Viwango vya mastaa Bongo wanaotesa nje

Muktasari:
- Wachezaji kama Lionel Messi, Cristiano Ronaldo na Kylian Mbappe ni mifano ya wanasoka waliotumia viwango vyao kupata mapato na utajiri mkubwa. Miaka mitano nyuma ilikuwa nyota walewale Mbwana Samatta, Simon Msuva na Himid Mao kusikia kuwa wanatoka sehemu moja kwenda nyingine katika timu tofauti nje ya Tanzania.
KWA sasa kuona Mtanzania anasajiliwa na timu kubwa kutoka mataifa mbalimbali ikiwemo Ulaya ni jambo la kawaida kutokana na maendeleo ya soka.
Wachezaji kama Lionel Messi, Cristiano Ronaldo na Kylian Mbappe ni mifano ya wanasoka waliotumia viwango vyao kupata mapato na utajiri mkubwa. Miaka mitano nyuma ilikuwa nyota walewale Mbwana Samatta, Simon Msuva na Himid Mao kusikia kuwa wanatoka sehemu moja kwenda nyingine katika timu tofauti nje ya Tanzania.
Lakini, hivi sasa soka kila kukicha unasikia Watanzania wanatambulishwa kwenye klabu mbalimbali za nje. Kwa kuangalia hilo na kuthamini mchango wa Watanzania wanaokipiga timu mbalimbali, Mwanaspoti inakuchambulia baadhi ya nyota ambao viwango vyao vinawapa ulaji nje ya nchi kwa sas.

SELEMAN MWALIMU (Wydad AC)
Ndiye mchezaji anayecheza Ligi ya Botola Pro akiwa na miamba ya Morocco, Wydad AC ikimsajili akitokea Fountain Gate FC.
Anakuwa mchezaji wa tano kusajiliwa na Morocco baada ya Simon Msuva aliyewahi kucheza Wydad,
Nickson Kibabage,Maka Edward na Shabani Chilunda.
Mwalimu kiwango alichoonyesha msimu huu akifunga mabao sita kwenye Ligi Kuu Bara mzunguko wa kwanza kimembeba hadi akalamba dili hilo.
Kabla ya hapo akiwa na KVZ ya Zanzibar msimu uliopita aliifungia timu hiyo mabao 20 kwenye michezo 27 na kumfanya aondoke na kiatu cha ufungaji.

ISMAIL MGUNDA (AS VITA)
Mshambuliaji huyo wa zamani wa Mashujaa FC hivi karibuni alitambulishwa AS Vita ya DR Congo inayofundishwa na Youssuf Dabo aliyewahi kuifundisha Azam FC. Msimu ambao alifunga mabao mengi ulikuwa 2023/24 akiwa na Singida Black Stars akitupia sita.
Ndio msimu aliofunga mabao mengi kwani Mashujaa na Tanzania Prisons aliingia kambani mara mbili, Kyetume ya Uganda akifunga moja na Jomo Cosmos (Afrika Kusini) bao moja mechi mbili.

NOVATUS MIROSHI (GOZTEPE)
Ndiye mchezaji pekee anayekipiga Ligi Kuu Uturuki akiwa na Goztepe baada ya Mbwana Samatta aliyewahi kukipiga Fenerbance kutimkia PAOK ya Ugiriki. Sio tu sehemu ya kikosi hicho lakini ni mchezaji tegemeo kwenye timu hiyo iliyopo nafasi ya tano kwenye msimamo ikiwa na pointi 35.
Nyota huyo ambaye pia ana uwezo wa kucheza kiungo wa chini amekuwa na mwendelezo mzuri sio tu wa kuzuia lakini hata kufunga. Novatus alianzia Azam baadaye Biashara United, kisha Maccabi, akapelekwa kwan mkopo Beitar Tel Aviv.
Msimu mmoja aliocheza Israel ulimpa shavu la kwenda Ubelgiji alikojiunga na Zulte Waregem 2022/23 ndipo akaibukia Shakhtar Donetsk kabla ya kutua Uturuki aliko hadi sasa.

