Prime
Kocha Simba aionya Yanga mapema

KLABU ya Simba imekuwa gumzo barani Afrika katika msimu wa 2024/25, si kwa sababu tu ya kufika fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika, bali kwa namna ilivyoweza kusimama imara licha ya kuwa na kikosi kilichojengwa upya.
Wakati wengi walitazamia kuwa ni msimu wa mpito, Simba waligeuka kuwa tishio kwa kila timu, wakicheza soka la kisasa lenye kasi, nidhamu na uimara wa kimwili ambao ulidhihirisha maandalizi mazuri nyuma ya pazia.
Katika mahojiano maalum na gazeti hili, kocha wa viungo wa Simba, Reidoh Berdien, alifungua ukurasa wa ndani wa mafanikio hayo, akieleza kwa undani falsafa ya maandalizi ya kimwili, mbinu za kisasa za mazoezi, na mchango wa benchi la ufundi chini ya kocha mkuu, Fadlu Davids, ambaye anamuelezea kama ‘mtaalamu wa soka la mipango.’€
Berdien, ambaye ni mzawa wa Afrika Kusini na mzoefu wa zaidi ya miaka 15 katika kazi ya ukocha wa viungo na sayansi ya michezo, alijiunga rasmi na Simba mwaka 2024. Tangu wakati huo, amekuwa nguzo muhimu ya maendeleo ya wachezaji, akisimamia siyo tu uimara wa mwili wa mchezaji, bali pia mabadiliko ya kifikra kuelekea ufanisi na taaluma.
Katika maelezo yake, Berdien alieleza kuwa mafanikio ya Simba hayakuwa ya bahati au kwa sababu ya wachezaji wakubwa pekee, bali ni matokeo ya mchakato wa kisayansi uliofuatwa kwa umakini mkubwa, ushirikiano wa karibu kati ya makocha, madaktari, wataalamu wa lishe na wachezaji wenyewe.
Ni mahojiano yaliyojaa mbinu za kiufundi, dira ya maendeleo, changamoto zilizoshughulikiwa kwa weledi, na pia matumaini ya kile ambacho Simba inaweza kuwa msimu ujao. Katika kila jibu, Berdien aliwasilisha picha ya timu iliyopangiliwa kisasa, timu yenye maono ya mbali, na yenye kiu ya kutawala tena kuanzia soka la ndani hadi Afrika.
Katika majibu yake, alizungumzia jinsi Simba ilivyoweza kuhimili ratiba ngumu ya mashindano, kupunguza majeraha, kukuza wachezaji na kuweka mazingira ya kitaalamu yanayovutia hata familia za wafanyakazi wa timu hiyo.
Zaidi ya hayo, alitoa mtazamo wake kuhusu soka la Tanzania na Afrika kwa ujumla, akifananisha kiu ya mafanikio kati ya wachezaji wa Kusini mwa Afrika na wale wa sehemu nyingine za bara, huku akiwashauri makocha wanaochipukia kutokata tamaa.

SIO RAHISI KABISA
Reidoh anafunguka kwa kusema kuwa mafanikio ya Simba msimu uliopita hayawezi kupuuzwa wala kuchukuliwa kuwa yalitokea kwa bahati. Anasisitiza kuwa kulikuwa na kazi kubwa ya kitaalamu nyuma ya pazia.
“Tunapaswa kujivunia wachezaji wetu na benchi la ufundi. Haikuwa rahisi. Kocha Fadlu Davids alielewa fika mahitaji ya kimwili ya mfumo wake. Aliweza kupangilia mazoezi kwa uwiano wa utimamu wa mwili. Mzunguko wa wachezaji pia ulisaidia kupunguza uchovu,” anaeleza.
MBINU ZA KISASA
Kocha huyo anaeleza kuwa timu yao haifanyi mazoezi ya kukimbia au kubeba vyuma, bali hutumia mbinu ya ‘Tactical Periodization’ ambapo alifafanua kuwa ni mfumo wa mazoezi unaochanganya mbinu na nguvu za mwili kwa pamoja, huku lengo likiwa ni ‘kucheza jinsi unavyofanya mazoezi.’€
“Katika mashindano ya CAF, tulitumia mtindo wa timu ya taifa. Tulipunguza idadi ya mazoezi lakini tukaboresha ubora. Hii iliongeza tija na ufanisi,”€ anasema.
KASI, NGUVU NA BUSARA
Katika soka la kisasa, kasi na nguvu ni mambo ya msingi. Berdien anaamini kuwa kazi ya benchi la ufundi la Simba limewawezesha wachezaji kuhimili kasi ya mechi nzima na kufanya uamuzi sahihi kwa wakati sahihi.
“Wachezaji wetu hawakimbii tu ovyo. Kila zoezi lina mwelekeo unaohusiana na mfumo wa kocha. Na kila kitu tunakipima kwa kutumia GPS ya kisasa iitwayo fitogether,”€ anabainisha.

