Waamuzi waliowahi kushangaza dimbani

Muktasari:
- Kwa mfano katika robo fainali ya Kombe la Dunia 1980 iliyofanyika Italia, mwamuzi Edgardo Codessa wa Mexico na wasaidizi wake walilaumiwa kwa kuikaba koo Cameroon ili kuhakikisha England inashinda.
MARA nyingi katika soka mwenendo wa mwamuzi huzua mjadala na kudaiwa hakutenda haki na kudaiwa aliamua kuikandamiza timu moja. Hali kama hiyo inatokea katika michezo ya ligi au mtoano na hata katika michezo ya kimataifa ya mabara au Kombe la Dunia.
Kwa mfano katika robo fainali ya Kombe la Dunia 1980 iliyofanyika Italia, mwamuzi Edgardo Codessa wa Mexico na wasaidizi wake walilaumiwa kwa kuikaba koo Cameroon ili kuhakikisha England inashinda.
Ubaya alioufanya mwamuzi huyo mpaka leo hutolewa mfano kwa mwamuzi anapokuwa mchezaji wa 12 wa moja ya timu zinazocheza.
Hali kama hiyo iliikuta tena Cameroon ilipocheza na England 2019 katika fainali za Kombe la Dunia la Wanawake, ambapo mwamuzi alionekana kuipendelea England mpaka ikaibuka na ushindi wa 3-0.
Hapa kwetu hivi karibuni zilishuhudiwa lawama alizotupiwa mwamuzi mmoja akidaiwa kuibeba timu moja hadi ikajipatia ushindi wa mabao 2-1 ilipokutana na timu ya kawaida tu katika mchezo wa Ligi Kuu.

Ukiachia mazungumzo ya namna mwamuzi alivyosimamia mchezo yapo mambo ambayo wapo waamuzi waliyafanya na kuacha historia katika kandanda. Kwa mfano mwamuzi kutoka Zanzibar, hayati Musa Bakari alifanya jambo ambalo halisahaulika alipokabidhiwa filimbi ya mchezo wa fainali wa Klabu Bingwa ya Afrika kati ya Hafia ya Guinea na Etoile Flante du Togo (Togo Shooting Stars) uliofanyika Lomme, Togo 1975.
Mchezo huo ulikuwa na vurugu ya wachezaji kukanyagana, kukwaruzana na kuumizana, lakini Musa alionekana kuvumilia na watazamaji kumshangaa. Kipindi cha pili kilipoanza aliwapanga wachezaji kama inavyokuwa kabla ya kuanza mchezo na watu kuona hicho ni kiroja. Hapo tena akawapa kadi za njano wachezaji na viongozi wa timu zote mbili.
Musa ambaye alikuwa mwalimu wa shule na aliwahi kuchezea timu ya Vikokotoni ya Zanzibar, ameia-cha kumbukumbu hii iliyolifanya Shirikisho la Kandanda la Kimataifa (Fifa) kumpa pongezi na zawadi.

Miongoni wamuzi aliyefanya mambo kama ya hayati Musa ni Damian Rubino wa Argentina ambaye Machi 4, 2011 alikasirishwa na wachezaji waliotaka kupigana licha ya kutoa onyo na alipoona wameanza kusukumiana makonde alichukua kadi nyekundu iliyokuwa mfukoni na kuwaonyesha wachezaji wote waliokuwepo uwanjani na waliokuwa katika benchi la wachezaji wa akiba na viongozi wao.

Jumla ya kadi alizotoa zilikuwa 36 na mchezo ukavunjika. Baada ya mchezo kuvunjika alisema alikuwa anasikitika kwa nini hakuwapa kadi wasaidizi wake wawili (washika vibendera), kamisaa wa mchezo na yeye mwenyewe. Alisema alihisi angefanya hivyo ingependeza kwa sababu kadi ambazo zingekuwa zimetolewa ni 40 na kufanya watu iwe rahisi kumkumbuka.
Mchezo huo mchafu wa kutafuta klabu bingwa ulikuwa wa klabu hasimu za Argentina yaani Claypole na Victoriano Aarenas.
Wakati mwamuzi alipotoa hizo kadi na mchezo kumalizika mara tu kilipoanza kipindi cha pili, Claypole ilikuwa inaongoza 2-0. Baada ya mchezo kuvunjika wachezaji, viongozi na mashabiki wa timu hizo mbili waliendelea kupigana kwa muda kidogo na yeye aliwasogelea baadhi yao kusimamia kwa kutumia fil-imbi yake.

