Nini kimemkuta Neymar?

Muktasari:
- Miaka mingi imepita, Lionel Messi na mshkaji wake sasa wapo kule fukwe za Miami wanapunga upepo, Iniesta amestaafu, Xavi amekuwa kocha, Gerard Pique anafanya biashara zake. Kwa kifupi Barca ile ndio imeshabaki historia.
NIMEKAA nimewaza tu, miaka ya 2013 kuja juu, nimekumbuka zile herufi tatu zilizoiteka dunia MSN. Barcelona ya ajabu ile, katikati Xavi Hernandez, Andreas Iniesta na Sergio Busquets, pale juu Neymar, Lionel Messi na Luis Suarez, ungejiteteaje ulipokutana nao.
Miaka mingi imepita, Lionel Messi na mshkaji wake sasa wapo kule fukwe za Miami wanapunga upepo, Iniesta amestaafu, Xavi amekuwa kocha, Gerard Pique anafanya biashara zake. Kwa kifupi Barca ile ndio imeshabaki historia.
Hata hivyo, mwanadamu ana kawaida ya kusahau, hasa wakati kama huu ambao Lamine Yamal, Pedri, Raphinha, Gavi na wengine wanaendelea kutoa burudani, hufikia mahali tunaisahau Barcelona ile, ingawa hatuwezi kusahau baadhi ya mastaa wake. Ndio huwezi kumsahau Messi, Suarez, Neymar na mastaa wengine waliocheza wakati ule.
Wote hao waliendelea na maisha ya soka na wakapata mafanikio sehemu nyingine, lakini hadi leo hatujui nini kimemkuta Neymar.
Unyumbulifu, akili kubwa ya mpira wa miguu na kila aina ya sifa bora unayohitaji kumpa mchezaji bila shaka ungempa Neymar yule wa Barcelona.

Wakati nyayo yake inaacha kukanyaga punje za mchanga pale Governor Andre Franco Montoro International Airport, Wabrazil walimuaga kama shujaa, hawakuhitaji aende Ulaya kwa ajili ya pesa walihitaji aende kuiendeleza heshima ya bendera ya Brazil. Wakampa na baraka zote.
Neymar tayari alishakuwa anajiweza kifedha kabla hata hajaondoka Brazil, miaka miwili nyuma alinunua boti inayofikia dola 10 milioni (zaidi ya Sh20 bilioni). Aliondoka Brazil akiwa amebebeshwa bendera na sio pochi ya pesa.
Hicho ndicho alichoenda kukifanya kule Catalunya, akisababisha dunia ijaribu kuona tena miguu ya ajabu katika ardhi ya Hispania.
Usingeweza kutaja wachezaji watano bora wanaowania tuzo ya Ballon d’Or ukaacha kutaja jina lake, dunia isingekuelewa.
Waarabu wa Qatar wakaja mezani wakaweka ada ya uhamisho ambayo haijawahi kuvunjwa hadi leo Euro 222 milioni.

Neymar akatimkia zake PSG, Wabrazil walifurahishwa sana na usajili huu, pengine zaidi ya rais wa PSG, Nasser Al-Khelafi, waliamini ni muda sasa wa mchezaji wao kusimama kama Mfalme peke yake, waliamini Barcelona alikuwa akikaa nyuma ya kivuli cha Messi, nini kimekumta mshkaji wetu?
Hata hivyo, mambo hayakuwa yalivyotarajiwa, maisha yake PSG hayakubadilisha chochote, dunia haikutaka kukubali kulitaja jina lake katikati ya Messi na Cristiano Ronaldo, wachache sana waliazima muda wao kuwasha TV ili kumtazama akicheza akiwa na PSG, ghafla stori yake ikabadilika, haikuishia hapo, mashabiki wa PSG waliompokea kwa nderemo na vifijo nao wakamkataa, majeraha yakawa sehemu ya maisha yake.

Baadhi ya mashabiki wakajaribu hadi kwenda kuandamana nyumbani kwake jijini Paris wakimtaka aondoke, waarabu wa Saudi wakapiga hodi, pengine waliamini angeweza kuwasadia sana katika ligi yao kwa sababu haikuwa na presha sana. Wao walihitaji mambo mawili kwanza jina lake, pili uwezo wake, bahati mbaya wakapata kimoja kile cha jina lakini uwezo akawanyima.
Pesa nyingi sana ikawekwa mezani, mshahara wa karibia Pauni 2.5 milioni kwa wiki, wapishi kutoka Brazil, magari ya kifahari pamoja na madereva wa kumwendesha, ndege binafsi ya kumsafirisha muda wowote, bonasi za kufunga na kucheza katika mechi. Waarabu walichafukwa tu, waliamua kuweka pesa ya ajabu ili kumpata kwa gharama yoyote.
Hadi kufikia muda huo Wabrazil walishakata tamaa naye tena, waliwekeza nguvu zao kwa Vinicius, jina lake halikuimbwa tena, hivyo hata wakati anasajiliwa na Al-Hilal ya Saudia, hawakushangazwa sana.
Waarabu nao wakapigwa na butwaa pale staa huyu alipokanyaga ardhi ya jangwa lao. Walichokuwa wakikiwaza juu yake wala hakikuwa, Neymar alizidi kuwa mgonjwa siku hadi siku, katika mkataba wake wa miaka miwili aliosaini hakuwahi kucheza hata mechi 20, ajabu hii. Huyo ni Neymar, nini kimekuta?

Baada ya kuona hasara inazidi, Wasaudia nao wakanyoosha mikono, wakamwachia buree. Neymar sasa amerudi nyumbani kwenye timu yake ya utotoni ‘Santos, Hajarudi na kile Wabrazil walichomtuma, amerudi na kile ambacho ulimwengu unakihitaji - pesa.
Licha ya kwamba alikuwa tajiri kabla, kucheza katika nchi zote kumemfanya awe tajiri zaidi. Akiwa na Santos dunia iliamini kwamba angerudisha zile enzi zake hata kwa asilimia 30, lakini mambo yamezidi kuwa magumu. Tangu atue hapo majeraha yanamwandama. Juzi juzi pia amekutwa na virusi vya Corona. Yaani ni kinyume nyume tu kwake.
Inawezekana na wewe ukawa unajiuliza na usipate jibu, sote hatuna majibu, nini kimemkuta mwanetu Neymar.