muktasari:
- Timu alizopitia Majimaji (2009-2011), Yanga (2011-2013), Mtibwa Sugar (2013-17) na Simba (2017/18), Ndanda (2018/19) na akarejea tena Mtibwa 2019/20 na kwa mara ya mwisho alikuwa na Ihefu FC.
KUNA mikasa inapomtokea mtu hubaki akiduwaa, akiwaza na kuwazua. Hivi umewahi kufikiria itakuwaje ukijikuta huioni pasipoti yako mfukoni ukiwa katika nchi ya kigeni na tena kwenye uwanja wa ndege ukitakiwa kuondoka? Achana na nchi zinaounda Jumuiya ya Afrika Mashariki kama Kenya, Uganda, Rwanda, Sudan Kusini, Burundi na DR Congo ambako unaweza kusikilizwa na kueleweka.
Lakini, suala kama hilo likukute kwenye nchi ya Kiarabu katika zama hizi ambazo ishu ya usalama na mambo ya uhalifu kila nchi inayatilia mkazo kuliko kawaida. Hata hivyo, kipa wa zamani wa Simba, Said Mohammed maarufu kama Nduda ana simulizi flani hivi inayoweza kukushangaza alivyochomoka katika mikono ya maofisa uhamiaji wa Misri na hatimaye akarejea nchini.
Kilichomuokoa Nduda ni ukweli kwamba wakati anakutana na mkasa huo alikuwa na kikosi cha timu ya taifa (Taifa Stars) kilipokuwa nchini humo kwa mchezo wa kimataifa.
Mkongwe huyo anasema wakati huo anacheza Mtibwa Sugar msimu wa 2013-2017 kiwango chake kilikuwa juu na alibahatika kwa nyakati tofauti kuzichezea timu za taifa za chini ya miaka 17, 20 na 23 pamoja na ile ya wakubwa yaani Taifa Stars ambayo ilikwenda Misri kucheza dhidi ya timu ya taifa ya nchi hiyo.
"Nilikuwa nimevaa koti sikujua kama lilitoboka mfuko. Ulifika muda wa kukaguliwa pasipoti nikawa siioni, nikahisi labda Kelvin Yondani (mchezaji na nahodha wa zamani wa Stars) kaificha maana alikuwa ananiambia 'shauri yako ukifanya mzaha unaachwa'... nikawa nimemkomalia, ila baada ya kuona hadi wanaenda kupanda ndege (siioni) ndipo akili ikanikaa sawa na kuamini Yondani hajaichukua," anasema Nduda na kuongeza:
"Nikaja kuambiwa na wasimamizi wa uwanja wa ndege kwamba inabidi niende Ubalozi wa Tanzania (nchini humo) nikasubiri jambo langu kushughulikiwa...nikaanza kuwaza nitaishi vipi? Akili yangu ikavurugika, wakati navua koti pasipoti ikadondoka chini niliiokota na kukimbilia sehemu ya kukaguliwa kisha nikaruhusiwa kuondoka na wenzangu."
Mchezaji huyo anaendelea kusimulia: "Baada ya kupanda ndege kila mtu akawa anacheka, Yondani akasema mzeebaba sijui ungefanyaje, nikawa mnyonge kwenda kukaa kwenye siti yangu, hicho kitu sitakaa nikisahau katika maisha yangu."
Baada ya hapo Nduda alijiunga na Simba ambako alicheza na kuonyesha uwezo mkubwa katika kikosi hicho cha Msimbazi.