Katika mchezo ule hata watoaji huduma ya kwanza nao walichapana makonde. Hii haikuwa burudani ya kawaida. Mwamuzi Robino baadaye alikwenda chumba cha mawasilianio na kutumia kipaza sauti na kuwaambia polisi alishatoa kadi nyekundu uwanjani na kilichobaki ni kwa polisi kuwakamata waliokuwa wanapigana na kwenda kuwapa kadi nyekundu kituoni.
Mwamuzi huyo alilaumiwa na viongozi wa klabu na viongozi wa Shirikisho la Kandanda la Argentina kwa hatua yake hiyo isiyo ya kawaida. Katika ripoti yake, Rubino alisema alidhani alipewa jukumu la kusimamia mchezo wa kandanda, lakini alichokiona ni wachezaji kuugeuza uwanja kuwa ulingo wa ma-sumbwi.
Kwa kuwa hakuwa na ujuzi wa kuchezesha masumbwi aliamini ni bora avunje mchezo na alilishauri shi-rikisho la kandanda nchini humo litayarishe onyesho la masumbwi katika uwanja huohuo kwa wachezaji na viongozi wa klabu hizo mbili. Katika kandanda mashabiki wamezowea kuona mwamuzi anatoa kadi moja au mbili na zikizidi huwa tatu, lakini wapo waamuzi walioweka rekodi za kugawa kadi nyekundu kama njugu.
Kwa mfano, katika mchezo uliofanyika Paraguay kati ya Sportivo Ameliano na General Caballero 1993 mwamuzi alitoa kadi nyekundu kwa zaidi ya nusu ya wachezaji wa pande zote mbili na mchezo ikabidi uvunjike.
Michezo mingine maarufu ambayo waamuzi walitoa kadi nyingi nyekundu na njano ni Ureno dhidi ya Uholanzi zilipokutana 2006 katika mzunguko wa timu 16 wa fainali za Kombe Dunia ambapo mwamuzi Valentin Ivanov wa Urusi alitoa kadi 16 za njano na nne nyekundu.

Hii ni rekodi katika fainali za Kombe la Dunia zilizoanza 1930 nchini Uruguay. Fenerbahce na Galatasaray ambao ni watani wa jadi wa Uturuki walipokutana katika ligi 2002 wachezaji wanne wa Galatasaray walipata kadi nyekundu na kufungwa 1-0. Mwamuzi alidaiwa kula rushwa ili kuhakikisha Galatasary wanafungwa na kukosa ubingwa.
Atletico Madrid na Osasuna zilipokutana katika ligi 2007 wachezaji wanne wa Osasuna walipewa kadi nyekundu katika kipindi cha pili na wapinzani wao kupata ushindi wa 2-0. Chesterfield na Plymouth Ar-gyle zilipocheza 1997 wachezaji wanne wa Plymouth walipewa kadi nyekunda kwa mpigo. Bristol Rov-ers na Wigan Athletic zilipopambana 1997 wachezaji watano wa Wigan walitwangwa kadi nyekundu, nne katika kipindi cha kwanza.
Katika Ligi Kuu Hispania 2003 Espanyol ilipokutana na Barcelona mwamuzi alitoa kadi tatu nyekundu kwa kila timu na zikiwa zimebaki dakika 10 za mwisho za mchezo kila upande ulikuwa na wachezaji wanane. Katika mchezo kati ya Recreativo Linense na Saladillo De Algeciras 2009 mwamuzi alitoa kadi 19, nyingi zikiwa za njano.
Kilichoshangaza ni wakati wa mapumziko mwamuzi alikwenda vyumbani na kutoa kadi tisa kwa wachezaji kwa maelezo kwamba alisahau kufanya hivyo uwanjani.
Hata kwetu vipo visa vizuri vya waamuzi. Wakati nilipokuwa naandika habari za michezo, lakini kutoka-na na kutokuwepo kumbukumbu habari zake hazisikiki. Hata hivyo, nawajua waamuzi wawili wa za-mani ambao baada ya mchezo waliwatafuta wachezaji waliowatukana na kupigana nao masumbwi. Mmoja wao alikwenda klabu usiku uleule akamtafuta mchezaji aliyemtukana na kumsukumia ma-konde. Ni vizuri Shirikisho la Kandanda Tanzania (TFF) na vyombo vya habari kuwa na mpango mzuri wa kuwa na kumbukumbu zote za michezo ambazo baada ya miaka kupita zikifanyiwa simulizi huwa ni bu-rudani ya ziada.