Wanapiga soka na kusoma vitabu
Hawakukosea waliosema “usihukumu kitabu kwa kuangalia pambo la nje, kabla ya kujua kilichomo ndani.” Ndivyo yalivyo maisha ya wanasoka wengi nje ya uwanja kwani wana maisha mengine mazuri.
Wataalamu wengi wa mambo wanasema kuwa, ili uwe na maarifa ya kutosha unatakiwa kusoma sana. Ni kawaida kwa baadhi ya watu kutaja idadi ya vitabu ambavyo wamevisoma kwa mwaka, ingawa kwa wachezaji wengi wa soka ni jambo adimu.
Spoti Mikiki imezungumza na baadhi ya wachezaji kujua kama wanasoma vitabu na wamejifunza nini kupitia hilo na kwa maelezo yao wametoa somo kubwa kwa wengine.
Asilimia kubwa, wameonyesha hawataki kuachwa nyuma na ulimwengu wa wasomi ambao wanafikiria zaidi, hivyo wanahitaji akili zao kujazwa maarifa mapya kila wakati.
DANNY MRWANDA - COPCO (Uchumi)
Straika wa zamani wa Simba na Yanga, Danny Mrwanda anasema vitabu anavyovisoma vinahusu uchumi, jamii, mabadiliko ya dunia na maadili.
Ingawa ilikuwa ngumu kututajia kitabu kimoja baada ya kingine, baadhi alivyovisoma zaidi ni Think and Grow Rich kilichoandikwa na (Napoleon Hill) Lows of Success (Les Brown).
“Nimesoma vitabu vingi sana na naendelea kuvisoma, mfano kingine kinachoitwa Cultural Differences Between Africans and Americans, kilichoandikwa na Joseph Mbele, najifunza mambo mengi ambayo niliyapuza shule, ama sikubahatika kuyasoma, nje na vitabu naangalia muvi zenye mafunzo, maana siyo mpenzi wa muziki kabisa,” anasema Mrwanda anayecheza Copco ya Championship kwa sasa.
LAMBART SABIYANKA - PRISONS (Teknolojia)
Kiraka wa Prisons, Lambart Sabiyanka, anasema anapenda sana kusoma vitabu kutokana na mabadiliko ya dunia na jinsi ambavyo uvumbuzi na watu wanavyofikiri sana kufanya vitu vikubwa.
“Nyumbani kwangu nina sehemu maalumu ya vitabu, hivyo siwezi kutaja kimoja baada ya kingine ila mojawapo ni The Darkness of Dark Phychology kilichoandikwa na Erik Phill, Think and Grow Rich (Napoleon Hill),” anasema.
“Ukiachana na vitabu najifunza vitu vingi kwenye mitandao ya kijamii, angalau kuijua dunia kwa sehemu, inakokwenda, mfano niliwahi kuiona muvi fulani nadhani ilikuwa 2019, ilikuwa inaelezea ugonjwa wa covid 19 hata ilivyokuja kutokea, haikuwa picha ngeni kwangu.
“Pia nikitaka kwenda sehemu, naingia mtandaoni, nasoma sana kuijua hiyo sehemu na tamaduni zake, hata nikienda kunakuwa hakuna jipya, hivyo ni vizuri sana vijana wakapenda kusoma vitabu, kuna kitu watajifunza.”
Anaulizwa mchezaji mwingine wa Prisons, Jeremiah Juma Mgunda kama anapenda kusoma vitabu? Anajibu “Nasoma siyo kivile, ila kwenye timu yetu mpenzi wa kusoma vitabu sana na anavinunua kwa gharama hadi tunamshangaa ni Lambart.”
MEDDIE KAGERE - NAMUNGO (Maisha)
Straika mpya wa Namungo FC, Meddie Kagere anasema anapenda sana kusoma: “Siwezi kukutajia kimoja baada ya kingine, ila mimi nasoma sana mfano vya About Life na Fiction and Literature.”
JACOB MASSAWE-NAMUNGO (dini)
Kiungo wa Namungo, Jacob Masawe anasema asilimia kubwa anasoma vitabu vilivyoandikwa na wachungaji kama vya Christopher Mwakasege mfano Ndoto, Akili, Ulimwengu wa Roho na kingine cha mchungaji Eliona Kimaro kinachoitwa Kujitunza Nafsi.
“Vimenifanya nikae karibu na Mungu. Nimeamini unachoilisha akili yako ndicho kinachoitawala roho yako, lakini pia huwa nasoma vya kijamii na uchumi, vinanipa nguvu ya kuendelea kupambana kusaka maisha,”anasema.
ABDULHALIM HUMOUD - KONKOLA (Maarifa)
Kiungo wa zamani wa Simba, Abdulhalim Humud ‘Gaucho’ ambaye kwa sasa anacheza klabu ya Konkola Blades inayoshiriki Ligi Kuu ya Zambia, anasema anapenda kusoma vitabu vinahusiana na maisha, ili kuendelea kuulisha ubongo wake kujua mambo mengi kwenye dunia ya sasa.