SABABU KUONDOKA SIMBA
Kipa huyo anasema akiwa Simba maisha ya kambi, kuishi na wachezaji, viongozi na baadhi ya watu katika benchi la ufundi yalikuwa mazuri, lakini ishu ngumu kwake ilikuwa kwa kocha wa makipa ambaye hakutaka kumtaja jina kuwa sababu ya kuondoka Simba.
"Kocha Patick Aussems na msaidizi wake Masoud Djuma walikuwa wananikubali sana, ila kocha wa makipa alikuwa ananifuata kwa siri na kuniambia maneno ya kunikatisha tamaa. Nakumbuka kuna kiongozi mmoja mkubwa akawa anahoji kwa nini Nduda hachezi wakati anaonyesha uwezo na aliniuliza mimi pia nikamwambia, ikabidi achunguze na akaujua ukweli," anasema kipa huyo.
"Mechi ya Mei 19, 2018 tulifungwa bao 1-0 na Kagera Sugar mfungaji alikuwa Edward Christopher dakika 85 mbele ya Rais Hayati John Magufuli. Nilipewa taarifa ya kudaka mchezo huo saa sita mchana. Kuna wachezaji walinipa moyo wa kwenda kupambana mmojawapo alikuwa Emmanuel Okwi hadi aligombana na huyo kocha kwamba anayofanya siyo sahihi.
"Kabla ya siku ya mechi usiku kocha huyo aliniambia sitakuwa sehemu ya mchezo atadaka Aishi Manula kwa sababu anashindania clean sheet na Razack Abarola aliyekuwa kipa wa Azam, nikaona ni sawa, akili yangu nikajua nitakuwa jukwaani kumbe alikuwa ameishaambiwa na Aussems kwamba mimi ndiye nidake mechi hiyo.
"Mechi nyingine ilikuwa dhidi ya Lipuli, Manula alifiwa sikumbuki na nani, hivyo kocha mkuu wa timu akaniambia nitadaka. Ajabu kocha wa makipa akampigia simu Aishi arudi haraka kambini, akaja tena kuniambia nimuachie adake kwa sababu ya kupambania clean sheet. Sikuona ubaya mwenzangu afanikiwe hilo. Namna alivyokuwa anafanya huyo kocha ndio kitu kilikuwa kinaniumiza.
"Kocha Djuma aliniambia Manula atapumzika hivyo nitadaka Kombe la Mapinduzi, nikawa nimejiandaa kwenda kule kocha yuleyule wa makipa akaniambia mechi hizo anatakiwa adake Manula, nikabeba begi langu na kuondoka kurudi Dar es Salaam. Baada ya hapo nikawaomba viongozi kuvunja mkataba wa mwaka mmoja kisha nikaenda kujiunga na Ndanda FC. Nakumbuka nilipishana na Deogratus Munishi 'Dida' kipindi hicho akawa ametoka Afrika Kusini."
Nduda anasema kuna wakati wachezaji wanapitia mambo magumu, lakini wanakosa pa kusemea na kuacha watu wawashambulie katika mitandao ya kijamii.
Anasema kiuchumi ni ngumu kusema kanufaika pa kubwa kuzichezea Simba na Yanga kutokana na kuwa chaguo la pili, kwani alipata pesa za kawaida
"Yanga nilikuwa chaguo la tatu, kipa namba moja alikuwa Yaw Berko namba mbili Shaban Kado. Simba namba moja alikuwa Manula bado, hivyo isingekuwa rahisi kupata mafanikio makubwa ingawa nina mji wangu, namiliki gari, vitu ambavyo ni vya kawaida sana," anasema.
Anasema ukicheza Simba na Yanga mchezaji unaondoka na jambo moja kati ya mawili yaani heshima au aibu, akisema hayo huja iwapo ulifanya mambo makubwa na ukawakosha mashabiki wa timu husika au ukacheza lakini ukaishia kutowakosha.
Lakini, kwa Nduda pia anasimulia rekodi iliyobaki kama mfano kila inapofika mechi za dabi akisema: "Mwaka 2012 nikiwa Yanga tulifungwa na Simba mabao 5-0. Kila inapofika mechi ya dabi natolewa mfano hadi leo, Berko alifungwa bao moja mimi nilifungwa mabao manne ...naonekana nilikuwa kipa mbovu, ila hawawezi kujua kilichokuwa nyuma ya pazia."

