UBISHI WA MZEE WA KALIUA: Kwanini Simba mnamtega Juma Mgunda?

Kwa Mgunda tulieni muone

MOJAWAPO kati ya makosa wanayofanya viongozi wa Klabu ya Simba ni kutoamua hatima ya kocha Juma Mgunda kwa wakati. Makocha wana athari nyingi sana kwenye mchezo wa soka. Tumeshuhudia chini ya kocha Zoran Maki baadhi ya wachezaji hawakuwa kipaumbele chake.

Zoran hakumtaka Clatous Chota Chama, hakumtaka Moses Phiri. Chini ya Juma Mgunda hawa wawili ni kama wamezaliwa upya. Huku mabao ya Phiri kuna mipasi ya Mwamba wa Lusaka. Viongozi wa Simba ni lazima wafanye uamuzi mapema. Kwa Mara ya kwanza msimu huu timu inaonekana kucheza vizuri chini ya Mgunda na hasa mechi ya mwisho dhidi ya Nyasa Big Bullets ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Haya ni mabadiliko makubwa kiuchezaji. Kuna dalili njema kwa Kocha Mgunda. Kuendelea kufanya kazi wakati hana uhakika na kesho yake ni kutomtendea haki kocha na klabu kwa ujumla. Sidhani kama ni sawa kuendelea kuwa na kocha ambaye hujampa uhakika.

Sidhani kama ni sawa kwa timu moja kuwa na makocha zaidi ya wanne ndani ya msimu mmoja. Nadhani ni wakati sasa wa Simba kuamua. Nadhani ni wakati wa kumleta kocha mpya mapema au kumpa mkataba Mgunda mpaka mwishoni mwa msimu. Kwa namna ulivyomtazama Mgunda anatosha kupewa timu mpaka mwisho wa msimu? Naomba maoni yako kwa kuniandikia ujumbe mfupi wa maandishi kupitia namba yangu ya simu hapo juu.

Kuna uwezo wa mchezaji mmojammoja umeanza kuonekana. Kuna uwezo wa timu umeanza kuonekana. Kama kocha atakuwa na uhakika wa kibarua chake anaweza kutuonyesha kitu cha tofauti. Hata uwe kocha mzuri kiasi gani unahitaji pia kuwa na wachezaji wazuri.

Mgunda taratibu anaanza kupata kikosi chake cha kwanza. Kuendelea kumtumia kwenye mechi zaidi ya tatu bila kumhakikishia ajira ya kudumu ni kujidanganya we-nyewe. Simba ni lazima wakubali kujitoa mhanga kujaribu kwenda na Mgunda msimu huu.

Kama hawana mpango huo ni bora kocha mpya aje mapema sana. Mambo ya kukuta timu imeshatolewa Ligi ya Mabingwa hayatasaidia. Mambo ya kuleta kocha mpya wakati timu imeshazidiwa pointi 10 na Yanga kwenye ligi itakuwa pia haina maana.

Muda wa kufanya mabadiliko au kumthibitisha Mgunda ni sasa. Pamoja na mambo mengine kama Simba hawatafanya vizuri msimu huu mchawi mkubwa ni viongozi wa klabu wenyewe. Timu inayotaka ubingwa wa ligi na nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika haiwezi kuendelea na michuano hiyo bila kuwa na uhakika na kocha wao.

Mpaka sasa ni kama Simba wanabahatisha. Hawana imani bado na Mgunda, lakini hawana pia kocha mkubwa wa kigeni. Timu zote kubwa huwa zinatimua makocha, lakini hawawezi kukaa bila uhakika na kocha mkuu kwa muda wote huu. Kama hadi sasa Mgunda hajui hatima yake atatimiza kweli malengo ya klabu? Sina uhakika.

Kesho Simba inaweza kuleta kocha mgeni akataka Moses Phiri auzwe. Ndivyo makocha walivyo. Kila mtu na mbinu zake. Kila mtu na watu wake. Anaweza kuja kocha mgeni akasema Pape Ousmane hafai. Ligi muda sio mrefu itachanganya na michuano ya Ligi ya Mabingwa nayo inapamba moto.

Kama hakuna hela ya kumleta kocha mwingine mpeni kibarua cha kudumu hadi mwishoni mwa msimu kocha Mgunda. Kama hakuna kocha mkubwa mnayemtaka mpaka sasa mpeni rungu Mgunda.

Ni kweli makocha ndiyo msingi wa timu kupata mafanikio, lakini Kibongobongo makocha hawana asilimia kubwa ya kuleta matokeo chanya.

Mambo ya kila kocha kuja kuingiza mbinu zake kwa wachezaji ni kuwachanganya tu. Kwa namna ambavyo umemtazama Mgunda kwenye mechi mbili dhidi ya Nyasa Big Bullets na ile ya Tanzania Prisons unadhani anatosha kupewa mkataba wa hadi mwisho wa msimu? Naomba maoni yako Kwa kuniandikia ujumbe mfupi wa maandishi kupitia namba yangu ya simu hapo juu.

Kwanini Simba mnamtega Kocha Mgunda? Mpeni Uhakika wa kazi awatumikie. Ni kweli wapo makocha wazuri sana huko nje, lakini pia wapo wa kuchovya na wanatusumbua. Makocha wakati mwingine ni kujaribu tu. Natamani kuona Simba wakijaribu kwa Mgunda.

Kama hauna timu bora hata ukimlela Pep Guardiola kutoka Uingereza pale Simba huwezi kupata kitu. Timu bora ikiwepo uwanjani kazi ya kocha inakuwa ndogo sana. Kwa sababu makocha pia ni binadamu kuna muda na wao wanahitaji muda kuzoea ligi na wachezaji.

Simba wanatakiwa kufanya uamuzi sahihi katika hatua hizi za mwanzo kabisa. Ama Mgunda abaki mpaka mwisho wa msimu au kocha mpya aje sasa hivi kuchukua timu. Tofauti na hapo ushindani wa Yanga na Azam utawasumbua sana mechi za ndani. Azam hawakutaka mambo yawe mengi waliachana na kocha mapema kabisa kabla mambo hayajakorogeka. Wakati wa ama kusuka au kunyoa kwa Simba ni leo.