Unajua faida za mazoezi kabla hujakimbia?

ZOEZI la kukimbia mbio nyepesi kwa mwendo wa wastani kitaalam hujulikana kama Jogging, ni moja ya zoezi linaloainishwa kama zoezi jepesi kitabibu Aerobics exercise.
Ni aina ya zoezi ambalo linaweza kufanywa na watu wa rika lote lakini watu wazima ambao hata umri wa uzee uliowadia yaani 45+ nao wanalimudu vyema.
Ni zoezi ambalo linalokupa matokeo makubwa kiafya katika kukabiliana na unene ambao ni kihatarishi cha magonjwa yasiyoambukiza ikiwamo ya moyo, sukari na kiharusi.
Zoezi linaweza kuwa na matokeo makubwa endapo utalifanya muda wa dakika 150 kwa wiki ambazo ni sawa na dakika 30 kwa siku katika siku 5 za wiki.
Ili kujihami na majeraha yasiyo na lazima ni vyema zoezi la ukimbiaji mbio nyepesi likaambatana na mazoezi lainishi ya viungo vya mwili.
Si sahihi kiafya kuingia katika ukimbiaji ama mchezoni wowote pasipo kufanya mazoezi ya viungo ambayo huwa ni kunyoosha viungo bila kukimbia au kutembea.
Mazoezi haya ni ya msingi kwani yanauandaa mwili kuweza kukabiliana na hali ngumu zinazojitokeza michezo kama vile kujipinda uelekeo hasi, kuvutika kwa nyuzi mvutiko za misuli, nyuzi ligamenti na tendoni.
Zoezi hili kiujumla linasaidia mwili kukabiliana na mijongeo hasi inayoweza kujeruhi tishu laini za mwili hivyo kumuepusha mwanamichezo na majeraha yasiyo na lazima.
Ikumbukwe kuwa wakimbiaji wengi wanakimbilia katika maeneo kama vile pembezoni mwa barabara za huduma, viwanja tambarare, vimipando au vilima na vifaa vya Gym vya kukimbilia.
Katika maeneo kama haya wakati wa ukimbiaji inaweza kutokea kupata ajali au kujikwaa au kukanyaga kitu ambacho kikapinda kiungo na kwendo uelekeo hasi kwa mwili na hatimaye kujijeruhi.
Kama mazoezi ya viungo yamefanyika kwa ufanisi basi matukio kama haya yanapotokea wakati wa ukimbiaji yanaweza kutokea lakini mkimbiaji asipate majeraha kwakuwa tayari viungo viliandaliwa.
Zoezi la kunyoosha viungo huwezesha misuli ya mwili kupata utulivu na kuwezesha damu na virutubisho muhimu kutiririka kwa wingi katika mifupa plastiki na misuli.
Mazoezi ya viungo kwa mkimbiaji yanahitajika kufanyika kwa muda wa dakika 5-10 kabla na baada ya ukimbiaji mwepesi.
Basi baada ya kuona hayo, hebu tuone faida 7 za kiafya mazoezi
ya viungo ikiwamo kulainisha na kunyooosha misuli ya mwili kwa mkimbiaji wa mbio nyepesi yaani Jogging.
Moja ni kuondokana na uchovu hivyo kukufanya kupata utulivu wa kimwili na kiakili wakati wa kufanya zoezi la ukimbiaji.
Kurundikana kwa shinikizo katika misuli huifanya misuli ya mwili kujikunyata hivyo kuleta hali ya hisia za kukakamaa na kutohisi wepesi hivyo kuleta madharaya kiakili na kimwili.
Kuondoa au kupunguza shinikizo lililopo katika misuli kwani hivyo siku inayofuata unapoomka huwezesha mwili kuwa mpya kiutendaji hatimaye kupata hamu ya ukimbiaji hapo baadaye.