WAZIR JUNIOR (AL MINA’A)
Nyota huyo hivi karibuni alitambulishwa na Al Mina’a inayoshiriki Ligi Irak akiungana na Simon Msuva wa Al Talaba. Wazir Jr alijiunga na timu hiyo iliyopo nafasi ya 16 kwenye msimamo wa timu 20 akitokea Dodoma Jiji.
Kabla ya hapo alisumbua makipa wa Ligi Kuu kwa mabao yake akiwa na KMC.
Msimu wa 2015/16 na 2016/17 akiwa na Toto Africans alifunga mabao 14, msimu uliofuata akatua Azam FC na kufunga moja, msimu 2018/19 (Biashara United) mabao matatu. Akiwa Mbao FC, Waziri Jr alifunga mabao 14 kwenye mechi 12 msimu 2019/20 ndipo Yanga ikamsajili uliofuatia akafunga mabao mawili, 2021/22 mabao manne Dodoma Jiji akacheza misimu miwili KMC na kufunga mabao 13.

SIMON MSUVA (AL TALABA)
Kwa kipindi cha miaka 10 sasa Tanzania haijapata mshambuliaji mwenye mwendelezo mzuri wa kufunga ukimtoa nahodha Mbwana Samatta kwenye ngazi ya klabu lakini hata kikosi cha Stars.
Mabao mawili aliyofunga kwenye mechi mbili za mwisho kufuzu Acon dhidi ya Ethiopia ambapo Tanzania ilishinda 2-0 na dhidi ya Guinea 1-0 iliyoipa nafasi Stars kufuzu fainali hizo zitakazofanyika nchini Morocco.
Kwa sasa yuko Irak akikipiga na Al Talaba aliojiunga msimu huu akifunga tayari mabao manne. Ukiachana na kucheza Ligi Kuu Bara akiwa Azam na Yanga nyota huyo amekuwa akiwaniwa na timu kutoka mataifa mbalimbali kutokana na anachokifanya uwanjani kila mara. Baada ya kucheza Yanga 2012/17 msimu uliofuata alitua Difaa El Jadida ya Morocco alikocheza misimu mitatu mechi 80 na kufunga mabao 28 mashindano yote.
Kiwango bora alichoonyesha akiwa na Difaa kikaivutia Wydad AC, Msuva akasaini mkataba wa miaka minne akicheza mechi 37 na kufunga mabao 10.
Mambo hayakwenda sawa akaondoka zake na kutua Al Qadisiah ya Saudia akaweka kambani mabao nane kwenye mechi 28, kabla ya kuibukia JS Kabylie ya Algeria. Msimu 2024/25 alirejea Saudia na kukiwasha Al Najma akafunga mabao manne kwenye mechi 15, akatimkia Talaba.

CYPRIAN KACHWELE (Vancouver Whitecaps)
Ni mchezaji wa zamani wa Azam kwa sasa anakipiga Vancouver Whitecaps inayoshiriki Ligi Kuu Marekani (MSL).

JARUPH JUMA (AIN DIAB)
Mshambuliaji huyo ndiye nyota wa kwanza kucheza soka la kulipwa nchini Morocco kwa upande wa soka la ufukweni.
Kwa sasa anawania tuzo ya mchezaji bora wa dunia akishindana na wachezaji kutoka mataifa mbalimbali lakini kwa Afrika Mashariki na Kati akiwa pekee. Jaruph pia aliwahi kukipiga Simba na Yanga za vijana na alijiunga msimu uliopita na timu hiyo inayoshiriki Ligi ya Ufukweni Morocco. Msimu wake wa kwanza akiingia katikati kwenye mechi 10 amefunga mabao nane.
Mbwana Samatta (PAOK)
Nahodha huyu wa Stars ana rekodi nyingi za ndani na kimataifa na ndiye mchezaji anayetajwa sana linapokuja suala la wachezaji wa Tanzania waliopo nje. Kiwango cha nyota huyo kimemfanya aheshimike na kutajwa kama mchezaji mwenye mafanikio makubwa Tanzania. Samatta alianza maisha yake ya soka la kulipwa akiwa na Simba 2010/11, lakini kapita katika timu mbalimbali ikiwamo TP Mazembe (DRC Congo), KRC Genk (Ubelgiji), Aston Villa (England), Fenerbance (Uturuki), Royal Antwerp, kisha PAOK ya Ugiriki ambapo yupo hadi sasa. Pia huwezi kuzungumzia mastaa waliopo nje ya nchi waking’ara bila kumtaja Baraka Majogoro wa Chippa United ya Afrika Kusini,