Kibabe tu!, cheki Namungo ilivyotoboa Caf

SAFARI ya Namungo katika michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika ilianza kama utani, lakini vijana hao wa Ruangwa wako siriaz ile mbaya na tayari wameingiza mguu mmoja kwenye hatua ya makundi.

Haikuwa safari nyepesi kwa Namungo kufikia hatua hiyo, imekutana na changamoto za hapa na pale ikiwamo kushindwa kucheza dhidi ya CD Primeiro de Agosto nchini Angola, baada ya kutolewa taarifa na wenyeji wao kwamba wachezaji Fredy Tangalo, Lucas Kikoti, Hamis Mgunya na mtendaji mkuu Omary Kaaya, wana virusi vya corona, hivyo kutakiwa timu nzima ikae karantini.

Jambo hilo liligomewa na viongozi wa Namungo ambao iliwalazimu kubaki garini, hali iliyosababisha mchezo huo kufutwa kabla ya Kamati ya Caf kuamua mechi zote mbili zichezewe Tanzania.

Katibu wa timu hiyo, Ally Suleiman aligusia baadhi ya changamoto ambazo walikutana nazo Angola kuwa ni kulala na njaa, kukaa garini kwa muda mrefu na hatimaye haki ikapatikana katika mechi yao ya kwanza iliyopigwa Jumapili kwenye Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam kwa De Agosto ambao walikuwa wenyeji wa mchezo kuchapwa mabao 6-2.

Namungo inashiriki kwa mara ya kwanza katika michuano hiyo na imeonyesha uwezo wa kufika hatua nzuri na inahitaji japo sare au kipigo kisichozidi tofauti ya mabao manne ili kuingia hatua ya makundi.

Wakati michuano hiyo inaanza viongozi wa Namungo kupitia kwa Katibu Suleiman, walikaririwa na Mwanaspoti kwamba bajeti yao ilikuwa Milioni 500, ingawa hawakuwa na uhakika wa kufika hatua waliyopo sasa ya mwisho ya mchujo.

Mwanaspoti inakuletea ilichofanya Namungo hadi kutanguliza mguu moja hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika.


INA MABAO 14

Katika mechi nne ilizocheza Namungo imefunga mabao 14, huku straika wao, Stephen Sey ‘Mzee wa Kuwakera’, akiwa anaongoza kwa kutupia matano, jambo linaloonyesha ni timu yenye washambuliaji wazuri.


MATOKEO YA MECHI

Katika mchezo wa kwanza ambao Namungo ilicheza Novemba 28, 2020 dhidi ya Al Rabita, iliibuka na ushindi wa mabao 3-0, yaliofungwa na Stephen Sey aliyetupia mawili katika dakika 20 na 38 na Shiza Kichuya (61). Mchezo wa marudio uliopangwa upigwe Desemba 06, 2020 Al Rabita haikutimiza vigezo hivyo Namungo ikapewa ushindi wa mezani.

Namungo iliendeleza ubabe wake baada ya Desemba 23, 2020 kuichapa Hilal Obayed mabao 2-0, yaliyofungwa na Sixtus Sabilo (dakika 13) na Sey dakika (31) na kisha Januari 05, 2021 timu hizo zilitoka sare ya mabao 3-3, wafungaji wakiwa ni Sey (dakika 2), Blaise Bigirimana (38) na Edward Manyama (50).

Katika hatua ya mwisho ya mchujo wa kuwania kuingia hatua ya makundi imekipiga na 1 de Agosto ikiwa ndio mwenyeji wa mchezo huo uliopigwa Uwanja wa Azam Complex, Namungo ilishinda mabao 6-2 yaliyofungwa na Hashim Manyanya (dakika 32), Sabilo (38, 59), Reliants Lusajo (55), Eric Kwizera (66) na Sey dakika (71).


KAULI ZA WACHEZAJI

Sey ambaye ana mabao matano katika michuano hiyo, anasema kila wanapocheza mechi wanapata morali ya kujituma na kutamani kufika nyingine zaidi wanayoamini itawapa mafanikio makubwa.

“Japokuwa timu inaonekana ni ngeni kwenye michuano hii, tulikuwa tunahamasishana kupambana na kuonyesha nini kipo kwenye miguu yetu. Tunachokiangalia kwasasa ni mechi ya marudiano na Agosto. Tukishinda ama kutoka sare tutaingia hatua ya makundi,” anasema.

Naye Adam Salamba anasema hadi timu ilipofikia inawapa moyo wa kuendelea kupambana kuhakikisha wanapeperusha vyema bendera ya Tanzania kwa timu wanazocheza nazo.

“Sio michuano myepesi, lakini pia ina faida kwetu kwani anayefanya vizuri ni rahisi kuonekana na timu nyingine za nje,” anasema.


NENO LA WADAU

Beki wa zamani wa Simba na Taifa Stars, Boniface Pawasa anasema japokuwa Namungo haikutazamwa kwa jicho kubwa kama ilivyo kwa Simba inayoshiriki Ligi ya Mabingwa Afrika, anaielezea kwamba imepambana na kuonyesha inawezekana.

“Binafasi nawapongeza wachezaji, benchi la ufundi na viongozi wote kwa ujumla kwa namna walivyopambana na kuipeperusha bendera ya taifa kwa ushindi dhidi ya wale ambao wamecheza nao,” anasema.

Naye Edibily Lunyamila anasema Namungo inapambana na nyakati ngumu, akitolea mfano kilichowatokea Angola kwamba hakijawakatisha tamaa badala yake kimewapa nguvu ya kupambana zaidi.

“Pamoja na ugeni wao kwenye michuano ya kimataifa, naamini imeandikwa historia ya timu za Tanzania zimefanya kitu cha tofauti, hivyo nawashauri wachezaji waendelee kukaza buti kwa hatua zaidi,” anasema.