Kumbuka kuwa pale unapoamka na uchovu au kuumwa viungo huweza kukupa hofu pengine unaumwa na magonjwa ikiwamo malaria.
Mazoezi haya yanaifanya misuli ya mwili isibane na kuipa utulivu hivyo kutoa nafasi kwa damu kutiririka kirahisi.
Pia mazoezi haya husababisha mwili kutiririsha kemikali mwili ijulikanayo kama Endorphins inayoufanya mwili kupata hisia za furaha hivyo baadaye utaona ukimbiaji ni burudani.
Vile vile kufanya mazoezi haya pamoja na ukimbiaji husaidia kukupa usingizi mzuri kwani hautakuwa na hali ya maumivu au uchovu wa misuli hapo baadaye.
Mbili, kusaidia kuweka ulalo sahihi wa mwili, kunyoosha misuli ya mwili iliyokakamaa husaidia kuivuta na kuirudisha katika sehemu yake asilia inayotakiwa kuwepo.
Kunyoosha misuli eneo la chini mgongoni, kifuani na mabega husaidia kuuweka uti wa mgongo katika mpangilio sahihi hivyo kuboresha mkao wake ambao hauleti uchovu wa misuli hii.
Hii itakusaidia kulianza zoezi la ukimbiaji ukiwa na hamasa na mweye kujiamini hivyo kufanya ukimbiaji wako kwa ufanisi.
Tatu kuimarisha wepesi wa mwili, wepesi huufanya mwili kuwa na utayari wa mabadiliko wakati wowote ikiwamo unaporuka, kukimbia au kujipinda.
Wepesi wa mwili kwa mijongeo hii huupunguzia mwili mzigo kiutendaji kwani mwili utatumia nguvu kidogo kufanya matendo hayo.
Pia epesi husaidia kuboresha utendaji wa kimwili na kupunguza hatari ya kupata majeraha ya mara kwa mara wakati wa ukimbiaji.
Nne ni kuongeza stamina kwani huifanya misuli na nyuzi za tendoni na ligamenti kuwa laini na nyepesi hivyo kuondokana na kukamaa na uchovu . Hii ni kwasababu damu hutiririka kwa wingi maeneo hayo.
Kadiri unavyofanya mazoezi ya viungo na ukimbiaji ndivyo pia mwili huchoma kiasi kikubwa cha sukari hivyo kuchangia kuondoa mrundikano wa mabaki baada ya sukari mwili kuvunja vunjwa.
Mazoezi ya viungo husaidia kuchelewesha kujijenga kwa uchovu unaoletwa na mabaki hayo kwani damu safi kufika kwa wingi katika misuli na kuyaondoa hivyo kuongeza utimamu wa mwili.
Tano, kupunguza hatari ya kupata majeraha kwani misuli kupokea damu na virutubisho kwa wingi huwa na faida kubwa kiafya hivyo hupunguza vijidonda vya misuli. Vile vile husaidia majeraha ya misuli na maungio kupona kwa wakati.
Sita, mazoezi ya viungo yanaufanya mifumo nyeti ya mwili ikiwamo mfumo wa upumuaji na mfumo wa Moyo na mzunguko wa damu kuwa katika utayari wa awali kuweza kufanya zoezi la ukimbiaji kwa ufanisi.
Saba, mazoezi ya viungo yanapofanyika yanakupa nafasi ya kukagua utayari wako wa viungo vya mwili dhidi ya ukimbiaji mwepesi wa siku hiyo na baada ya ukimbiaji kujua kama kuna shida yoyote katika mwili.
Kutokana na faida hizi ni vizuri kwa Mkimbiaji kuyafanya mazoezi haya kama sehemu ya maisha ya kila siku kabla na baada ya kukimbia.
Hakikisha unaitumia vyema simu Janja yako kwa kupakua taarifa zaidi za mazoezi ya viungo pamoja na apps zenye kuelekeza namna ya kufanya mazoezi ya viungo kwa mkimbiaji.