Prime
Swanga na rekodi mbovu ngumi za ridhaa, tamu za kulipwa

Muktasari:
- Swanga ni mmoja kati ya majina ya mabondia wachache wa ngumi za kulipwa katika uzani mkubwa yaani heavy wanaopambana kurudisha heshima ya mabondia wa uzani huo ambao kawaida umekosa ushindani kama miaka nyuma kutokana na uchache wa mabondia wake.
HARUNA Mhando Swanga, mkali wa masumbwi kutoka Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanazania (JWTZ) akiwa na cheo sajini taji (staff seargent) huku akiwa ndiye nahodha wa gym ya Ngome inayopatikana kwenye kambi JWTZ Lugalo, Mwenge.
Swanga ni mmoja kati ya majina ya mabondia wachache wa ngumi za kulipwa katika uzani mkubwa yaani heavy wanaopambana kurudisha heshima ya mabondia wa uzani huo ambao kawaida umekosa ushindani kama miaka nyuma kutokana na uchache wa mabondia wake.
Kwa mujibu wa rekodi yake inayotambulika na mtandao wa Boxrec, Swanga amepanda ulingoni katika mapambano matano kati ya hayo mawili katika ngumi za ridhaa ambayo amepigwa yote na matatu katika ngumi za kulipwa ambayo ameshinda yote kwa knockout.
Bondia huyo anakamata nafasi ya pili katika mabondia tisa wa uzani wa juu nchini wakati duniani akiwa wa 444 katika mabondia 1559 wa uzani huo akiwa na uwezo wa kushinda kwa knockout kwa asilimia 100, huku akiwa na hadhi nusu nyota.
Swanga amefanya mahojiano maalumu na Mwanaspoti, ambapo amezungumza mambo mengi ikiwemo kilio chake cha mabondia wa uzani wake kutopewa nafasi ya kupigana katika majukwaa makubwa tofauti na miaka ya nyuma, hali inayofanya wengi kukaa pembeni kwa kuwa mapromota hawapo upande wao.

Bondia huyo anaeleza kuwa ugumu wa maisha ndiyo sababu kubwa iliyofanya aingie katika mchezo huo kwa kuwa hakujua sehemu itayakayompa ugali wa uhakika kwa kila siku katika maisha yake.
"Unajua kitu kilichonifanya niingie kwenye mchezo wa ngumi, suala la kwanza nitakwambia kuwa ni ugumu wa maisha kwa sababu nimetokea katika maisha magumu kiasi kwamba sijui hata kesho yangu," anasema Swanga.
"Lakini suala la pili ambalo limenifanya niingie huku limetokana na tabia ya kutokupenda kuona watu wakionewa. Hata mimi mwenyewe sipendi kuonewa tabia ambayo imejijenga hadi sasa.
"Wakati naendelea na mchezo huo ndiyo nilipata nafasi ya kujiunga na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) mwaka 2004, nashukuru nilipata bahati ndani ya mwaka huo nikapandishwa kupigana kwa sababu kwangu naona haikuwa rahisi.
"Niliendelea kupigana pale na mara nyingi nilikuwa nashika nafasi ya pili. Wakati huo nilikuwa napigana kama raia ndani ya JKT na mwaka 2006 ndiyo nikaajiriwa na Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) kilichonifanya niajiriwe ni mchezo wa ngumi.

"Lakini nakumbuka sikuwa peke yangu alikuwepo Selemani Kidunda, Machichi na mabondia wengine ambao tuliajiriwa kwa wakati huo. Tangu mwaka 2006 nilipoingia JWTZ nilikuwa napigania ngumi za ridhaa ingawa ngumi za ridhaa nilianza mwaka 2004, mwaka 2021 ndiyo niliingia kwenye ngumi za kulipwa kutoka kwenye ridhaa nikiwa bingwa wa taifa.
"Katika ngumi za ridhaa si haba kwa sababu nimefanikiwa kupata medali za dhahabu nyingi ikiwemo za mashindano ya kimkoa na kitaifa zipo nyingi. Lakini wakati napigana kwenye ngumi za ridhaa, nimeshiriki mashindano makubwa mbalimbali kama Jumuiya ya Madola, nimeshiriki mara tatu Gold Coast mara moja na Senegal.
"Nashukuru kwa hatua hiyo kwa sababu katika mashindano hayo makubwa nilikuwa najifunza mambo mengi muhimu, ikitokea nakuwa mwalimu wa mchezo huu yaweze kunisaidia katika kazi yangu.
Kuhusu ndoto yangu nilitamani kuona nafika katika mashindano ya Olimpiki, lakini sijawahi kufika kabisa kushiriki katika mashindano hayo makubwa.
"Mwaka 2021 niliingia katika ngumi za kulipwa na pambano langu la kwanza nilimpiga mtu kwa knockout, lakini niliendelea kufanya vizuri na sasa naushikilia mkanda wa ubingwa wa taifa wa uzani wa juu."

