Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Wabunge wanaelewa, tatizo lipo kwa klabu

WABUNGE Pict

Muktasari:

  • Ni kweli kwamba ili wabunge waweze kuchangia kwa ufanisi katika Bunge la Bajeti ni lazima wafanye utafiti wa kina ili wawe na hoja za kukosoa au kuishauri serikali kuhusu masuala mbalimbali, lakini ufuatiliaji wa masuala ambayo hayazungumzwi sana umeonyesha wabunge walikuwa makini safari hii katika mambo mengi kuhusu utamaduni, sanaa na michezo.

PENGINE ni kwa sababu ya ukubwa, historia na utamaduni wa klabu za Simba na Yanga ndio ulifanya mjadala wa hotuba ya makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo ya mwaka wa fedha wa 2025/26 kuchangamka sana, lakini kilichojionyesha dhahiri ni ufahamu na ufuatiliaji wa wabunge katika masuala yanayoendelea katika michezo, hasa soka.

Ni kweli kwamba ili wabunge waweze kuchangia kwa ufanisi katika Bunge la Bajeti ni lazima wafanye utafiti wa kina ili wawe na hoja za kukosoa au kuishauri serikali kuhusu masuala mbalimbali, lakini ufuatiliaji wa masuala ambayo hayazungumzwi sana umeonyesha wabunge walikuwa makini safari hii katika mambo mengi kuhusu utamaduni, sanaa na michezo.

Ingawa wakati wa kupitisha bajeti hiyo, wabunge waliotaka kushikilia shilingi kuzuia isipite hadi wapate maelezo ya kutosha, walikutana na 'cha mtema kuni', bado walionyesha kuwa si wakati tena wa viongozi wa michezo, hasa soka kupandisha kiburi na kudhani kuwa hawawezi kuwajibishwa.

WABU 01
WABU 01

Ni kanuni za Bunge na kuheshimu utamaduni wa Shirikisho la Kimataifa la Soka (Fifa) ndio uliwezesha serikali isishinikizwe kuchukua hatua, hasa baada ya sakata la kuahirishwa kiholela kwa mechi ya Yanga na Simba.

Hatimaye wabunge walipitisha bajeti hiyo ya Sh519.66 Bilioni, ambayo mbali na shughuli nyingine za wizara, imejikita kuhakikisha maandalizi kwa ajili ya fainali za Ubingwa wa Mataifa ya Afrika kwa wanaocheza ndani ya nchi zao (CHAN) zitafanyika kwa mafanikio Agosti na pia zile za Mataifa ya Afrika (AFCON) za mwaka 2027.

Sehemu kubwa ya mjadala iliegemea katika mchezo huo wa Machi 8 ulioahirishwa saa mbili kabla ya muda wa mechi, kwa madai kuwa kulikuwa na viashiria vya vurugu na rushwa, na mbunge mmoja akataka Waziri Palamagamba Kabudi aeleze hiyo taarifa ilipatikana kutoka chombo gani cha dola.

Hata hivyo, siku chache baadaye Mwenyekiti wa Bodi ya Ligi (TPLB), Steven Mnguto alisema walilazimika kuahirisha mechi hiyo kwa kuzingatia matokeo yake kikanuni kwa sababu klabu moja ingeshushwa daraja.

WABU 04

Kubadilikabadilika huko kwa Bodi ya Ligi kulitafsiriwa kama ni kukosa uhuru wa kufanya kazi.

"Tumeweza kuona Ligi Kuu ya England, inaongozwa na Bodi ya Ligi ambayo inaitwa EPL. Na Federation (Chama cha Soka) ya England ina ligi yao, hizi ni Ligi mbili. Na Bodi ya Ligi ya England inasimamia kila kitu kuhusu masuala mazima ya Ligi Kuu," alisema mbunge wa Manonga (CCM), Seif Khamis Gulamali wakati akianza kujenga hoja yake.

"Tumeona Ligi Kuu ya Hispania inaongozwa na Bodi ya Ligi. Mheshimiwa Naibu Spika, pale Spain kuna Bodi ya Ligi inaitwa La Liga, inasimamia masuala mazima ya michezo kuhusu ligi, lakini pia Federation ina ligi yake.

"Hapa Tanzania nimpongeze Mheshimiwa Leodegar Chila Tenga kwa kuanzisha Bodi ya Ligi kama idara ya TFF na imekuwa nzuri tangu ilipoanzishwa mwaka 2008. Ilianzishwa ikiwa idara ya TFF lakini malengo yalikuwa ije ijitegemee kama zilivyo bodi za ligi ya Uingereza, kama ilivyo bodi ya Ligi ya Spain.

WABU 05

"Sasa bodi yetu bado iko chini ya TFF. Tunaomba Mheshimiwa Waziri uiboreshe, iwe independent (huru), ijitegemee. Tunaona bodi ambayo haijisimamii. Asubuhi inatoa matamko haya, jioni inatoa matamko haya. Hii inaonekana nyuma ya pazia bodi hii inasukumwa."

Hata hivyo, Naibu Spika Mussa Azzan Zungu, alimzuia kuendelea kuzungumzia suala hilo kwa maelezo kuwa alikuwa anakituhumu chombo ambacho hakina nafasi ya kujitetea bungeni na kuzungumzia masuala ambayo hayajafanyiwa uamuzi.

