UBISHI WA MZEE WA KALIUA: Tunahitaji kweli wachezaji 12 wa kigeni nchini?

FUNDI wa mashairi na mwanamuzi wa Bongo Fleva, Mrisho Mpoto aliwahi kusema kuanza upya sio ujinga kwenye moja ya mashairi yake.
Msingi wa kuwa na kanuni inayoruhusu wachezaji 12 wa kigeni kwa kila klabu ni kuzisaidia timu zetu ziweze kuwa na nguvu ya kushindana kimataifa na kuliletea heshima Taifa letu.
Nia ni njema kabisa na mimi naunga mkono lakini baada ya kuziona timu zetu zikicheza kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika na Kombe la Shirikisho, nimegundua wachezaji 12 wa kigeni ni wengi sana.
Timu zetu bado hazina ubavu wa kupata wachezaji 12 wote wakiwa na ubora wa kwenda kushindana Afrika na kuleta mafanikio. Unadhani sababu ni nini? Wacha nikupe majibu. Kwanza wachezaji wengi wanaosajiliwa hasa pale Simba na Yanga, wengi wanakuwa na umri mkubwa na pili, wengi wanakuja bure.
Ni mara chache sana timu hizi zimemnunua mchezaji wa kigeni kwa kuvunja mkataba na timu yake ya nje. Ni mara chache sana timu hizi zimepata mchezaji kijana. Wachezaji wengi wa kigeni wanakuja nchini wakiwa tayari na miaka 30 au karibu na hapo.
Sioni sababu za kuendelea kuwa na kanuni inayoruhusu wachezaji 12 wa kigeni wakati hakuna kikubwa wanachosaidia huko Kimataifa. Hatuwezi kuwa na wachezaji 12 wa kigeni ambao kazi yao ni kuwafunga Ihefu FC na Kagera Sugar.
Hatuwezi kuwa na wachezaji wengi wa kigeni ambao umaarufu wao unakuja kwa kuwasumbua Tanzania Prisons na Namungo FC. Hii sio dhamira ya msingi ya kuruhusu wachezaji 12 wa kigeni kusajiliwa nchini.
Pamoja na kuruhusu wachezaji 12 wa kigeni, Geita Gold FC wameondolewa hatua za awali kabisa Kimataifa.
Pamoja na kuwa na wachezaji 12 wa kigeni, Yanga na Azma FC nao wote wameondolewa kabla ya hatua ya makundi!
Hakuna maana yoyote ya kuwa na wachezaji wengi wa kigeni wakati hawaleti mabadiliko yoyote Kimataifa. Hata pale Simba, pamoja na kufuzu kwenda hatua ya makundi bado kuna wachezaji wengi wa kigeni ambao ni kama wanakula mshahara wa bure tu.
Kuna wachezaji wengi pale ambao wanaishia kukaa benchi tu. Kuna wachezaji wengi wa kigeni ambao ni mzigo tu! Kwa kutazama timu zetu zinavyocheza Kimataifa, kwa kutazama aina ya matokeo tunayopata kwenye michuano ya Afrika, sioni sababu ya kuwa na wachezaji 12 wa kigeni.
Wachezaji wengi wanaokuja kwenye timu zetu, wako maji ya jioni, wachezaji wengi wa kigeni wanaokuja kwenye klabu zetu, wengi wanaelekea kutundika daluga.
Wana nguvu ya kushindana na Mtibwa Sugar na Police Tanzania. ukiwapa mechi na Raja Casablanca hawawezi kukuvusha. Ukiwapa mechi na Orlando Pirates, hakuna mahali wanatoboa.
Ni bora tupunguze idadi ili Klabu zetu zipunguze kuokota okota wachezaji. Tukipunguza idadi, klabu zitaongeza umakini kwenye kuketa wachezaji.
Walau klabu inaweza kusajili wachezaji wenye uwezo kwa sababu watakuwa na bajeti walau ya kununua kuliko hawa wa bure wa kila siku.
Tunahitaji wachezaji wenye uwezo kama kina Clatous Chota Chama, Fiston Mayele na kina Yannick Bangala. Hatuhitaji wachezaji wavunja kuni. Hatuhitaji wachezaji wastaafu. Baada ya kuona Geita Gold FC wanahangaika Kimataifa, Yanga hoi na Azam FC chali sioni sababu ya kuwa na wachezaji wengi wa kigeni wakati hakuna jipya wanaloleta Kimataifa.
Klabu zikipewa nafasi ya kuketa wachezaji watano tu wa kigeni, watajitahidi kutuletea wachezaji wa kigeni wa ukweli kama walivyokuja kina Pascal Wawa, Haruna Niyonzima, Emanuel Okwi, Kipre Tchetche na wengine wengi.
Ukianza kutazama uwezo wa mchezaji mmoja mmoja wa kigeni, utagundua pale Simba kuna wachezaji sita tu. Wale wengine wote wanaobakia ni wavunja kuni tu. Ukitazama pale Yanga, huwezi kupata wachezaji kweli wa kigeni zaidi ya sita, wengi pale wanaongeza idadi tu. Hakuna haja ya kuwa na wachezaji 12 ambao kazi yao ni kuwafunga Zalan FC tu. Hatuwezi kuwa na wachezaji wa kigeni ambao wanazidiwa uwezo kwa mbali na wachezaji wazawa. Sasa walikuja kufanya nini? Hawatufai. Mpira wetu sio nyumba ya wastaafu. Ni bora tupunguze idadi ili tuongeze ubora. Wachezaji wengi wa kigeni 12, hawajasaidia chochote timu zetu kimataifa.
Simba imefuzu sio kwa sababu ya wachezaji 12 wa kigeni. Pale Simba kuna kama wachezaji sita tu wa kigeni wa ukweli, wengine wamekuja kustaafu tu na mwendo walishaumaliza siku nyingi tu.
Unahitaji kweli wachezaji 12 wa kigeni? Baada ya matokeo ya timu zetu kimataifa, jibu langu ni hapana. Hatuna uwezo wa kuleta wachezaji 12 wa ukweli wa kigeni. Tuna uwezo wa kuleta wachezaji wa bure. Tuna uwezo wa kuketa wachezaji wanaokaribia kustaafu. Hakuna haja ya kuwa na wachezaji wengi wakati hawazipeleki timu zetu popote.
Naiona haja ya kwenda kubadili kanuni hii. Kuanzia msimu ujao turudi tu kwenye wachezaji watano wa kigeni. Hakuna haja ya kuwa na wachezaji wengi wasio na uwezo. Hakuna.
Kama Yanga wanaleta wachezaji 12 wa kigeni na kwa miaka 25 hawajatinga michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika, hao wachezaji ni wa kazi gani? Usinipe jibu. Kama Azam FC kwa mismu 13 hawajawahi kufika hata hatua ya makundi kwenye michuano ya CAF, hao wachezaji 12 wa kigeni niwa kazi gani? Usinipe jibu. Kuna haja ya kurudi nyuma na kutazama Kanuni zetu upya. Sioni tija ya kuwa na wachezaji wengi wa kigeni wakati hawaleti jambo jipya.
Ni bora tubaki na wachezaji watano tu wa ukweli. Wachezaji wengi wa kigeni wanakuja nchini kama wako Royal Tour.
Walishamaliza kila kitu wanakuja kutalii tu kwenye mpira wetu. Tunahitaji wachezaji wachache sana wa kigeni wenye uwezo wa kutuvusha. Tunahitaji wachezaji wachache wa kigeni wenye kuleta utofauti kikosini.