Tamu, chungu Pablo wachezaji Simba

JUZI, Simba ilitinga kwa mara ya kwanza hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika licha ya kufungwa bao 2-1 na Red Arrows jijini Lusaka, Zambia.
Ushindi wa bao 3-0 walioupata Simba nyumbani dhidi ya Arrows, Novemba 28 ndio umewapa nafasi ya kusonga makundi kwa jumla ya mabao 4-2.
Kupitia makala hii, Mwanaspoti linakuletea uchambuzi wa mechi ya juzi kuelekea kwenye hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho ambapo malengo ya Simba ni kufika nusu fainali baada ya kuikosa Ligi ya Mabingwa kwa kutolewa na Jwaneng Galaxy ya Botswana katika hatua za awali.
MCHEZO ULIVYOKUWA
Kocha mkuu wa Simba, Pablo Franco alifanya badiliko moja tu katika kikosi chake kilichoanza juzi kwa kumuingiza beki wa kati, Henoc Inonga kuchukua nafasi ya Joash Onyango aliyeanza kwenye mchezo wa kwanza Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.
Wengine walikuwa walewale kina Aishi Manula, Israel Mwenda, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’, Pascal Wawa, Jonas Mkude, Hassan Dilunga, Rally Bwalya, Meddie Kagere, Benard Morrison na Sadio Kanoute.
Simba iliingia katika mchezo ule ikicheza kwa kujilinda na kushambulia kwa kushtukiza na walifanikiwa kufanya hivyo hadi dakika ya 44 waliporuhusu bao lililofungwa na Ricky Banda na kipindi cha kwanza kumalizika kwa Simba kuwa nyuma kwa bao 1-0 dhidi ya Red Arrows.
Kipindi cha pili kilirejea kwa Arrows kuendelea walipoishia kwani dakika ya 47 Saddam Phiri alitupia bao la pili na kuamsha morali ya wachezaji wa timu hiyo huku wale wa Simba wakipoteana.
Kasi ya Arrows katika kushambulia ilikuwa ya hali ya juu na kuwafanya Simba muda mwingi wacheze nyuma ya mpira wakikaba, huku Arrows wakiendelea kutafuta bao la tatu ili kusawazisha mabao ambayo walifungwa kwa Mkapa.
Wakati huo, Simba waliendelea kukaba kwa makini na kushambulia kwa kushtukiza na dakika ya 67 Dilunga aliwamaliza nguvu wachezaji wa Arrows baada ya kuifungia Simba bao pekee katika mechi hiyo na kuongeza mlima kwa Arrows ambao walihitajika kushinda 5-1 ili kusonga mbele.
Baada ya hapo Pablo alijilipua na kufanya mabadiliko yaliyoashiria kutaka kulinda zaidi kwa kuwatoa viungo Bwalya na Morrison na kuwaingiza mabeki Onyango na Kapombe ambao waliongeza nguvu eneo la ulinzi.
Pia, kiungo mkabaji Mzamiru aliingia kuchukua nafasi ya Dilunga na Bocco akachukua nafasi ya Kagere na kuingia kuwabana Arrows ambao walikuwa wamoto zaidi kuliko Simba.
Kwa ufupi Simba haikucheza soka la kuvutia, lakini ilijitahidi kutengeneza nafasi chache za mabao lakini hazikuzaa mabao hadi Dilunga alipofunga kwa juhudi zake binafsi.
PABLO KAZI ANAYO
Licha ya kuipeleka Simba makundi kocha Pablo bado ana kazi ya kufanya marekebisho na kuongeza ubora na morali ya wachezaji kuelekea katika mechi za makundi.
Simba inavyocheza sasa ni tofauti na ile ya msimu uliopita, baadhi ya wachezaji wa kikosi hicho waliokuwa bora msimu uliopita msimu huu viwango vyao vimeshuka.
Hilo ni jambo ambalo kocha huyo anatakiwa kuanza nalo. Simba ina wachezaji zaidi ya 25, wengi wao viwango vinalingana kwa sasa na wachache wapo juu ilhali wengine chini zaidi, hivyo kocha anatakiwa kutoa nafasi kwa kila mchezaji kucheza ili kubaini nani na nani watafiti zaidi kwenye mifumo yake mbalimbali kisha kuanza kuwapa maelekezo mengi ya kimbinu.
Katika hatua ya makundi Simba itakutana na vigogo wengine kutoka Afrika, hivyo Pablo anahitaji kuwa na uharaka wa kuwasoma na kuwaelewa wapinzani, kuweka timamu miili ya wachezaji na kuelekeza mbinu mbalimbali ambazo watazitumia katika michezo ya hatua ya makundi nyumbani na ugenini.
WACHEZAJI HAPA TU
Wachezaji wote wa Simba watakiwa kuongeza vitu - iwe kwa kutaka au lazima ili kuhakikisha wanafikia malengo yao ya kufika nusu fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika.
Kujituma ni jambo la kwanza ambalo linaambatana na uzalendo kwa timu. Kila mchezaji anapaswa kujituma na kuwa mzalendo katika kuipambania timu kwani macho ya mashabiki na wadau wa soka Tanzania na Afrika Mashariki yapo kwao.
Pili, wachezaji wa Simba wanapaswa kutumia vyema uwanja wa nyumbani katika hatua ya makundi na pia kutumia kila nafasi wanazopata kufunga ikiwemo kutengeneza nafasi tofauti na wanachofanya kwa sasa.
Ushirikiano na maelewano mazuri wao kwa wao ni silaha nyingine ambayo itaifanya Simba kufikia malengo na kama yote hayo yakifanyika kwa ufasaha, basi huenda wakavuka makundi na kuingia robo fainali hadi nusu fainali wanapotaka.
WASIKIE MAKOCHA
Kocha mkuu wa chama hilo, Pablo anaeleza kuwa wachezaji wamefanya kile alichokitaka na sasa anarudi kambini kujiandaa na mechi zijazo.
“Nimefurahi kwa sababu yametimia malengo ya Simba kuendelea kuwa kwenye michuano ya kimataifa na sasa tumetinga hatua ya makundi. Sasa tunaenda kujipanga zaidi kwa ajili ya mechi zijazo,” alisema Pablo.
Nyota na kocha wa zamani wa timu hiyo, Abdallah Kibadeni anasema juhudi na kucheza mechi kwa kutafuta ushindi ndivyo vitu Simba wanatakiwa kufanya kuelekea mechi za hatua ya makundi.
“Michuano hii inaamuliwa na matokeo. Wachezaji wanatakiwa kuongeza juhudi na kupambana zaidi ili kuhakikisha timu inapata ushindi, iwe nyumbani au ugenini. Wanahitaji kuchanga vyema ratiba zao ili wasonge mbele zaidi,” alisema Kibadeni.
Kocha wa Red Arrows, Osward Mutapa anawatahadharisha Simba akisema: “Nawapongeza Simba kwa kusonga mbele lakini wanahitaji kuhakikisha wanatengeneza timu imara zaidi kuelekea mechi za makundi.”