Gulamali, ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Yanga, alikuwa akimaanisha uamuzi wa Bodi ya Ligi kuweka msimamo asubuhi siku ya mechi ya Machi 8 kuwa mchezo huo ungefanyika kama ulivyopangwa, lakini baadaye mchana ikatangaza kuuahirisha.

WABU 03

Mbunge mwingine aliyezungumzia sakata hilo, ni Joseph Musukuma, ambaye alianza kwa kutaka taarifa ya mazungumzo baina ya Serikali, Simba, Yanga, Bodi ya Ligi na Shirikisho la Soka (TFF).

Alitaka taarifa hiyo ili wabunge waende kuwashirikisha wananchi wao kuhusu kilichotokea Machi 8 hadi mechi kuahirishwa, lakini akaenda mbali zaidi kutaka kunyoosha mambo huko mbele.

"Mheshimiwa, naomba nishauri," alisema mbunge huyo. "Bodi ya Ligi isiongozwe na TFF. Iwe independent (huru) wazungu wanasema. Tunaona sasa inapokea maelekezo tu kutoka TFF. Kwa hiyo naomba sana Mheshimiwa Mwenyekiti, tuache na tuunde Bodi ya Ligi inayojitegemea."

Masuala hayo yalijitokeza wakati wa kupitisha mafungu ya fedha kwa ajili ya matumizi tofauti, lakini Naibu Spika akawa mkali na hivyo bajeti hiyo kupita bila ya shilingi yoyote kuzuiwa.

Pamoja na Bunge kutofikia hatua ya kutoa maagizo kuhusu sakata hilo, cha kushangaza imekuwa ni rahisi kwa wabunge kuelewa kuwa tatizo kubwa la uendeshaji na usimamizi wa ligi zetu ni kutokuwa na chombo huru, ama bodi ya ligi iliyo huru kama malengo ya waasisi wake walivyotaka.

WABU 02

Hili lilitakiwa liwe limeeleweka mapema sana kwa viongozi wa klabu za Ligi Kuu na Championship, ambao wanasimamiwa na TPLB. Cha ajabu ni kwamba hakuna anayezungumzia uhuru huo wala kasoro zinazotokana na chombo hicho kutokuwa huru.

Katika hali ya kawaida, kama mechi zaidi ya tatu zimeahirishwa kisanii sanii namna hiyo, tayari waliohusika wangekuwa wameshawajibishwa na mianya kuchunguzwa na kutafutiwa suluhisho.

Kwa kutochukua hatua hadi sasa baada ya mechi ya Yanga na Simba kubadilishwa muda kiholela mwaka 2021, mechi ya Kagera na Simba kuahirishwa kiholela msimu uliopita na mechi ya Yanga na Simba kuahirishwa kiholela, ni rahisi kutafsiri kuwa Bodi iliamriwa iahirishe mechi hizo na si uamuzi wa bodi.

Kama Gulamali alivyodai, kuna msukumo uliokuwa nyuma wa kubadili msimamo wa TPLB uliotolewa asubuhi kuwa mechi iendelee kama ilivyopangwa.

Hilo ni moja kati ya makosa mengi yanayotokana na chombo hicho kutomilikiwa na klabu zenyewe na kuwa na muundo wa uwazi na uwajibikaji.

Haiwezekani Mwenyekiti wa TPLB awe ndiye Mwenyekiti wa Kamati ya Usimamizi na Uendeshaji wa Ligi. Hapa kosa likitokea katika kamati, haitawezekana Mwenyekiti kujiwajibisha kwa kuwa mikono yake tayari ina madoa.

Na haitawezekana kwa chombo kingine kumuadhibu Mwenyekiti wa Bodi kwa makosa ambayo kamati yake ilifanya akiwa anaiongoza. Hii ni kwa sababu Kamati ya Uongozi wa TPLB pia iko chini ya uenyekiti wa Steven Mnguto huyohuyo.

Sasa katika utawala bora, nani anaongoza menejimenti, ambayo kimsingi hujihusisha na shughuli za kila siku; nani anaiongoza bodi, kwa maana inayoundwa na wakurugenzi, na nani anawajibika kwa wanachama, yaani mkutano mkuu wa klabu?

Hivi ni vitu ambavyo klabu zinatakiwa zivione na kuvipigia kelele ili virekebishwe na kuundwa kwa muundo ambao utaonyesha uwajibikaji na utawala bora.

Uhuru wa Bodi ya Ligi unagombewa na wenye ligi wenyewe kama ilivyo ligi nyingine za Hispania, England, Ujerumani na Ufaransa. Mtu anaweza kusema hao tusijilinganishe nao, sasa tujilinganishe na Burundi? Hao ndio wanatuwekea viwango vya ubora kwa hivyo hata tukifikia robo ya wanachokifanya, tunakuwa tumefanya makubwa.

Klabu hazina budi kuamka. Zisitegemee vita yao ipiganwe na wabunge au waandishi wa habari, bali klabu zenyewe kwa kuwa na watu makini, wanaoelewa mambo na wenye ujasiri wa kuziambia mamlaka kwamba wakati umefika wa TFF kujihusisha na mambo yanayoihusu tu na kuziachia klabu ligi yao.

Wabunge wameamka na viongozi wa klabu nao waamke.