UCHAMBUZI: Sura mbili tofauti za Meneja wa Tshabalala

Muktasari:

MENEJA wa nahodha msaidizi wa Simba, Mohamed Hussein ‘Tshabalala’ aitwaye Heri Mzozo amekuwa gumzo kwenye vyombo vya habari katika siku za hivi karibuni.

MENEJA wa nahodha msaidizi wa Simba, Mohamed Hussein ‘Tshabalala’ aitwaye Heri Mzozo amekuwa gumzo kwenye vyombo vya habari katika siku za hivi karibuni.

Msimamo wake juu ya hatima ya beki huyo wa kushoto kama atabaki Simba au ataondoka umemfanya awe lulu kwa waandishi wa habari ambao mara kwa mara wamekuwa wakimpigia simu ama kumfanyia mahojiano ya ana kwa ana.

Tofauti na mameneja wengi wanaosimamia wachezaji ambao kipindi mikataba yaa wachezaji wao inapoelekea ukingoni hutoa kauli za kuonyesha kuipa nafasi ya kwanza klabu ya mchezaji husika katika mazungumzo ya mkataba mpya, hali imekuwa tofauti kwa Mzozo ambaye yeye amekuja kivingine.

Mzozo amesema kuwa yeye na mteja wake walishakubaliana kuwa hawatoongeza mkataba mpya wa kuendelea kuitumikia Simba kwa vile mchezaji huyo hakuonyeshwa heshima na thamani kubwa ndani ya timu hiyo kwa muda wa takribani miaka saba aliyoitumikia.

Meneja huyo anasema kuwa mteja wake licha ya mchango mkubwa anaoutoa kwa timu, amekuwa akilipwa fedha kiduchu za mshahara na dau la kusaini mikataba mipya tofauti na wachezaji wengine katika timu hiyo.

Alienda mbali zaidi kwa kusema kuwa Simba imekuwa ikithamini zaidi wachezaji wa kigeni kuliko wazawa ambao hawapewi heshima na thamani stahiki klabuni hapo.

Bahati nzuri mchezaji huyo amefikia makubaliano na Simba na ameongeza mkataba wa miaka mitatu kuitumikia timu hiyo

Najaribu kuzitafakari kauli za Heri Mzozo katika pande mbili za shilingi ambazo moja ni ukweli na uhalali wa kile anachokisema na kukisimamia lakini upande mwingine ni ule wa makosa ya meneja huyo katika kauli zake.

Kwa mtazamo wa kupigania maslahi ya mchezaji, Mzozo amefanya kitu sahihi kwa sababu yeye ndio mwenye jukumu kubwa na la mwisho kusimamia haki na stahiki za mchezaji huyo.

Kama meneja ni lazima atengeneze mazingira bora na wezeshi ya kumfanya mchezaji anayemsimamia apate maslahi bora zaidi kupitia mkataba mpya iwe kwa timu anayoitumikia au nyingine.

Inawezekana Mzozo amekuwa akitoa matamshi hayo kwa nia ya kuipa presha Simba itoe kiasi kikubwa cha fedha pengine kuliko hata kile ambacho ilikuwa inafikiria kumpa beki huyo waliyemnasa kutokea Kagera Sugar.

Labda pia Mzozo amezungumza hivyo akiwa tayari ameshafikia makubaliano na klabu nyingine hivyo anayoyaongea pengine yanatokana na uhakika kwamba upo uwezekano wa yeye na mteja wake kupata kiasi kikubwa cha fedha nje ya Simba.

Kinyume na hapo kuna namna fulani ambayo Mzozo hajaitendea haki klabu ya Simba na kiungwana angeshauriwa aiombe radhi kutokana na kauli zake ambazo zinaweza kuiathiri nembo na hadhi ya klabu hiyo.

Kauli ya kusema Simba haiwapi thamani wachezaji wazawa kwa kuhusianisha na kuchelewa kwa mchezaji wake kusaini mkataba mpya sio sahihi na haikupaswa kutolewa na mtu kama yeye.

Tshabalala ni miongoni mwa wachezaji ambao wamedumu Simba kwa muda mrefu hadi kupelekea kuchaguliwa kuwa nahodha msaidizi wa timu je kama ingekuwa wazawa hawathaminiki, angeweza kupewa jukumu hilo huku wale wa kigeni wakiachwa?

Huyohuyo Tshabalala alijiunga na Simba akiwa na umri mdogo wa chini ya miaka 20 tena akiwa sio mchezaji aliyekuwa na jina kubwa ama kuwa na uhakika wa namba katika kikosi cha Kagera Sugar, lakini Simba ilimuamini na kumpa nafasi hadi kumfanya awe hivyo alivyo leo je kama ingekuwa wazawa hawathaminiwi angeweza kupewa?

Lakini kabla ya huyo Tshabalala, wachezaji kadhaa wanaosimamiwa na Mzozo wameshawahi kuichezea Simba kwa mafanikio katika nyakati tofauti na wengine wamekuwa vipenzi ndani ya timu hiyo.

Mfano wa wachezaji hao ni mshambuliaji Athuman Machupa na viungo Haruna Moshi ‘Boban’ na Ramadhan Chombo ‘Redondo’

Kama Simba ingekuwa haiwajali wachezaji wazawa sidhani kama Mzozo angeendelea kukubali kufanya nao kazi hadi leo hii akiwa anamsimamia Tshabalala.

Tunahitaji kuwa na mameneja na wasimamizi ambao watapigania maslahi ya wachezaji wao kwa njia sahihi ambazo hazivurugi mahusiano baina yao na wachezaji wao na klabu ambazo zinafanya nao kazi. Lipo la kujifunza kupitia kwa sakata la Heri Mzozo na Simba katika kushughulikia suala la mkataba mpya wa Tshabalala. Wengine watumie kama darasa.