MABADILIKO YA KIKOSI
Berdien alikiri kuwa kilichowafanya waonekane wa ajabu ni namna walivyoweza kuunganisha wachezaji wapya waliotoka katika mazingira tofauti ya mazoezi. Alieleza kuwa hawakutumia mbinu za kijeshi, bali walijikita katika mbinu za kisasa za kisoka, jambo ambalo lilivutia wachezaji.
“Wachezaji walipenda mbinu ya Fadlu. Walijituma zaidi, waliamini mfumo na walijitoa kwa moyo wote,”€ anasema.
WACHEZAJI WALIOINUKA
Alitaja majina kama Fabrice Ngoma, Yusuph Kagoma, Joshua Mutale, Mpanzu, Mukwala na Kijili, kuwa miongoni mwa waliofanya vizuri kimwili, huku Shomari Kapombe na Mohamed Hussein “Tshabalala’ wakitajwa kuwa waliodumisha kiwango cha juu kwa kucheza karibu mechi zote, klabuni na kwenye timu ya taifa.

VIWANJA NA RATIBA
Berdien anasema Simba haikuwa na janga la majeraha, na yalipotokea yalidhibitiwa na wachezaji walipona haraka zaidi. Changamoto kubwa ilikuwa ni ubovu wa viwanja na ratiba mbaya ya mashindano.
“Tulicheza mechi nyingi kwa muda mfupi, huku timu nyingine zikipumzika wiki nzima kabla ya mechi. Hiyo ilituathiri,” anaeleza.
FADLU NI MASTAA
Kocha huyo alimuelezea Fadlu Davids kuwa si tu kocha wa kawaida, bali ni mtaalamu wa soka anayeleta watu pamoja kwa kutumia mpira.
“Ana akili ya hali ya juu ya soka. Anaweka kila kitu katika muktadha wa mpira. Kazi yetu kama wasaidizi wake ni kumsapoti tu. Anafanya kazi tofauti na wengi,” anasema.
LISHE NA MALEZI BORA
Berdien anaeleza namna Simba ilivyowekeza kwenye mbinu za kisasa za kurejesha nguvu mwilini kwa kutumia ice baths, virutubisho na mpangilio wa mazoezi ya kurejesha nguvu. Alipongeza madaktari kwa kazi nzuri.
NJE YA AFRIKA KUSINI
Reidoh pia alitoa mtazamo wake kuhusu tofauti ya kisaikolojia kati ya wachezaji wa Afrika Kusini na wale wa mataifa mengine ya Afrika, akifichua kuwa ameweza kufundisha katika mataifa kama Togo, Gambia na Mali, na kugundua kuwa nje ya Afrika Kusini, wachezaji huonyesha kiu kubwa zaidi ya mafanikio.
“Wachezaji wengi wa Afrika wanataka kutoka katika mazingira yao na kujitengenezea maisha bora. Njaa yao ya mafanikio ni kubwa, na hiyo inaathiri moja kwa moja namna wanavyojitoa kwenye mazoezi na mechi,” anasema Berdien.
Anasisitiza kuwa hiyo ndiyo sababu hata Simba waliweza kufikia mafanikio kwa wachezaji wengi wapya kwa haraka kwa sababu walikuwa tayari kujifunza na kujitoa kwa moyo.
Kocha huyo hakusita kuweka msimamo wake kuhusu dhana ya maendeleo ya kimwili kuwa ni kazi ya mtu mmoja. Kwa mtazamo wake, mafanikio ya kisayansi na kimwili kwa timu yoyote yanahitaji mshikamano wa pamoja kati ya wachezaji, benchi la ufundi, madaktari na uongozi wa juu.
“Mafanikio si ya mtu mmoja. Tunawafundisha wachezaji kuwa wanapaswa kuheshimu kile wanachofanya. Lazima wafanye kazi kwa bidii lakini pia kwa akili. Mafanikio yanahitaji nidhamu, maelekezo, na ushirikiano,”€ anaeleza kwa msisitizo.

