Watauana kila siku fainali tu

MARA PAAP msimu umetamatika kwa upande wa Ligi Kuu Bara, lakini hata nje na kuna mechi za kuhitimisha msimu huu na balaa zito lilianzia hatua ya makundi mpaka fainali kwa upande wa Ligi ya Mabingwa Afika na Kombe la Shirikisho Afrika bila kusahau mashindano ya Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC). Hizi ndizo fainali ambazo zitaanza kupigwa wikiendi hii nje na ndani ya nchi.


KOMBE LA SHIRIKISHO (ASFC)
Katika mchezo huu Yanga na wenyeji Azam FC watamenyana, ambapo Azam iliitoa Simba katika nusu fainali kwa mabao 2-1, huku Yanga wakimalizana na Singida kwa kuwachapa nyumbani kwao bao 1-0. Fainali kati ya timu hizo iliyopangwa kufanyika Juni 3 imeahirishwa kwa sababu Yanga itakuwa na mchezo wa pili wa fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika utakaochezwa nchini Algeria.


KOMBE LA SHIRIKISHO AFRIKA
Yanga inakwenda kukutana na USM Alger katika fainali ikiwa imetoka kuilaza Marumo Gallants kwa mabao 4-1 katika mechi mbili za nusu fainali, ilhali USM-Alger ilimalizana na ASEC Mimosas katika hatua hiyo mabao 2-0 ikiwa nyumbani matokeo yaliyoiingiza fainali. Fainali hiyo itaanzia katika Uwanja wa Benjamin Mkapa Jumapili wiki hii na kumalizia Algiers, Algeria Juni 3.


LIGI YA MABINGWA AFRIKA
Katika nusu fainali ili kutinga fainali hizo, Waydad Casablanca waliitoa Mamelodi Sundowns kwa mabao 2-2 wakinufaika na bao la ugenini katika mchezo wa marudiano uliopigwa Afrika Kusini, huku Al Ahly wakiifunga ES Tunis kwa cha mabao 4-0 michezo wa kwanza wakishinda mabao 3-0 kisha wakamalizia kwa bao 1-0.


LIGI YA MABINGWA ULAYA
Barani humo kuna fainali kibao zinazotarajiwa kupigwa ili kufunga msimu huu wa mashindano ya soka kubwa ikiwa ni Ligi ya Mabingwa itakayochezwa Juni 10 kwa Manchester City na Inter Milan kukipiga jijini Istanbul, Uturuki. Timu hizo zilitinga fainali baada ya kuzifunga timu kubwa katika nusu fainali. Man City iliifunga Real Madrid kwa jumla ya mabao 5-1 katika nusu fainali mbili za michuano hiyo. Katika mchezo wa kwanza mabingwa hao watetezi wa England walitoka sare ya bao 1-1 katika Uwanja wa Santiago Bernabeu, Hispania kisha wakaifumua Madrid kwa mabao 4-0 uwanjani Etihad. Inter Milan nayo iliichapa AC Milan kwa mabao 2-0 katika mchezo wa kwanza wa nusu fanali na ule wa pili ikashinda bao 1-0 dhidi ya mahasimu wao hao wa Jiji la Milan.


FA ENGLAND
Fainali ya Kombe la FA itapigwa Juni 3 na kwa hakika sio ya kuikosa kwani itawakutanisha mahasimu wa Jiji la Manchester yaani Manchester United dhidi ya Manchester City. Timu hizo kila moja tayari ina kombe moja ililotwaa msimu huu ambapo Man United imebeba lile la Carabao na Manchester City ikinyakua Ligi Kuu England. Fainali hii itachezwa katika Uwanja wa Wembley, Juni 3. Timu hizo kila moja inafukuzia taji la pili msimu huu kwani Man City pia ipo katika fainali ya Ligi Mabingwa Ulaya.


EUROPA LEAGUE
Hii ni fainali itakayopigwa Mei 31 kati ya Sevilla na Roma itakayochezwa katika Uwanja wa Puskas Arena jijini Budapest, Hungary. Sevilla iliyoanza kwa kusuasua hatua ya makundi ya mashindano hayo iliibuka na kuing'oa Manchester United katika robo fainali ya michuano hiyo kabla ya kumenyana na Juventus katika nusu fainali. Sevilla itakuwa na kibarua dhidi ya AS Roma inayonolewa na Jose Mourinho. Kocha huyo anafahamika kwa mbinu zake hususan katika michuano mikubwa kama hiyo. Mourinho ameweka rekodi kali katika michuano ya Ulaya huku Sevilla ikiweka rekodi nzuri ya kubeba Kombe la Europa. Sevilla imeweka historia ya kubeba taji hilo mara tano.


CONFERENCE LEAGUE
Kipute cha fainali ya Conference League kitapigwa Juni 7 kati ya West Ham United ilitinga fainali kwa mara ya kwanza tangu 1976 baada ya kung'oa AZ Alkmaar katika nusu fainali iliyochezwa wiki iliyopita. Katika nusu ya kwanza West Ham United iliibuka na ushindi wa mabao 2-1 katika uwanja wa nyumbani. Katika nusu fainali ya pili West Ham ikaibuka ushindi wa bao 1-0. Fainali ya Conference League kati ya West Ham na Fiorentina itafanyika Jamhuri ya Czech katika Jiji la Prague, Czechoslovakia. Itakumbukwa AS Roma ndio iliyokuwa bingwa wa mashindano hayo msimu uliopita.


DFB-POKAL
Kule Ujerumani kuna fainali ya Pokal itakayochezwa Juni 3. Mzigoni kutakuwa na RB Leipzig itayomenyana na Eintracht Frankfurt. Wababe Frankfurt waliifunga VfB Stuttgart kwa mabao 3-2 katika mechi ya nusu fainali na kutinga fainali hizo ilhali Leipzig iliibuka na ushindi wa mabao 5-1 dhidi ya SC Freigburg.