UBISHI WA MZEE WA KALIUA: Simba na Yanga ni mechi kubwa lakini sio tofauti

JUMAMOSI jiji la mipango mingi Dar es Salaam litasimama tena kwa dakika 90. Inapigwa mechi kubwa zaidi nchini, Simba na Yanga wanakutana katika mechi ya ufunguzi wa ligi. Mechi ya ngao ya jamii. Kwani kuna mechi kubwa zaidi ya hii Tanzania? Baada ya nchi kusimama katika matamasha ya siku ya Simba na Yanga, sasa ni zamu ya wao kukutana.

Mechi kubwa hii! Watu wameomba ruhusa kazini ili wapate nafasi ya kuishuhudia. Wengine watafunga biashara na kujisogeza uwanja wa Benjamin Mkapa au mbele ya vioo vya televisheni zao ili kushuhudia wenyewe.

Nani anataka kusimuliwa? Matokeo ya leo yatawanyima wengine usingizi na wengine watashindwa kuamka na kwenda kazini Juma lijalo. Kama ilivo kwa mechi zingine pambano la watani wa jadi linaisha ndani ya dakika tisini lakini matokeo yake yanakumbukwa miaka. Mechi kubwa hii.

Kwasababu hii ni mechi kubwa, mashabiki tumekuwa tukijidanganya kuhusu hii mechi kwa ëhoja za kijingaí. Kwa mfano mtu anaweza kukuambia ëmechi kubwa kama hii refa anatoaje penalti mbili?í Mwingine atakuambia ëMwamuzi anatoaje penalti ya mapema kwenye mechi kubwa hivi?í

Ukizunguka zaidi utakutana na mwingine anasema ëmwamuzi anatoaje penalti ya dakika za mwisho kwenye mechi kubwa hivi?í

Sasa hapo unaweza kujiuliza, muda sahihi wa mwamuzi kutoa penalti ni upi? Kwa hoja zilizotolewa na hawa watu, tuta linapaswa kutolewa katikati ya mchezo. Si sawa kutoa tuta mapema au jioni kwasababu hii ni mechi kubwa. Sheria haitoi muongozo wa muda wa kutoa adhabu ya penalt. Sheria inamuelekeza mwamuzi kufunika penalt iwapo mchezaji anayelinda amezuia nafasi ya kufunga kimakosa. Sheria haibagui mechi kubwa na ndogo.

Mara nyingi tunawabebesha waamuzi mizigo ya lawama ambayo hawastahili. Tunajikuta tukilaumu kwasababu tu ya mapenzi na mahaba tuliyonayo kwa timu zetu. Tunakuwa wavivu wa kufikiri na kuzitazama sheria kwasababu ya mahaba. Tunasahau sheria kumi na saba za soka haziubagui mchezo wa Simba na Yanga.

Tuache kulaumu vitu ambavyo havipo kwa kigezo kwamba hii ni mechi ya Simba na Yanga. Tukumbuke kwamba hii ni mechi ya kawaida ya ligi, kuwa mechi kubwa hakuifanyi ihukumiwe tofauti na mechi zingine. Ingekuwa ni mechi tofauti isingechezwa dakika tisini, labda ingechezwa dakika mia na hamsini!

Kabla ya kulaumu kwa mahaba tujifunze kutazama ukweli na sheria. Tuache huu upuuzi wa kusema ëPambano kubwa kama hili mwamuzi anatoaje kadi nyekundu mapema?í Kadi nyekundu inatoka muda wowote kosa la kadi nyekundu linapotokea. Fainali ya klabu bingwa Ulaya mwaka 2006, mwamuzi wa Norway Terje Hauge alimuonesha kadi nyekundu golkipa wa Arsenal Jens Lehmann katika dakika ya 18 baada ya kumchezea rafu Samuel Etoío wa Barcelona. Fainali ya 2019 tena, mwamuzi Damir Skomina aliwapa Liverpool penalti ndani ya sekunde ishirini nne tu baada ya mchezo kuanza.

Hivo wakati tunalaumu kwa kujificha kwenye kichaka kinachoitwa mechi kubwa tukumbuke kuwa zipo mechi kubwa zaidi ya hii yetu yaliyofanyika maamuzi kama haya tunayoyalaumu. Ina maana wao wanakosea?

Tukazane kuwaamini waamuzi na kuwapunguzia shinikizo. Tuache kuwaandama kuwa wamehongwa kwa kila kosa wanalolifanya. Hata nao ni binadamu, wanaruhusiwa kukosea.

Siamini kama mwamuzi anaweza kukubali kuhongwa aje atudanganye watanzania elfu sitini tuliokaa uwanja wa taifa na wengine mamilioni tunaotazama kwenye televisheni. Tutambaini tu. Kikubwa waamuzi wawe makini na wasimamie sheria za soka. Wasikubali kuibwa na shinikizo la mchezo.

Mwisho kabisa nawasihi mashabiki kwenda kufurahia mpira. Wasiende na matokeo mfukoni kwamba lazima washinde. Haipendezi kuona watu wa msalaba mwekundu wakiwabeba mashabiki waliodondoka kwasababu ya timu yake kufungwa bao.

Tusisikie tena kuna shabiki amefariki kwasababu matokeo yoyote yalitokea Kwa Mkapa jumamosi. Twendeni tukafurahie mchezo tukiwa tayari kwa matokeo ya kushinda na kushindwa.