Prime
Soka la kisasa lilivyohamia kwenye maroboti

Muktasari:
- Patrice Evra anasema hivi: “Kwa sasa tuna maroboti. Hata kwenye shule za kufundishia mpira (academy), kila mtu anataka kucheza kama Pep Guardiola. Hakuna ubunifu, hakuna wale majiniazi wa soka. Huwezi kumwona mchezaji kama Ronaldinho au Eden Hazard tena kwa sababu tangu utotoni makocha wanawaambia watoto ‘kama hupasii mpira kwa mwingine, anakuweka benchi.”
PATRICE Latyr Evra. Beki wa kushoto wa zamani wa klabu kibao vigogo huko Ulaya kama AS Monaco, Manchester United, Juventus kwa kuzitaja kwa uchache pamoja na timu ya taifa ya Ufaransa, amekiri kushtushwa kwa kitendo cha mchezo wa soka kwa sasa kugeuzwa roboti.
Patrice Evra anasema hivi: “Kwa sasa tuna maroboti. Hata kwenye shule za kufundishia mpira (academy), kila mtu anataka kucheza kama Pep Guardiola. Hakuna ubunifu, hakuna wale majiniazi wa soka. Huwezi kumwona mchezaji kama Ronaldinho au Eden Hazard tena kwa sababu tangu utotoni makocha wanawaambia watoto ‘kama hupasii mpira kwa mwingine, anakuweka benchi.”
Evra anachojaribu kusema ni kwamba wanasoka wa kisasa hata awe na ujuzi na ufundi kiasi gani wa kuonyesha ubora wake wa kupiga chenga, hatakubaliwa kufanya hivyo na badala yake atacheza kwa maelekezo maalumu ndani ya uwanja. Hiyo ina maana wachezaji kama Austin Jay Jay Okocha, Ronaldinho, Eden, Denilson wangepata shida kucheza soka la kisasa.
Udambwidambwi kwenye soka umepungua na ndio maana vitu vinavyofanywa na wachezaji kama Lamine Yamal na Pacome Zouzoua ndani ya uwanja vimekuwa adimu kwenye soka la kisasa kwa sababu wachezaji wengi wanacheza kwa maelekezo kwa vile soka lenyewe limekuwa lenye kujali matokeo zaidi kuliko kuburudika.
Hata hivyo, hilo limetokana na mapinduzi yanayofanyika kwenye mchezo wa soka kwa sasa wa utambulisho wa roboti katika mambo mbalimbali kama nyenzo muhimu kuanzia mazoezini hadi kweye mechi. Wakati mwanasoka binadamu akiwekwa uwanjani na kupangiwa majukumu maalumu ya kufanya ndani ya uwanja na si vinginevyo, imekuwa kama roboti.
Sikia kisa hiki
Supastaa Thierry Henry aliwahi kutolewa uwanjani na kocha Guardiola wakati anakipiga Barcelona kwa sababu tu aliondoka kwenye eneo ambalo alipangiwa kucheza. Henry alitolewa uwanjani baada ya kufunga bao dhidi ya Sporting Lisbon, lakini alifunga bao hilo baada ya kuondoka kwenye eneo ambalo alipaswa kucheza.
Henry aliondoka kati na kwenda pembeni na kufunga bao hilo, lakini alitolewa kwa sababu Guardiola hakutaka aondoke kwenye eneo hilo kutokana na mipango yake ya kiufundi. Guardiola alimtoa Henry wakati wa mapumziko na kumwingiza Bojan Krkic, kitu ambacho kilithibitisha kwamba wachezaji sasa wamebadilishwa maroboti ndani ya uwanja, kwamba wanapaswa kucheza kwa maelekezo pekee na siyo kujiongeza.
Roboti mchezaji
Kuna utafiti umefanyika na kugundua tu roboti anaweza kuwa mchezaji makini uwanjani. Kwamba, anaweza kukimbia eneo kubwa bila ya kuchoka, hata kama atavunjika mguu itakuwa rahisi kumrekebisha na kurudi uwanjani kuendelea na mechi. Huo ndio mpango uliopo mbele, japo utachukua muda kiasi kuanza kuona mechi ya maroboti yasiyokuwa binadamu uwanjani. ARTEMIS ni roboti iliyotengenezwa ili kuja kuleta ushindani kwenye soka la dunia. Kwamba roboti hiyo imetengenezwa na kuwekewa uwezo wa ujuzi kumzidi Lionel Messi.

