Wembley na ugumu wa mipira ya kona

Muktasari:

KWA kawaida kinachovutia watu wengi katika mchezo wa kandanda ni kuona nyavu zinatikiswa.

KWA kawaida kinachovutia watu wengi katika mchezo wa kandanda ni kuona nyavu zinatikiswa.

Pia vipo vivutio vingine katika mchezo huu unaopendwa zaidi duniani, kati ya hivyo ni kona, chenga na wachezaji wanapougeuza uwanja kuwa ulingo wa kupigana ngumi.

Wapo wanaosema kona inahesabika kama robo bao kwa kumaanisha kila panapopigwa kona nne upo uwezekano mkubwa wa kupatikana bao.

Tukio la mchezo wa dakika 90 au unaoongezwa muda kumalizika bila kuwepo kona mbili au tatu.

Hadi leo yapo matokeo machache ya kuwepo kona ambazo ukizihesabu hazimalizi vidole vitano.

Uzoefu umeonyesha michezo mingi ya kandanda katika miaka ya karibuni huwa na wastani wa kati ya kona 10 na 12 kwa timu zote mbili zinazocheza.

Kwa mujibu wa kumbukumbu za michezo ya mashindano kuna mechi mbili tu kwenye Uwanja wa Wembley zilizomalizika bila ya kona hata moja kupatikana.

Mchezo mmoja ni wa fainali ya Kombe la FA wa Aprili, 28, 1923 kati ya Bolton Wanderers na West Ham katika Uwanja wa Wembley, London.

Mchezo huu ambao ulikuwa wa kufungua uwanja wa zamani cha Wembley uliweka historia nyingi, mojawapo ikiwa kutokuwa na kona hata moja.

Zaidi ya watu 250,000 walifurika na kukaa ndani ya uwanja na kusababisha kukawia pambano hilo kuanza.

Polisi walikuwa na kazi pevu katika zoezi la kuwatoa zaidi ya watazamaji 30,000 nje na mchezo kukawia kuanza kwa saa 1 na dakika 10.

Watu zaidi ya 900 waliumia katika vurugu hiyo ya kihistoria na baadaye mashabiki wapatao 28,000 walirejeshewa fedha walizokatia tiketi.

Mchezo ulisita mara tatu kwa vurugu kati ya dakika 3 na 5 baada ya mashabiki kuvamia uwanja na polisi kulazimika kutembeza mkong’oto na kulipua mabomu ya machozi. Timu zote mbili zilitumia ule mfumo maarufu wa mchezo wa zama zile wa 2-3-5.

Filimbi ya mwisho ilipopulizwa West Ham walibeba kombe kwa ushindi wa 2-0.

Mfalme George wa sita wa Uingereza (baba wa Malkia wa sasa Elizabeth wa Pili) ambaye alitambulika kama shabiki mkubwa wa West Ham pamoja na wengi wa wana familia yake alifanya karamu maalum katika makazi yake ya Buckingham kuipongeza timu yake ya West Ham.

Vile vile West Ham ilimzawadia kila mchezaji na kiongozi saa ya dhahabu, hii ni mbali ya medali za dhahabu walizopewa wachezaji na viongozi na Shirikisho la Soka Uingereza.

Mchezo mwingine uliomalizika kwa kutokuwa na hata kona moja ni wa Agosti 21, 2010 wa Ligi Kuu ya England kati ya Wigan Athletic na Chelsea.

Filimbi ya mwisho ilipopulizwa Chelsea waliibuka na ushindi wa mabao 6-0 na kutangazwa klabu bingwa ya England.

Lakini ipo michezo ambayo ilikuwa na kona baada ya kila dakika chache na hata kupoteza ladha ya pambano.

Miongoni mwa michezo hiyo ni wa Novemba, 13, 1965 Leicester City walipocheza na Manchester United. Leicester walishambulia sana na walimiliki zaidi mpira kuliko wapinzani na kufanikiwa kupata kona 34 wakati wenzao walipata sita.

Lakini filimbi ya mwisho ya mchezo ilipopulizwa Manchester United walitoka uwanjani na furaha kubwa wakiwa washindi wa mabao 5-0.

Katika mchezo wa Ligi Kuu ya England uliofanyika miaka nane iliyopita, Everton ilipiga kona 16 wakati wapinzani wao Sunderland walipata kona mbili tu.

Kilichowashangaza watu wengi ni kuiona Sunderland iliyosakamwa sana katika mchezo huu ikiibuka na ushindi wa bao 1-0.

Uzoefu umeonyesha kuwepo timu ziliopata kona nyingi kiasi, lakini zikashindwa kutumia hata moja kwa kujipatia bao.

Rekodi zinaonyesha Novemba, 13, 1965 Leicester City walipata kona 34 walipocheza Uwanja wa nyumbani na Manchester United.

Kila kona ilipopigwa mashabiki wa Leicester walitarajia kupata bao, lakini hadi filimbi ya mwisho wa mchezo ilipopulizwa hapakuwepo bao na matokeo ya mchezo yalikuwa ya Manchester kupata ushindi wa bao 5-0.

Kwa hakika kuuchambua uzuri wa timu ya kwa asilimia ya kumiliki mpira, kona ilizopata, chenga safi au mipira ya adhabu iliyopiga ni kama kuisifu kachumbari ya pilau iliyooza au kusifia kile kinachoelezwa katika soka kama ‘twafungwa, lakini chenga twawala’.

Matokeo ya mchezo huamuliwa kwa mabao yaliyofungwa na sio kwa mtindo wa chenga twawala, mipira ya kurusha, ya adhabu, kona zilizopigwa, kadi za njano au nyekundu zilizotolewa na mwamuzi.

Wakati umefika kwa Shirikikisho la Soka Tanzania (TFF) kwa kushirikiana na vyama vyingine vya michezo kama Chama cha Waamuzi, Waandishi wa Habari za Michezo (TASWA) kuweka kumbukumbu za aina hii ili tujuwe tulikotoka katika soka, tulipo na tunapoelekea.

Imeandikwa na SALIM SAID SALIM