Wamehama wakiwa bado wanapendwa

KUNA usajili wa kigeni ulifanywa na timu za Simba, Yanga na Azam FC ambao uliwabamba mashabiki wao hadi walikuwa hawatamani mastaa hao kuondoka ndani ya vikosi hivyo.
Maproo hao walikuwa na ushawishi mkubwa, uliowapa raha mashabiki wao kujivunia uwepo wao, thamani yao ilikuwa kubwa iliyozivuta timu nyingine kuwanyakua. Mastaa hao walipoondoka kwenye timu hizo, waligeuza furaha za mashabiki wao na kuwa machungu, kwani bado walikuwa wanawahitaji waendelee kusalia ndani ya timu hizo.
Mwanaspoti linakuchambulia baadhi ya mastaa hao, walipohamia timu nyingine ilileta kichefuchefu kwa mashabiki wao.


OKWI-SIMBA
Baada ya Simba kumsajili, Emmauel Okwi akitokea SC Villa ya Uganda, alijizolea umaarufu mkubwa nchini, Wanasimba walimuita mfalme, alipewa thamani hiyo kutokana kazi ya miguu yake.
Okwi amecheza Simba kwa vipindi tofauti, vilivyowafanya mashabiki wa timu hiyo kuwa na furaha, wakati mwingine huzuni ziliwatawala alipokuwa anatimka kwani bado walikuwa wanahitaji huduma yake.


Misimu aliyocheza Okwi ndani ya Simba ni 2010-2013, 2014/15 na 2017-2019 huu wa mwisho alikuwa mfungaji bora wa Ligi Kuu (mabao 20).
Ufalme wake ndani ya Simba, ulifutwa na uwezo mkubwa wa Meddie Kagere ambaye alichukua kiatu cha dhahabu misimu miwili mfululizo, hilo lilifanya mashabiki kumsahau, pia hudumu nzuri ya Luis Miquissone na Clatous Chama ilikuwa faraja kwao.


CHAMA-SIMBA
Kiungo mchezeshaji Clatous Chama ameacha alama ya maumivu kwa mashabiki wa Simba baada ya kupata dili ya kuichezea RSB Barkane ya Morocco, ameondoka ndani ya kikosi hicho akiwa bado anahitajika.
Katika misimu mitatu aliyocheza Simba, Chama amechangia asisti 34 na mabao 17, msimu wa 2018/19 alifunga mabao saba na asisti tisa, 2019/20 mabao 2 na asisti 10 na 2020/21 mabao nane na asisti 15, Simba ilimsajili staa huyo akitokea Lusaka Dynamos.


KISINDA-YANGA
Amecheza mwaka mmoja tu, ukamtambulisha uwezo wake hasa mbio alizokuwa anawatesa nazo mabeki wazito na wakati mwingine kusababisha wapate kadi.
Yanga ilimsajili Tuisila Kisinda kutoka AS Vita ya Congo, anaondoka ndani ya klabu hiyo na kujiunga na Perkane ya Morocco, mashabiki wa Wanajangwani wakiwa bado wanamhitaji.


LUIS-SIMBA
Luis Miquissone ameondoka Simba akiwa anahitajika na mashabiki wake, kusajiliwa kwake na klabu ya Al Ahly kunadhihirisha huduma yake namna ilivyokuwa muhimu.


Luis alikuwa na uwezo wa kufunga na kutoa pasi, pia alikuwa anawapa presha mabeki, alikuwa na uwezo wa kupenyeza katikati yao na kwenda kufanya madhara langoni kwao.




NIYONZIMA- YANGA, SIMBA
Kitendo cha Haruna Niyonzima kuondoka Yanga msimu wa 2017-2019 kwenda Simba, kiliwaumiza sana mashabiki wa

Yanga waliofaidi huduma yake tangu alipojiunga nao 2011-2017, akitokea APR ya Rwanda.
Angalau alipooza mioyo ya mashabiki wa Yanga baada ya kutokuwa na msimu mzuri Simba,


kisha kurejea tena kwao 2020/21 na baadae kuuagwa kwa heshima.


KIPRE TCHETCHEAZAM FC
Tangu alipojiunga na Azam FC na kuitumikia kuanzia msimu wa 2011-14, akisajiliwa kutoka Jeunesse alitumika kwa kiwango cha juu na aliondoka wakati bado anahitajika kwani alijiunga na Al-Suwaiq.


KAVUMBAGU-YANGA
Yanga ilimsajili Didier Kavumbagu msimu wa 2012-14 akitokea Atietico Olympic, baada akaamua kuondoka kwenda kujiunga na Azam FC msimu wa 2014-2016 akiwa kwenye kiwango cha juu na mashabiki wa Jangwani bado walikuwa wanamhitaji.


MORRISON-YANGA
Yanga ilimsajili Benard Morrison mwaka 2020 akitokea Motema Pembe, alikuwa wa moto, ilikuwa silaha ya mashabiki wao kuwatambia Simba kwa namna alivyokuwa anatembea juu ya mpira na kufanya maajabu.
Alidumu miezi sita tu, akahamia Simba usajili uliozua balaa hadi sasa bado hukumu haijatoka Cas, kujua alikuwa na mkataba au la, aliondoka akiwa bado anahitajika na mashabiki wake.