Kwa hili la dabi, tukubali soka lishinde kwa masilahi ya wote

Muktasari:
- Kwa muda mrefu tumekuwa tukitazama soka letu likipiga hatua na kuvutia wawekezaji na kuwa kivutio pia kwa wachezaji na makocha wa mataifa mbalimbali, huku tukifurahia namna klabu zetu na timu za taifa zikishindana kwenye michuano mbalimbali.
KWENYE ukuaji wa jambo lolote, changamoto zinazojitokeza ndizo sehemu ya ukuaji wenyewe. Hata ikitokea umevuka salama, changamoto hizo unaweza kuzitumia kama funzo na huo ndiyo ukuaji wenyewe.
Kwa muda mrefu tumekuwa tukitazama soka letu likipiga hatua na kuvutia wawekezaji na kuwa kivutio pia kwa wachezaji na makocha wa mataifa mbalimbali, huku tukifurahia namna klabu zetu na timu za taifa zikishindana kwenye michuano mbalimbali.
Katika kipindi hicho, bado tukaendelea kuzilea klabu zetu pendwa kama watoto wa uzeeni tukasahau zinakua, tunapaswa kuzifundisha zipi haki zao na upi wajibu wao na hakuna haki isiyokuwa na wajibu.
Tumekuwa tukizisaidia kufanya mambo kadhaa na kuvunja utaratibu na kanuni tulizojiwekea, ndiyo maana leo tunajadili Dabi ya Kariakoo inachezwa au haichezwi?

Mechi hiyo ambayo awali ilipangwa kufanyika Machi 8, lakini ikaahirishwa saa chache kabla ya kuchezwa kisha bodi ikatangaza kuipangia tarehe mpya ambayo ni Juni 15.
Tarehe hiyo mpya imekuwa ikipingwa na Yanga, iliyosisitiza haitacheza kwa sababu bado haijajua kilichosababisha dabi ya Machi 8 kuahirishwa.
Kama tunakumbuka vizuri, hii si mara ya kwanza kwa Dabi ya Kariakoo kuahirishwa na kuzua utata kwa timu moja kusimamia kwenye kivuli cha kanuni na kwenda uwanjani na kutotambua mabadiliko yanayohusu mchezo husika.

Ilitokea katika lililokuwa limepangwa kupiMei 8, 2021 liliahirishwa saa chache kabla ya kupigwa na kuibua mzozo mkubwa.
Hata hivyo, baadae mechi hiyo ilipangwa kuchezwa Julai 03, 2021 na Yanga kushinda kwa bao 1-0 lililofungwa na Zawadi Mauya dakika ya 12.

Kwa hali ya sasa, mzozo huu ndiyo ulipaswa kuwa kama sehemu ya kujitathimini na kujua hili dudu tunalolifuga kuna siku litatumeza litakapojihisi limekua kubwa kuliko mfugaji. Sasa ndipo zilipofikia timu za Kariakoo.
Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) na Bodi ya Ligi (TPLB) kama wasimamizi wa soka la nchi hii ni muda sasa wa kuziondolea upendeleo na zile kinga dhidi ya taratibu na sheria zinazosimamia mchezo, kila mmoja awe chini ya sheria na kanuni na hawa watoto pendwa wa Kariakoo wawe mfano wa kuigwa na klabu zingine.
Mimi naamini hili tutavuka na litatuimarisha sana kwenye kusimamia kanuni na taratibu tulizojiwekea ila tulipofikia tumepelekwa na kutumia busara zinapohitajika kanuni tulizojiwekea, hata kumaliza kwake tunaweza kumaliza kwa kutumia busara kuliko kurudi katika kanuni ambazo kama zingetumika mapema leo tungekuwa tunajadili mafanikio.

Hatuhitaji kutafuta mshindi bali mpira ushinde kwa kucheza michezo iliyobaki japo kuna upande utabidi kuwajibika kwa kuvumilia maumivu.
Ili mpira ushinde, maumivu hayo yanaweza kubebwa na TFF na TPLB kama wazazi wanavyobeba maumivu ya familia ili mambo yaende au kuangalia namna ya kuzipunguzia nguvu zile timu pendwa na kuzifanya zifuate na kutii sheria kwa kuweka uwanja huru wa kupambana na mwenye uwezo apate anachostahili.
Kuziondolea msaada ndani na nje ya uwanja bila kuzionea itazifanya zitambue nafasi zao ni ukweli usiopingika ni klabu zenye wafuasi wengi. Ndiyo kioo cha mpira wetu, ikifikia mahali wakajihisi wanaweza kufanya chochote na hakuna wa kuwawajibisha ni ngumu sana kusimamia soka.

Ni kweli kuna haja ya kuwa na chombo huru cha kusimamia na kuendesha ligi zetu ili kuipunguzia kazi TFF na wao kubaki kusimamia maendeleo ya soka nchini, ila wakati mwingine kinachotuangusha siyo kukosekana chombo huru pekee bali ni wale waliopo kukosa uadilifu na kuipambania timu wanayoipenda hata ikibidi kusigina kanuni.
Tukifanikiwa kuvua jezi za timu zetu za Kariakoo na kuvaa uzi wa taifa tunapokuwa katika majukumu ya kuusimamia mpira, tutafanikiwa kufika tunapopahitaji. Hapo ndipo tutaona soka letu limekuwa.