KUKIMBIA MECHI YA SIMBA
Nduda anasema wakati anaitumikia Majimaji ya Songea aliyokuwa amejiunga nayo 2009-2011 mechi ya mwisho ya kufunga msimu dhidi ya Simba alikuwa anategemewa kudaka kama kipa namba moja kutokana na kiwango chake kuwa juu, badala yake akalazimika kushuhudia mchezo akiwa jukwaani.
Anasema: "Kabla ya mechi hiyo nilikuwa nimesaini mkataba na Yanga sasa uongozi wa Simba ukajua hilo, ukawaambia viongozi wa Majimaji kwamba tayari mimi ni mchezaji wa timu nyingine inakuaje nipangwe katika mchezo huo, ikabidi nikae jukwaani.
"Nikashangaa mambo yamekuwa mengi kwamba nimetoroka kambini kwa sababu nimechukua rushwa ili nisicheze mechi hiyo, lakini nilikuwa jukwaani huo ndio ukweli ambao sikuwahi kuusema popote. Simba ingefungwa mechi hiyo Yanga ingekuwa bingwa, ila ilishinda ikawa bingwa labda ndiyo maana walihusanisha matukio."
Akizungumzia ishu ya penalti ambayo hawezi kuisahau maishani mwaka, kipa huyo anasema ilikuwa wakati akiichezea timu ya taifa 'Taifa Stars' mwaka 2017.
"Kama sikosei ilikuwa mwaka 2017 ambapo Taifa Starts tulimaliza nafasi ya tatu katika michuano ya Cosafa, nilidaka penalti mbili, hivyo (matokeo) ikawa penalti Tanzania 4 -2 baada ya dakika 90 kumaliza kwa sare ya bao 1-1 kocha alikuwa Salum Mayanga... naziona bora kwa sababu niliisaidia timu kushika nafasi hiyo," anasema.

KUCHUKULIANA WANAWAKE
Kwa wachezaji suala la kuchukuliana wanawake au wanaume miaka ya karibuni limekuwa la kawaida, lakini nyuma yake pia uongo mwingi na hapa Nduda anatia neno.
"Kuna wakati watu wanaweza wakavumisha vitu ambavyo havina kichwa wala miguu. Uvumi huo umewahi kunikuta mimi wakati nipo Simba kuna binti (anamtaja jina) waliwahi kuniona naye sehemu bila kujua ni jirani yangu na rafiki wa mke wangu, wakaanza kunisema natoka naye ikumbukwe huyo dada alikuwa anahusishwa yupo kwenye mahusiano na mdogo wangu Peter Manyika Jr ambaye ukweli wote anaujua," anasema Nduda anayewataja Juma Kaseja na Shaban Kado kuwa ndiyo waliokuwa wanamvutia na kupenda uchezaji wao kabla hajaanza kucheza Ligi Kuu Bara.

JINA NDUDA
Je, unajua wapi ilikotoka a.k.a ya jina la kipa huyo la Ndunda, lina maana gani na alipewa na nani? Mwenyewe anasema
alipewa na rafiki yake wa utotoni na ilikuwa jioni moja wakiwa mazoezini wakati yupo golini anaokoa penalti, ndipo akampachika jina la Nduda ambalo kwa watu wa Tanga linamanisha pikipiki maarufu kama bodaboda.
"Nilipewa jina hilo mkoani Tanga na rafiki yangu kutokana na tabia yangu ya kuvimba nikiwa golini. Awali nilikuwa nalichukia sana, lakini kitu unachokichukia ndicho kinachovuna kwa kasi, likanipa umaarufu sikuwa na namna zaidi ya kukubaliana nalo hadi leo nafahamika zaidi kwa jina hilo kuliko jina langu halisi," anasema.

YUPO WAPI
Nduda anasema timu ya mwisho kuichezea ilikuwa Ihefu na baada ya kupata matatizo ya kifamilia amekuwa nje ya uwanja kwa misimu miwili."Kwa sasa kila kitu kimekaa sawa nafanya mazoezi na timu za mtaani ili kujiweka fiti, nina asilimia kubwa za kucheza Ligi Kuu msimu ujao ingawa mengine namwachia Mungu mmiliki wa pumzi zetu."
Timu alizopitia Majimaji (2009-2011), Yanga (2011-2013), Mtibwa Sugar (2013-17) na Simba (2017/18), Ndanda (2018/19) na akarejea tena Mtibwa 2019/20 na kwa mara ya mwisho alikuwa na Ihefu FC.