UBISHI WA MZEE WA KALIUA: Kuna dhambi yoyote Yanga ikikosa ubingwa?

Kosa kubwa la Klabu ya Yanga ni kutaka kuwa na uwezo kama wa Simba kwa msimu mmoja tu! Simba haipo hapo kwa Bahati mbaya, wamewekeza sana kwa wachezaji, benchi la Ufundi, huduma za uhakika na kwa muda mrefu.

Yanga inaweza kuwa Bingwa msimu huu na hakuna tatizo. Yanga inaweza isiwe Bingwa na hakuna tatizo pia.

Ufalme walionao Simba kwa sasa ndani ya Ligi Kuu Tanzania Bara, waliusubiri kwa misimu mitano. Walijipanga, walivumilia, waliumia lakini mwisho wamejenga timu imara.

Tangu msimu wa 2012/2013 hadi 2017/208, Simba alikuwa anatazama michuano ya Vilabu Afrika kwenye Runinga tu! Ndiyo mpira ulivyo wakati mwingine! Simba hakushiriki michuano ama ya Klabu Bingwa au Kombe la Shirikisho Afrika kwa miaka mitano mfululizo na haikuwa dhambi.

Kuna kosa kubwa moja viongozi wa Yanga walilifanya tangu mwanzo wa msimu huu, unakumbuka? Ngoja nikukumbushe.

Walisikika mara nyingi wakisema kwamba msimu huu Ubingwa unaenda Jangwani! Hii ahadi ndiyo inayowatesa kwa sasa. Hii ndiyo ahadi inayoleta presha kubwa sana kwa sasa kwa Wachezaji, Benchi la Ufundi, Viongozi na Mfadhili wao! Yanga wana timu Bora sana msimu huu kuliko misimu mitatu iliyopita lakini bado hawajafikia ubora walionao Simba kwa sasa.

Nafahamu kwenye mchezo wa soka sio lazima uwe bora sana kuliko wote ndiyo ushinde mechi, lakini kwenye kutwaa Ubingwa wa Ligi ni ngumu kubahatisha!
Haijaandikwa kwenye kitabu chochote kwamba Yanga ni lazima na wao wasubiri miaka mitano.

Yanga bado wanahitaji kujenga timu. Bado wanahitaji kuwa na kikosi cha kushindana bila kubahatisha kama ilivyo sasa. Yanga ikimkosa Tonombe Mukoko, haipaswi kuwa na presha.

Inapaswa kuwa na wachezaji kama Mukoko hata wanne kwenye kikosi. Yanga ikimkosa Bakari Mwamnyeto, haipaswi kuwa na unyonge, inapaswa kuwa na kina Mwamnyeto kama watatu. Hiyo ndiyo Yanga inayoshikilia rekodi ya mataji 27 ya Bara.

Hiyo ndiyo Yanga ya Kampa, Kampa tena. Yanga ya sasa imefanya mikutano mingi na Wanahabari ya kulalamikia Waamuzi na TFF kuliko magoli aliyofunga mshambuliaji wao, Michael Sarpong! Yanga ambayo haina hata mchezaji mmoja mwenye mabao sita ya ligi, bado sio Yanga imara.

Yanga hii ya leo hakuna dhambi yoyote kama watapoteza ubingwa msimu huu, hakuna pia dhambi kama Yanga watakuwa Mabingwa kwa sababu kwenye mpira bahati pia ipo.

Kila Simba wanavyozidi kuikaribia kileleni, Yanga wanazidisha mikutano na Wanahabari ya kulalamikia kuonewa na Waamuzi! Yanga haikuwa Bingwa mara nyingi wa Ligi Kuu Tanzania Bara kwa kulalamika, wamekuwa na timu Bora Uwanjani na nje ya Uwanja. Usipokuwa na kikosi kizuri kwenye mpira, utaona unaonewa tu! Usipokuwa na maandalizi mazuri kwenye Soka, utaona hutendewi haki tu!

