UCHAMBUZI: Mechi Simba, Yanga na thamani ya soka

Siku zote katika maisha ya kila siku tasnia ya michezo itaendelea kutawala katika mijadala mbalimbali, sio tu katika vyombo vya habari, bali hata mitaani.

Hi ni kwa kuwa michezo mbali na kuwa ni ajira kwa waliopo ndani ya sekta hiyo, lakini kitendo cha kutoa burudani kwa watu ni miongoni mwa vitu muhimu vinavyosaidia michezo kuwa na thamani katika jamii na kutengeneza uhitaji mkubwa kama mahitaji mengine muhimu kwa mwanadamu.

Kwa mfano, tukichukulia tukio la Mei 8, mwaka huu lililotokea katika Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam, ambapo mechi kati ya watani wa jadi, Simba na Yanga haikuchezwa.

Hilo ni moja kati ya matukio yanayoweza kutumika katika kuonyesha umuhimu na thamani ya michezo katika jamii, kwani kila mtu anajua kuwa mahitaji ya muhimu ya kimwili kwa mwanadamu ni chakula, mavazi na malazi.

Lakini, matukio kama hayo yanapotokea ndio hutumika kama mifano kuainisha mahitaji mengine muhimu ya mwanadamu ambayo ni ya moyo ukiachilia mbali yale ya kiakili.

Mahitaji ya mioyo ya wanadamu huongozwa na utashi wa mtu kutokana na mapenzi yaliyopo moyoni mwake kwa timu au mchezo husika, hivyo kuwa ni hitaji muhimu kama vile mahitaji ya mwili.

Ndio maana katika mechi hiyo ambayo haikuchezwa tumeona kuna baadhi ya watu ambao si matajiri au watu wenye uwezo mkubwa wa kiuchumi, lakini kwa mahitaji ya mioyo yao walisafiri kutoka walipotoka ikiwemo mikoa mbalimbali kwa shida na kufika Dar es salaam kwa ajili tu ya kukidhi mahitaji ya mioyo yao.

Hawa ni wale ambao kwao ni huduma ya muhimu kuliko hata pengine chakula cha mchana au chai ya asubuhi. Hivyo mahitaji ya moyo ni muhimu kwa mwanadamu kama yalivyo mahitaji mengine ya kimwili na kiakili.

Kwa mataifa kama yetu matukio kama hayo yanapotokea ndio taswira halisi ya kile kilichokuwa pengine kinatafsiriwa tofauti inavyotakiwa hujulikana na uhalisia wake na tafsiri halisi ya jambo hilo hufahamika.

Katika hali ya kawaida inawezekana kabisa kwa mtu wa kawaida kubadilishwa kidogo tu kwa muda wa tukio kunaweza kuonekana kuwa ni jambo jepesi kama vile muda wa matukio mengine kubadilika - kama vile muda wa harusi na hata matukio mengine makubwa ambayo siku zote huwa yanatambuliwa kama ya kitaifa, ambayo huonekana kugusa maslahi ya Taifa.

Lakini, mabadiliko hayohayo kumbe ni vigumu kufanyika katika soka - mchezo unaogusa mioyo ya watu wengi kama ilivyo mechi ya Simba na Yanga.

Baada ya tukio hilo hilo la kihistoria kutokea tumethibitisha utofauti wake na matukio mengine yaliyowahi kutokea, na madhara yake kwa jamii sio tu jamii ya wanamichezo au mashabiki wa klabu hizi mbili za Simba na Yanga, bali hata wadau wengine ambao ni watoa huduma ikiwemo za usafiri, malazi, chakula hadi afya ambao nao wameathirika.

Pia wadau wengine walioathirika ni vyombo vya habari ambavyo katika hali ya kawaida inaeleweka kuwa kwa zaidi ya mwezi mmoja vilikuwa vinajipanga kutangaza na kurusha tukio hilo kwa watazamaji, wasilikilizaji na wasomaji, na viliingia makubaliano na kampuni mbalimbali za matangazo kwa ajili ya kutangaza bidhaa katika siku ya tukio hilo.

Ukiangalia kwa taswira hiyo unaweza moja kwa moja kulitafsiri kama tukio la kitaifa, ndio maana baada ya tukio hilo kutokea Serikali ilikuwa ndio ya kwanza kutoa taarifa na kuvielekeza vyombo vinavyosimamia michezo ikiwemo wizara vikutane kuangalia namna bora ya kurejesha matumaini kwa wadau walioathiriwa wakiwemo mashabiki waliolipa fedha za kuingilia uwanjani kutazama pambano hilo.

Hivyo kwa kuwa tukio hilo ndio mara ya kwanza kutokea katika mchezo wa soka nchini ambalo limetoa fundisho kubwa sio tu kwa jamii ya wanamichezo, bali wadau kutokana na ukubwa wake, mijadala ilichukua zaidi ya siku tatu kupitia vyombo vya habri ikiwemo mitandao ya kijamii.

Fundisho limethibitisha thamani halisi sio tu kwa mechi aina ya Simba na Yanga, ila thamani ya mchezo wa soka hasa kwa jamii ambapo wadau waliomo ndani huweka kipaumbele kama wadau wengine wanavyoweka vipaumbele katika sekta nyingine za kilimo, uvuvi, mifugo na kadhalika.

Inawezekana katika hali halisi mtu mwingine akaona kwamba ni jambo la kawaida kwa michezo kushabikiwa namna ile, lakini ukweli ni kwamba ukirejea katika msingi ya saikolojia unaona kwamba binadamu daima anapenda kufurahi na furaha ni jambo kubwa zaidi linalohitajika kwa mwili wake.

Kwa vyovyote vile, linapokuja suala la michezo - iwe soka au michezo mingine kulingana na mapenzi ya mtu, hiyo ni sehemu ya furaha yake.


IMEANDIKWA NA ALI MAYAY