Hata hivyo, hilo limekuja baada ya soka lenyewe kuwa mchezo wenye matumizi mengi ya roboti zilizowekewa akili mnemba ili kusaidia waamuzi, wachezaji, makocha na mabosi wa timu hizo.
Ukiweka kando ishu ya wanasoka kugeuzwa kama maroboti ndani ya uwanja kwa sasa, mchezo wa soka kwa sasa umezungukwa na vifaa vingi vinavyotumia akili mnemba pamoja na roboti, ambavyo vinafanya mambo kuwa mepesi kwenye uamuzi na ufundishaji.
Teknolojia mpirani
Katika enzi ya maendeleo ya sayansi na teknolojia, michezo mingi ikiwemo soka imeanza kutumia roboti na mifumo ya akili mnemba (AI) katika nyanja mbalimbali za mchezo huo. Soka sasa imekaribisha teknolojia ya kisasa kabisa kwa utambulisho wa roboti ambazo zimekuwa zikisaidia kuboresha uamuzi, mafunzo, uchambuzi wa data na hata uzoefu wa mashabiki. Zifuatazo ni baadhi ya roboti au mifumo ya kiteknolojia (robotic systems) maarufu inayotumika kwenye soka kwa sasa.
1. VAR (Video Assistant Referee) – Roboti Mwamuzi
Ingawa siyo roboti kwa umbo la kawaida, VAR ni mfumo wa kielektroniki unaotegemea kamera na AI kusaidia waamuzi kufanya uamuzi sahihi. Unatumika kuchunguza matukio ya kuotea, faulo, na mabao. Mfumo huo unashirikiana na teknolojia nyingine kama Hawk-Eye, ambao ni mfumo wa kamera wa hali ya juu unaosaidia kuangalia kama mpira umevuka mstari wa goli ili ithibitike kuwa ni bao endapo kama umeshindwa kugusa nyavu.

Pia kuna Semi-Automated Offside Technology ambao ni mfumo unaotumika katika mashindano kama Kombe la Dunia la Fifa, ukitumia kamera 12 na AI kutambua nafasi za wachezaji kwa sekunde chache kama alikuwa kwenye eneo la kuotea au la.
2. RoboKeeper – Roboti Golikipa
Hii ni roboti maarufu inayotumika kwenye maonyesho na mafunzo. RoboKeeper ina uwezo wa kuzuia penalti kwa usahihi mkubwa kwa kutumia kamera za kasi na AI kutabiri wapi mpira utaelekea. Imetengenezwa nchini Ujerumani na hutumiwa na timu mbalimbali kwa mazoezi ya kupiga penalti.

Kuna video kadhaa mtandaoni zinazoonyesha wanasoka mbalimbali maarufu akiwamo Messi, Ronaldinho na David Beckham wakipiga penalti kujaribu ‘kumfunga kipa roboti’.
3. Footbonaut – Roboti ya Mafunzo ya Pasi
Footbonaut ni mfumo wa roboti unaotumika kufundisha usahihi wa pasi na uamuzi wa haraka. Inatumika na klabu maarufu za Ulaya kama Borussia Dortmund ya Ujerumani. Mchezaji huingizwa ndani ya chumba maalumu ambapo mipira hutupwa kutoka pande mbalimbali na mchezaji anatakiwa kurudisha haraka. Hii husaidia kuongeza kasi ya uamuzi wa haraka uwanjani wakati wa mechi.
4. Playermaker – Kifaa cha Roboti cha kichwani au kwenye miguu
Hiki ni kifaa kidogo cha kielektroniki kinachovaliwa kwenye viatu vya wachezaji. Huchambua harakati za miguu, kasi, nguvu ya kupiga mpira, na mwelekeo.

Ingawa siyo roboti kamili, ni sehemu ya teknolojia ya AI inayosaidia makocha kutathmini wachezaji kwa usahihi.
5. Veo Camera – Kamera ya Roboti kwa ajili ya kurekodi na kuchambua mechi
Veo ni kamera inayotumia akili mnemba inayoweza kurekodi mechi na kuchambua matukio bila kuhitaji mpiga picha. Inatumika sana kwenye timu za vijana na kwenye mazoezi ya akademia.

Roboti hii husaidia pia kwenye uchambuzi wa video kwa ajili ya mafunzo ya makocha kwa wachezaji baada ya tathmini ya mwenendo wa mechi au mazoezi yalivyokuwa.
6. STRIVR na Rezzil – Roboti za mazoezi ya akili kwa Teknolojia ya VR
Hizi ni programu za mafunzo zinazotumia Virtual Reality (VR). Zinasaidia wachezaji kujifunza mbinu, kufanya uamuzi wa haraka na hata kurekodi kasi ya ufikiri wao. Timu nyingi hutumia kwa makocha wa akili (mental coaching).

Hitimisho
Matumizi ya roboti katika soka yanaendelea kubadilisha mchezo huu kuwa wa kisasa zaidi, unaotegemea ufanisi na usahihi. Roboti kama RoboKeeper, Footbonaut, na mifumo ya VAR siyo tu huongeza ubora wa mchezo, bali pia husaidia kuibua vipaji na kupunguza makosa ya kibinadamu. Kwa nchi zinazoendelea kama Tanzania, teknolojia hizo zinaweza kuwa chachu ya mageuzi iwapo utawekwa mkazo kwa timu mbalimbali pamoja na akademia.