MZEE WA UPUPU: Povu la Yanga ni hisia na tatizo la matokeo

JUMA lililopita nilikuwa kwenye viunga vya Azam Complex Chamazi, Dar es Salaam kwenye mazoezi ya Namungo FC wakijiandaa na mchezo wao wa Kombe la Shirikisho dhidi ya Primero de Agosto ya Angola.

Siku hiyo Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Innocent Bashungwa aliwatembelea wawakilishi hao wa Tanzania na kuwapa salamu za serikali.

Alipoondoka, nikaendelea kubaki nikisubiri mazoezi yaishe ili nifanye mahojiano na kocha na baadhi ya wachezaji ikizingatiwa siku hiyo Shirikisho la Soka Afrika (CAF) ilitoa uamuzi kwamba mechi zote mbili za Namungo na De Agosto zichezewe Tanzania.

Kiongozi mmoja wa Namungo akawa anahangaika kumpata mtu ambaye atawapokea De Agosto na kuwaongoza wakiwa nchini. Alitaka ampate mtu anayejua Kireno ili kunasa.


UMBEA KIDOGO

Jina lilikokuja la kwanza likawa la Said Maulid, akampigia simu na kumuomba amsaidie hilo kwa sababu yeye ameishi Angola na anakijua Kireno.

Maulid ama SMG alikubali, lakini akasema yeye ni mwajiriwa wa Yanga, hivyo lazima viongozi wake waambiwe ili watoe ridhaa.

Akapigiwa kiongozi mmoja wa Yanga ili atoe ridhaa au asaidie kupatikana kwa ridhaa hiyo. Alichojibu ni habari kubwa sana.

“Nyinyi Namungo hamna urafiki na sisi. Mechi zetu mnatukamia sana, lakini mechi za Simba mnawaachia.

“Tunajua kuna mtu anawapa kiburi sana...na huyo mtu anashirikiana na TFF (Shirikisho la Soka Tanzania) kutuhujumu. Msitarajie sisi kuwasaidia kwa jambo lolote.” Halafu akakata simu.

Yule kiongozi wa Namungo masikini ya Mungu alibaki hoi kwa mshangao.

Siku mbili baadaye, Makamu Mwenyekiti wa Yanga, Fredrick Mwakalebela, aliitisha mkutano na vyombo vya habari kulalamikia hujuma za waamuzi dhidi ya timu yao, akirejea matukio ya kwenye mechi mbili - dhidi ya Mbeya City na Kagera Sugar.

Hakuna shaka kuhusu malalamiko hayo, ni kweli kabisa kwamba Yanga walistahili penalti mbili dhidi ya Kagera Sugar na labda moja dhidi ya Mbeya City.

Na kama wangezipata penalti hizo na kufunga, basi wangejivunia alama sita kwenye mbili zilizopita. Na kama ingekuwa hivyo, wangeendelea kupunga upepo mwanana kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu Bara.

Lakini kwa sababu haikuwa hivyo, ndiyo maana wanatoka povu la kujaza bahari. Wanamchukia kila mtu. Wanamhisi kila mtu na wana mashaka na kila mtu.

Hata hivyo, kimsingi kinachowaumiza Yanga siyo zile penati walizonyimwa, bali matokeo waliyoyaoata.


KWANINI

Mwaka 2004, Manchester United ya Sir Alex Ferguson ilikutana na FC Porto ya Jose Mourinho kwenye hatua ya 16 bora ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Katika mchezo wa mkondo wa kwanza, United walifungwa 2-1 huku nahodha wao Roy Keane, akitolewa nje kwa kadi nyekundu baada ya kumkanyaga mgongoni kipa wa FC Porto, Vitor Baia.

Ferguson alikerwa sana uamuzi ule na baada ya mchezo alikataa kumpa mkono Jose Mourinho kama ulivyo utamaduni.

Ferguson alilalamika kwamba Keane hakumkanyaga Baia, bali kipa huyo alimdanganya mwamuzi ili Keane atolewe.

Waandishi wakamuuliza Mourinho kuhusu wachezaji wake kufanya udanganyifu.