MAISHA NJE YA UWANJA
Licha ya ratiba ngumu ya soka la kulipwa, Berdien anasema amekuwa akitenga muda kushiriki shughuli za kijamii na kielimu.
Amekuwa akiendesha webinars (semina fupi za sayansi ya michezo na maandalizi ya kimwili za live kupitia website), pamoja na kushiriki miradi ya kijamii kupitia taasisi ya Simsport International.
“Ninapenda kucheza soka la timu za wachezaji watano kila upande na padel (tenisi ya uwanja mdogo uliozungushiwa nyavu pande zote). Nje ya uwanja, ninafanya kazi nyingi za kijamii na elimu ya mpira,”€ anasema.
Alifichua ameishi na kufanya kazi katika mazingira tofauti lakini Tanzania ni nchi ambayo yeye na familia yake wameipenda kwa dhati.
“Nimewahi kuwa hapa, kurudi haikuwa ngumu. Tanzania ni nchi ya watu waungwana wanaopenda soka. Mashabiki wa Simba wametufanya tujisikie nyumbani,” anaeleza kwa furaha.
SIMBA FAMILIA YA PILI
Reidoh alifunguka pia kuhusu maisha ya familia na kazi, akisema licha ya changamoto za muda na majukumu ya kazi, klabu ya Simba imemrahisishia mambo.
“Soka na familia ni maisha yangu. Kwa zaidi ya miaka 15 nimekuwa nikifanya kazi hii, lakini Simba imenirahisishia maisha yangu binafsi. Si mimi tu, familia yangu pia imepokewa vizuri na mashabiki,” anaongeza.
SINA MPANGO WA KUONDOKA
Ingawa bado yuko ndani ya mkataba na Simba, Berdien anasema kwa busara kuwa soka ni mchezo wenye mabadiliko ya haraka, lakini kwa sasa hana mpango wa kuondoka.
“Kwa sasa, nina furaha Simba. Nimebarikiwa kufanya kazi na klabu kubwa kama Sundowns na timu za taifa kama Mali, lakini hapa ni mahali salama na penye dira,” anasema.

MAKOCHA VIJANA
Kocha huyo ambaye ni miongoni mwa wataalamu wachache wa kiwango cha juu katika Afrika alitumia nafasi hiyo kuwashauri vijana wanaotamani kuwa makocha wa viungo na wataalamu wa sayansi ya michezo.
“Jifunze. Pata vyeti, soma. Hili ni eneo la taaluma, sio mazoezi tu ya misuli. Na utakataliwa mara nyingi, utapoteza mechi nyingi, lakini usikate tamaa. Ukikata tamaa umeshindwa,” anasisitiza.
Anasema elimu ni msingi wa kuelewa hata mitazamo ya makocha na aina ya mchezo, jambo ambalo linaongeza thamani kwa mtaalamu wa maandalizi ya mwili.
YANGA YASIFIWA LAKINI...
Akitoa tathmini ya soka la Tanzania, Berdien anasema kuwa kwa kipindi kifupi alichokaa, ameona mabadiliko makubwa hasa katika uwezo wa kimwili na kimbinu wa wachezaji.
“Mpira wa Tanzania umebadilika sana. Unaweza kuona hilo hata kwa Taifa Stars kufuzu AFCON 2025. Kiwango cha Ligi kimeinuka,” anasema.
Kuhusu Yanga, wapinzani wakubwa wa Simba, Berdien anasema:
“Ni timu nzuri. Wamekuwa pamoja muda mrefu, hata wakibadilisha makocha hakuwaathiri sana mfumo wao. Nawapongeza. Lakini msimu ujao utakuwa tofauti. Tunajua sasa mahali pa kwenda kuchukua mataji, tunajua anwani yao.”
KOCHA, MWALIMU, MLEZI
Berdien anaendelea kumwaga sifa kwa kocha mkuu wa Simba, Fadlu akisema uhusiano wao ni wa heshima ya kitaaluma na pia wa kimalezi.
“Nimemfahamu kwa muda mrefu, sasa ni mlezi wangu kitaaluma. Anavyofikiri na kupanga mambo ni tofauti. Anatufanya kazi iwe rahisi. Yeye ni mwalimu wa kweli,” anahitimisha.