Prime
Kile kiburi cha FAT, kimerejea TFF

Muktasari:
Kujipenyeza kuingia katika uongozi, na hasa uenyekiti wa FAT ilikuwa ni kama kutaka kuuhamisha Mlima Kilimanjaro kutoka mkoani humo kwenda sehemu nyingine. Ilionekana kama haiwezekani.
WAKATI chombo kinachoendesha mpira wa miguu kikiitwa Chama cha Soka Tanzania (FAT), ilifikia wakati wajumbe wa mkutano mkuu na viongozi walidhani ndio wenye haki pekee ya kuongoza mpira.
Kujipenyeza kuingia katika uongozi, na hasa uenyekiti wa FAT ilikuwa ni kama kutaka kuuhamisha Mlima Kilimanjaro kutoka mkoani humo kwenda sehemu nyingine. Ilionekana kama haiwezekani.
Huku soka likiporomoka, wajumbe wa mkutano mkuu waliokuwa takriban 70 walikuwa juu. Hawakutaka mtu ambaye angewashawishi kwa hoja kuangalia mambo ya soka kwa mtazamo mpya.
Waliridhika na walichokiona na hawakutaka kipya. Mgombea ambaye alitaka kupambana na uenyekiti wa wakati huo alijikuta akikosa mpigakura kumshawishi ampigie kura. Kama uchaguzi unafanyika Tanga, basi angekutana na wajumbe kwenye chumba cha kupigia kura na huko angejieleza wala asiulizwe swali hata moja.
Ilonekana kama wajumbe walikuwa sehemu fulani ili wasikutane na wagombea kutoka nje hadi ukumbini siku ya kupiga kura ambayo ni shida kushawishi wajumbe hadi wakukubali.
Kila mara waziri aliyekuwa akihusika na michezo alipoona hali inazidi kuwa mbaya na kujaribu kuingilia alikutana na rungu la Shirikisho la Kimataifa la Soka (Fifa) na hivyo baadaye kusalimu amri.
Akijaribu kuunda kamati ya muda, Fifa walikataa na kupendekeza kamati itokane na wajumbe wa mkutano mkuu au iundwe ya pamoja ya uongozi inayojumuisha viongozi waliokuwa madarakani na wajumbe wapya.
Msimamo huo wa Fifa haukusaidia kufanya mageuzi ya uendeshaji mpira wa miguu nchini, zaidi ya kuimarisha kilichokuwa kwa viongozi wa juu wa FAT na wajumbe wa mkutano mkuu.
Lakini, nguvu ya wananchi ilifanikiwa. Baada ya shinikizo kutoka sehemu tofauti. Hatimaye wadau waliunganisha nguvu na kufanya kikao kwenye ukumbi wa Manispaa ya Temeke, ambako kulifikiwa maazimio ya jinsi ya kulishughulikia tatizo hilo.

Hali ilipozidi kuwa mbaya, ndipo Fifa nayo ilipoingia na kufikia makubaliano ambayo yalisaidia kuubadili mpira wetu kwa kuufanya uongozi uwe taasisi na kujenga vyombo mbalimbali vya maamuzi.
Mojawapo ya maazimio yaliyokubaliwa na Fifa ni pamoja na kukubali kuingiza wadau wengi zaidi kwenye mkutano mkuu, yaani wawakilishi wa wanawake na klabu katika ngazi ya mkoa, kuongeza klabu za Ligi Kuu kuwa wajumbe wa mkutano mkuu na pia kuzipa kamati hadhi ya kuwa vyama shiriki na hivyo kuwa wajumbe wa mkutano mkuu. Kamati hizo ni ile ya waamuzi, makocha, madaktari, wachezaji na soka la wanawake.
Hapo ndipo lilipozaliwa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), likishirikisha vyama na taasisi tofauti. Idadi ya wajumbe wa mkutano mkuu ikaongezeka maradufu na hivyo kuuweka uongozi na wagombea katika hali ngumu katika kampeni zao.
Ikawa ni vigumu tena kuficha wajumbe zaidi ya 130 hadi siku ya uchaguzi. Ikawa ni vigumu tena kuhonga au kuwakirimu wajumbe wote.
Wagombea wakalazimika kuwa na uwezo wa kujenga hoja ili kushawishi wajumbe wawapigie kura, huku kazi ya viongozi ikawa ni kuhakikisha wanafanya kazi ili maendeleo yapatikane na hivyo kuwa na hoja kwa wapigakura.
Lakini mabadiliko ya katiba ya mwaka 2019 yaliondoa ugumu huo na kulirejesha soka kulekule tulikotoka, yaani kupunguza idadi ya wapiga kura kutoka wanne katika vyama vya mikoa hadi wawili. Ndio maana wanachama 46, yaani wenyeviti wa mikoa na vyama shiriki wameweza kuamua kuweka azimio la kumuidhinisha mgombea mmoja asimame kwenye uchaguzi wa rais bila ya mpinzani.
Idadi hiyo ikajenga dosari ya kutojali katiba ya TFF. Yaani suala la uchaguzi linazungumzwa, tena kwa nia ya kumpigia debe mgombea mmoja kwenye mkutano mkuu kinyume na taratibu na katiba.
Kawaida ajenda kubwa kama ya kumuidhinisha mgombea mmoja kusimama katika uchaguzi wa rais inatakiwa iwasilishwe kwenye mkutano mkuu na Kamati ya Utendaji na si kwenye mengineyo.
Na hata hivyo, Kamati ya Utendaji haiwezi kuwasilisha hoja kama hiyo kwa kuwa si sehemu ya ajenda na wagombea si wajumbe wa mkutano mkuu pekee.
Lakini ni kama wamewafunga macho wasione dosari au walakini wa kikatiba. Suala la mgombea urais si la mkutano mkuu, bali la mkutano wa uchaguzi. Mkutano wa uchaguzi ndio una ajenda moja tu ya uchaguzi.