“Hapana. Ni tatizo la matokeo. Kama tungefungwa 5-0, hayupo ambaye angezungumzia udanganyifu,” alisema.

Mourinho akaongeza kwamba alikutana na Ferguson na wakalizungumzia hilo.

“Alinilalamikia kwamba wachezaji wangu wanaigiza sana. Nikamwambia ngoja nikaangalie video ya tukio. Kama kweli wanaigiza nitaomba msamaha. Kama hawaiigizi nitamtaka yeye aombe samahani,” alisema.

Mchezo wa mkondo wa pili ukaisha kwa matokeo ya sare ya bao 1-1 na Manchester United wakatolewa mashindanoni. Safari hii

Ferguson akapeana mikono na Mourinho.

Waandishi wakamuuliza Mourinho kama waliliongelea lile tukio la mechi ya mkondo wa kwanza.

“Hapana. Aliniambia tu, ‘hongera’, na kwangu mimi hiyo inatosha. Unajua mpira una sehemu mbili, hisia na busara. Lakini usije ukadhani upande wa hisia ni wa kijinga,” alisema kocha huyo.


NDIYO YANGA SASA

Ni kweli kwamba Yanga walistahili zile penalti, lakini usifikiri kwamba endapo wangeshinda mechi zile bila penalti wangelalamika namna hii.

Wanalalamika kwa sababu ya matokeo waliyoyapata siyo kingine.

Wanalalamika kwa sababu ya hisia, wanahisi kwamba siku zao za kukaa kileleni zinahesabika.

Kama hoja ni penalti katika hizo mechi mbili, hata wao msimu huu wamefaidika zaidi ya hivyo.

Mchezo wa kwanza dhidi ya Kagera Sugar kule Kaitaba, wenyeji walikataliwa penati dhahiri kabisa. Kama wangepewa penati yao na kufunga, Yanga wasingepata alama tatu siku hiyo.

Mchezo wao dhidi ya KMC pale CCM Kirumba, Yanga walipewa penati ambayo hawakustahili. Wakafunga na kushinda.

Mechi dhidi ya Gwambina pale Misungwi, wapinzani wao walikataliwa bao halali kabisa. Mechi ikaisha sare, Yanga wakapata alama moja.

Mechi dhidi ya Simba, penalti ya Tuisila Kisinda kwa madhambi yaliyofanyika nje ya eneo la hatari.

Chukua alama tatu za Kaitaba, alama tatu za CCM Kirumba, moja ya Gwambina na moja ya Simba, utapata nane, lakini katika hizi walistahili kupata mbili tu...alama sita za makosa ya waamuzi.

Yanga wanaongoza ligi kwa sasa kwa sababu ya zile alama sita za makosa hayo ya waamuzi...siyo kwa uwezo wao pekee.

Waamuzi walikosea kwa wapinzani, wakafaidika wao, leo waamuzi wamekosea kwao wamefaidika wapinzani - ndiyo mpira.

Msimu uliopita Yanga walimaliza nafasi ya pili juu ya Azam FC, lakini siyo tu kwa uwezo wao, bali pia makosa ya waamuzi.

Ruvu Shooting walikataliwa bao lao halali dhidi ya Yanga katika siku ya kwanza msimu.

Lipuli wakakataliwa bao lao dhidi ya Yanga kwenye ule mkasa wa ‘goal corner’.

Polisi Tanzania walikataliwa bao lao dhidi ya Yanga. Azam FC walikataliwa mabao mawili na penalti halali dhidi ya Yanga.

Hayo yote walifaidika Yanga, na wakasema ni makosa ya kibinadamu.

Lakini leo binadamu wale wamekosea upande mwingine, Yanga wanalalamikia hujuma na kutishia kwamba wasipojirekebisha basi watafanya jambo.


Nukuu za Mourinho

“Unajua mpira una sehemu mbili, hisia na busara. Lakini usije ukadhani upande wa hisia ni wa kijinga. Ni tatizo la matokeo. Kama tungefungwa 5-0, hayupo ambaye angezungumzia udanganyifu.”


Imeandiwa na Thabit Zakaria