“Dunia hairudi nyuma. Ya jana siyo ya leo, hivyo lazima akili ipate chakula kipya, vitabu vinasaidia kujua upeo wa watu wanavyofikiri mfano kitabu cha Keys for Leadership, kilichoandikwa na Dk Myles Munroe,” anasema.
ELIAS MAGURI -GEITA (Maarifa)
Straika wa Geita Gold, Elias Maguri anasema ni muumini wa kusoma sana vitabu, akiwa anasafiri, akipumzika baada ya mazoezi au mechi, akiwa mapumziko, anaamini kupitia hivyo anapata maarifa makubwa.
“Nimesoma kitabu cha Core Genius, Money Formula, cha Kiswahili Jinsi ya Kufanikiwa Nyakati Ngumu kilichoandikwa na Joel Manauka, kama kijana nina safari ndefu, lazima akili yangu ishibe maarifa yakunisaidia kutimiza malengo yangu,”anasema.
AQUILA GASPER- FOUNTAIN GATE PRINCESS (Morali)
Kiungo wa Fountain Gate Princess, Aquila Gasper anasema anapendelea kusoma vitabu vya motisha muda anaopumzika akiamini vinamsaidia kumpa morali ya kuendelea kupambana bila kukata tamaa licha ya changamoto nyingi za kimaisha.
“Japo sio mara zote, lakini nikipata muda huwa nasoma vitabu vya aina hiyo, kuna kitabu kinaitwa ‘Think Big’ ameandika Ben Carson kingine ‘Milango saba, vitabu hivyo vina maudhui yalionifanya niamini katika ndoto zangu, hata kama walionizunguka hawanielewi kwa wakati huo’,” anasema.
MUSSA MBISE - PRISONS (Maarifa)
Kipa wa Tanzania Prisons, Mussa Mbise anasema anasoma vitabu vya motisha, uchumi, mabadiliko ya dunia anataja baadhi kuwa ni Champions Cry Too kilichoandikwa na Jet Xavier, Think Big (Ben Carson ).
“Mfano hicho cha Champions Cry Too vijana wengi wanaweza wakafika hatua ya kukata tamaa hadi kutoa machozi haimanishi ndoto zake haziwezi kutimia, badala yake anatakiwa apambane zaidi ya alivyoanza jana,” anasema.
MAKA EDWARD - JKT TANZANIA (Mitindo)
Mshambuliaji wa JKT Tanzania, Maka Edward anasema anasoma vitabu vya uchumi na fasheni, kitu anachokipenda zaidi kwenye maisha yake.
“Mfano kuna kitabu kinaitwa Think Grow Rich ndani yake kinafundisha mambo mengi sana pia napenda uanamitindo, hivyo lazima nijue vitu vingi,” anasema.
GEORGE MPOLE - FC LUPOPO (Maarifa)
Straika wa FC Lupopo ya DR Congo, Mtanzania George Mpole pia ni muumini mkubwa wa kusoma vitabu kama anavyosimulia, “ingawa nasoma sana nikiwa Tanzania kimojawapo ninachokipenda ni cha maarifa zaidi kinaitwa Think Big’ ameandika Ben Carson.”
MANYIKA PETER JR - HURU (Maarifa)
Kipa wa zamani wa Simba, Peter Manyika Jr ambaye kwa sasa yupo nje kwa muda, anasema anapenda sana kusoma vitabu baadhi ni Glory Living, Burden of Freedom, Passing It On, vilivyoandikwa na Dr Myles Munroe.
“Nimeongeza maarifa makubwa sana kichwani, pia kuna mambo mengi ya kukatisha tamaa, nikisoma vitabu napata moyo wa kuendelea kupamba,” anasema.
JAMES AKAMINKO - AZAM (Uchumi)
Kiungo wa Azam FC, James Akaminko anasema anapenda sana kusoma vinavyohusu maendeleo ya kiuchumi kwani kwa maiaka ya baadaye ana ndoto ya kufanya biashara.
“Lazima nisome vitabu, kabla sijaingia kwenye biashara, ili nipate ujuzi, ingawa kwa sasa siwezi kukutajia majina yake, labda siku nyingine,”anasema.
MOHAMED IBRAHIM -PRISONS (Mapenzi)
Kiungo wa zamani wa Simba na sasa anacheza Prisons, Mohamed Ibrahim ‘Mo Ibrahim’ anasema anapenda kusoma vitabu vyenye stori za mapenzi, uchumi na jamii.
“Kuna kitabu kinaitwa A Love Story From the Heart (Terry Atkinson), My last Love, vipo vingi sana nimesoma na vya uchumi ambavyo siwezi kukutajia kwa haraka haraka,” anasema.