Hata kwenye mkutano huo wa uchaguzi, mwenyekiti ambaye anatakiwa kuwa mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi hawezi kumruhusu mjumbe atoe pendekezo la kumuidhinisha au kumpa kura zote mgombea mmoja kwa kuwa haitakuwa haki kwa wagombea wengine.
Hicho ndicho kinachowafanya wajumbe wadhani kwamba nje ya TFF au nje ya mkutano mkuu hakuna watu wenye sifa wanaoweza kutupeleka mbali zaidi ya hapa tulipo. Kwamba aliyepo anatosha na si kwamba apate ushindani ili ajitume zaidi, la hasha!
Wajumbe hawa wana nini kinachowalazimisha kufumba macho na kujisahaulisha kule tulikotoka, ambako mwenyekiti angeweza kusema mchezaji fulani hawezi kuitwa timu ya taifa labda yeye aondoke madarakani? Na kwa aina hiyo ya uongozi viongozi wakawasilisha kanuni inayozuia mwanachama mmoja kumuidhinisha zaidi ya mgombea mmoja huku ikimruhusu mgombea anayeidhinishwa kutafuta zaidi ya wanachama watano wa kumuidhinisha.
Kwa hichohicho, wanachama wakapitisha pendekezo hilo la kanuni kwa fikra kwamba watakuwa wameshamaliza uchaguzi kwa kupiga kura kabla ya siku ya uchaguzi.
Hilo pia limekomaa kutokana na jinsi uongozi ulivyowanasa baadhi ya waandishi na watangazaji ambao huchomeka kwenye vipindi, kurasa za mitandao na kwenye safu zao, maneno ya kusifu kile wanachoita mafanikio ya haraka na kumpachika mtu yeyote anayehoji sifa ya “ana chuki na fulani”.
Hiki kinachoendelea kinakuzwa na ukweli kwamba nchi yetu inaenda kuandaa fainali za Mataifa ya Afrika (CHAN) mwezi Agosti na fainali za Mataifa ya Afrika (Afcon) mwaka 2027.
Kwa hiyo kuna mazingira yanajengwa kwamba serikali haiwezi kufanya lolote hata shirikisho likifanya vipi kwa kuwa inahofia kunyang’anywa fainali hizo kubwa Afrika ambazo zinaandaliwa kwa pamoja na Kenya na Uganda.
Ndio maana leo kila mgombea asiyekuwa ndani ya mkutano mkuu anaambiwa eti uidhinishaji ulishaisha muda mrefu. Uliisha lini wakati tarehe ya kuchukua fomu za kugombea ndio kwanza ilikuwa inaanza na ni kwa siku tano tu? Kama huo uidhinishaji ulifanyika kabla ya kuchukua fomu, basi ni batili na hapo ndipo pa kuanzia.
Lakini changamoto ni kwa sekretarieti na Kamati ya Uchaguzi. Je zinaweza kutoa ushirikiano kujua muda ambao uidhinishwaji ulifanyika?
Pamoja na yote, ukweli unabakia kuwa kama aliyesimamia mkutano mkuu hakutakiwa kuruhusu hoja ambayo ni nje ya ajenda kujadiliwa na kufikiwa uamuzi, kwani alikiuka katiba yake mwenyewe. Hivyo, hata kama barua za uidhinishaji zitaonekana ziliandikwa baada ya tarehe ya kuchukua fomu, bado azimio la uidhinishaji lilikuwa batili na hivyo utekelezaji wake ni batili pia.
Mamlaka za nchi zina wajibu wa kuhakikisha vyama vya michezo vilivyosajiliwa vinakuwa na mfumo bora wa uchaguzi unaoweka mazingira ya ushindani wa haki na sawa bila kutumia sheria kudhibiti baadhi ya watu.
Kama Msajili wa Vyama vya Michezo aliruhusu katiba na kanuni zinazominya haki na usawa katika uchaguzi, hana budi kurekebisha mapema kwa kuwa ni suala la sheria za nchi. Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) si chama cha siasa ambacho kama mtu asipokubaliana na sera na katiba yake, anaweza kwenda chama kingine au kuanzisha chake.
TFF ni moja tu na haina mpinzani. Si chama cha watu wachache waliopewa dhamana ya kuingia mkutano mkuu, bali ni cha wapenda michezo wote ambao hawana chama kingine kinachoweza kuwaongozea mpira wao kwa jinsi wanavyoona ni sahihi isipokuwa TFF tu.
Hivyo ni jukumu la Msajili kuhakikisha anaondoa kasoro hiyo mapema, ikiwezekana kuamuru mamlaka za soka zisogeze mbele uchaguzi hadi hapo dosari hizo zitakaposhughulikiwa kwa mujibu wa utashi wa sera na sheria za nchi.
Na hiyo haitakuwa ni kuingilia soka kwa kuwa wahusika ndio watatangaza wenyewe kusogeza mbele uchaguzi na ndio watakaorudi ukumbini kupitisha katiba inayoendana na sera za nchi na kanuni zinazoweka usawa na haki kwa wagombea wote.
Ni muhimu sana serikali kuhimiza vyama vya michezo kuwajibika kwa wananchi na si kwa wajumbe wanaowapa kura viongozi. Wananchi ndio wadau wakubwa wa michezo na wasipoenda viwanjani, thamani ya michezo inapotea.