SWALI: Unasema ulikuwa hupendi kuonewa, je uliwahi kuonewa huko nyuma?
JIBU: "Hapana, kusema ukweli sijawahi kuonewa katika maisha yangu ila tu sipendi kuona mtu akiwa anaonewa, zaidi nilikuwa mtaalamu wa kukamata vibaka hasa wakati nilipokuwa raia na ili kujilinda ndiyo nikajifunza ngumi.
"Unajua hadi leo hii moyo wangu hautaki kuona mtu akipigwa mbele yangu, lakini zaidi nampenda sana mama yangu hivyo nikiona mwanamke anaonewa jua huo ugomvi nitaununua.
"Hata ukiangalia namna naingia jeshini, usaili wangu ulikuwa mnapigana watu wawili kabla ndiyo maana watu wengi wanashindwa kuelewa urafiki wangu wa Selemani Kidunda maana tulipigana ndiyo tukachukuliwa.

SWALI: Tangu umeingia kwenye ngumi za kulipwa umeona tofauti gani na ngumi za ridhaa?
JIBU: "Yaani ngumi za kulipwa imejaa kunyenyekea, yaani promota anataka anyenyekewe ndiyo akupe pambano. Hilo limekuwa likitupa ugumu wa kupata mapambano ya mara kwa mara.
"Lakini pia mabondia wa uzani wa juu wameshatengwa siyo kama zamani. Ukiangalia kama mimi umri unaenda hakuna mapambano ya haraka haraka, lakini promota anataka umlambelambe, umsujudie hata pesa zenyewe wanakupangia wao.
"Unajua ndiyo maana hata walivyokuwa Azam na bora warudi, heshima yangu itakaa kwenye mahali pake maana sasa hivi ngumi zimepoteza heshima yake. Ni'shasafirishwa hadi Tanga kwa gharama zangu, halafu nikakosa pambano ila wakati wa Azam hayakuwepo mambo hayo.
"Kuna wakati nawaza tulishauri hata jeshi lianzishe promosheni yake ili mabondia wa jeshi waweze kupigana, jambo ambalo linawezekana kabisa, lakini siyo mambo ya kuomba kwa promota wengine ambayo kila mmoja ana mabondia wake ambao hataki wapigwe. Kuna changamoto nyingi ambazo nilikuwa sizijui kwenye ngumi za kulipwa sasa nazijua."
SWALI: Kwenye ngumi za kulipwa ni kiasi gani kikubwa cha fedha ulichowahi kulipwa?
JIBU: "Nakumbuka ilikuwa ni Dola 1,000 ambayo ilikuwa ya kubembeleza promota.

SWALI: Mchezo wa ngumi unatajwa kujaa tuhuma za ushirikina, kwa upande wako vipi?
JIBU: "Sijawahi kukutana na hayo mambo kwa sababu naamini kwenye mazoezi na bidii. Ukiangalia umri wangu umeenda naenda kukutana na mtu wa damu changa nifanye nini ili nimshinde zaidi ya kufanya mazoezi peke yake.
"Nimeona hata katika bao alilofungwa Simba dhidi ya Azam ni kutokana na Mohamed Hussein 'Tshabalala' kuzidiwa spidi ya mbio na Zidane Seleli ambaye anaonekana ni damu changa tofauti na Tshabalala ambaye ukweli umri umeenda."