Uimara, udhaifu Simba na Yanga

Saturday September 25 2021
haya pic
By Charles Abel

TIMU za Simba na Yanga zitaumana leo kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa katika mechi ya Ngao ya Jamii ambayo itafungua msimu wa ligi 2021/2022.

Hii ni mechi ya nne kwa timu hizo kukutana mwaka huu kwani kabla ya hapo zimeshakutana mara tatu ambapo kati ya hizo, Yanga imeibuka na ushindi mara mbili, Simba imepata ushindi mara moja.

Watani hao wa jadi wanakutana huku wakiwa wametoka kufanya usajili katika dirisha la majira ya kiangazi lililofungwa Agosti 31 na baada ya hapo zikafanya maandalizi ya msimu kwa kuweka kambi huko Morocco katika miji tofauti na baadaye kurejea hapa nchini.

Mechi inayozikutanisha timu hizo mbili mara nyingi imekuwa haitabiriki na mara nyingi huwa na matokeo ya kushangaza ama yale yasiyotegemewa.

Lakini kwa kiasi kikubwa matokeo hayo huamuliwa kutokana na namna timu zilivyofanyia kazi ubora na udhaifu wao pamoja na ule wa timu pinzani.

Mwanaspoti inakuletea tathmini ya uimara na udhaifu wa timu zote mbili kuelekea mchezo huo ambao kama kuna upande utafanyia kazi unaweza kujiweka katika uwezekano mkubwa wa kupata ushindi katika mechi hiyo.

Advertisement


UIMARA

Uwepo wa wachezaji wenye uchu wa kufumania nyavu katika timu zote mbili, unafanya safu za ushambuliaji kwa kila upande kuwa idara tishio zaidi ambazo zinapaswa kutazamwa zaidi kwenye mechi ya kleo.

Safu ya ushambuliaji ya Yanga inaundwa na Mayele Fiston, Heritier Makambo, Ducapel Moloko na Yacouba Songne ambao wanapewa sapoti na kiungo mshambuliaji Feisal Salum.

Kwa upande wa Simba, safu yao ya ushambuliaji inaundwa na Chris Mugalu, Kibu Denis na Pape Sakho huku nyuma yao akiwepo Rally Bwalya.

Kocha Msaidizi wa Twiga Stars, Edna Lema alisema kuwa uwepo wa nyota wenye uwezo mkubwa wa kushambulia katika timu hizo, ni moja ya mambo yatakayoifanya mechi hiyo kuwa na ushindani.

“Ukiangalia timu zote zina washambuliaji wazuri na wanaojua kutumia nafasi hivyo kwa maoni yangu, walinzi kwa timu zote mbili wanapaswa kuwa makini kwa muda wote wa mchezo kwani wakijisahau tu wanaweza kujikuta wanawapa mwanya wapinzani kufunga bao au mabao,” alisema Lema.

Simba wamekuwa imara zaidi kwa mashambulizi ya kupitia katikati wakati uimara wa Yanga ni katika mashambulizi ya kupitia pembeni.

Uwezo wa viungo wa ulinzi wa Yanga kuichezesha timu kuanzia nyuma imewafanya Yanga kuwa na ufanisi pia katika mbinu ya kushambulia kwa kushtukiza hasa pale wanapokutana na timu ambayo inashambulia.

Simba wao wanabebwa zaidi na uwezo mkubwa wa kumiliki mpira wa mchezaji mmojammoja jambo ambalo limewafanya wawe na uwezo wa kuvunja ukuta wa timu pinzani.


UDHAIFU

Timu zote mbili zinaonekana kuwa na tatizo moja sugu la udhaifu wa kushindwa kuokoa mipira ya krosi na uthibitisho ni aina ya mabao ambayo zimefungwa katika mechi za hivi karibuni.

Mawasiliano baina ya makipa na walinzi wao yamekuwa duni lakini pia mabeki wamekuwa wakipoteza umakini katika kuokoa mipira ya juu jambo linalowapa faida wapinzani kuwafunga mabao.

Upande wa kushoto kwa kila timu umekuwa ukiruhusu mara kwa mara wapinzani kupiga mipira ya krosi

Winga wa zamani wa Simba, Mrage Kabange alisema iko haja kwa makocha wa timu hizo mbili kufanyia kazi changamoto hiyo.

“Ni kweli zimekuwa zikifungwa mabao ya aina hyo hivyo naamini makocha wameshafanya tathmini ya kugundua tatizo ni nini na bila shaka watafanyia kazi vinginevyo ni jambo linaloweza kuwagharimu,” alisema Kabange.

Rafu za mara kwa mara za viungo Lwanga Taddeo na Sadio Kanoute ni udhaifu mwingine wa Simba ambao wanapaswa waufanyie kazi kama ambavyo Yanga wanapaswa wajirekebishe kwa kiungo wao Zawadi Mauya.

Mkurugenzi wa ufundi wa timu ya DTB, Muhibu Kanu amesema Yanga ina wachezaji wengi wapya.

Advertisement