Huu ni muda mzuri sana kwa Yanga kuendelea kujenga timu bila presha yoyote. Katika miaka mitatu Yanga waliyokosa Ubingwa hivi karibuni, walau msimu huu wameimarika sana. Bila shaka yoyote nguvu aliyoiweka Mfadhili na Mdhamini wao GSM, Muda si mrefu itaanza kuzaa matunda uwanjani.


Kwani kuna dhambi yoyote Yanga akikosa Ubingwa msimu huu?

Wanajua kwamba timu yao sio bora kiivyo. Yanga ndiyo timu pekee Duniani ambayo imewahi kuongoza ligi kwa muda mrefu, tena bila kufungwa mechi hata moja lakini ndiyo yenye wasiwasi kuliko zilizofungwa! Unaijua sababu? Ni moja tu. Wakitoka nje na kuona ubora wa mpinzani wao, nafsi inawaambia muda wowote watafungwa.

Nafsi inawaambia wowote watashushwa kileleni! Ni kweli kuna makosa mengi ya Waamuzi kwenye mpira wetu lakini, kinachowatisha zaidi Yanga ni kasi ya Simba na wala sio makosa ya Waamuzi! Simba na Yanga ndiyo wanufaika wakubwa wa makosa ya uwanjani kwenye Ligi yetu. Ndiyo timu zinazoshinda mechi nyingi kwa matukio ya Kimazingaombwe!

Lakini, wao ndiyo Mabingwa wa kalalamika! Yanga hawatakiwi kujipa presha ya bure, wanapaswa kuendelea kujenga timu. Hakuna haja ya kutoa ahadi kwa mashabiki kwamba wataupata Ubingwa wa msimu huu, wanatakiwa wamkimbize Mwizi kimya kimya!

Mechi zetu bado zinamakosa mengi sana ambayo husababisha timu kubwa kushinda, bado Yanga anaweza kuwa Bingwa msimu huu.

Lakini kwa kutazama Ubora wa timu, sioni dhambi kama Yanga ataukosa Ubingwa!

Ni kweli Yanga yuko kileleni mwa Msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara lakini, hata Ushindi wao tangu mwanzo umekuwa wa Roho Mkononi! Bingwa wa Ushindi wa goli moja! Kila mechi kwa Yanga msimu huu ni kama Fainali.

Mara chache sana msimu huu mashabiki wa Yanga wamekwenda uwanjani wakiwa na uhakika wa kushinda!

Ni kweli mbele za watu wanatamba lakini wakibaki peke yao, wanauona ukweli. Hakuna haja ya kujipa Presha kubwa, Yanga inaimarika. Yanga itakuwa bora tu na Afrika itajua.

Yanga itakuwa bora tu na nchi itajua. Kujipa Presha ya Ubingwa kwa sasa ni sawa na kusubiri “Divisheni Wani” kwenye mtihani wa Taifa wakati mwanao hajawahi kuipata hata kwenye mitihani ya ndani. Kitu pekee ambacho nakiona pale Yanga, ni kuimarika nje na ndani ya Uwanja Kila kukicha. Kuwa na ndoto za Ubingwa ni dhamira ya kila timu kubwa lakini na Yanga wako sawa lakini, dhamira haishindi Uwezo.

Ukubwa na ubora wa Simba ya kizazi hiki, haujaja kwa bahati mbaya. Umejengwa na ukajengeka.

Timu imejengwa kwa Muda mrefu mno na bado inaendelea kujengwa na kuimarishwa kila msimu. Ni rahisi sana kushinda mechi kwa kubahatisha, lakini ni ngumu kushinda Ubingwa! Yanga wapunguze Presha kwenye timu yao, wanaendelea kupambana mchezo wa soka wakati mwingine huwa unaleta matokeo ya kustaajabisha, nawasubiri Yanga wanistajaabishe!

Imeandikwa na OSCAR OSCAR