Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

KANU: Kiungo aliyestaafu soka anayefanya maajabu Nigeria

Muktasari:

  • Katika orodha hiyo anayeonekana kuwa karibu sana na timu ya Nigeria ni Kanu ambaye huambatana na timu ya Nigeria inapokwenda nje kwa michezo ya kimataifa.

NIGERIA imetoa wachezaji wengi maarufu wa kandanda katika miaka iliyopita na majina kutawala kurasa na vipindi vya michezo katika redio na runinga. Orodha ni ndefu, lakini miongoni mwa waliotamba ni Jay-Jay Okocha, Rashidi Yekini, Victor Osimhen, Nwankwo Kanu, Stephen Keshi, John Obi Mikel, Segun Odegbami, Vincent Enyeama na Taribo West.

Katika orodha hiyo anayeonekana kuwa karibu sana na timu ya Nigeria ni Kanu ambaye huambatana na timu ya Nigeria inapokwenda nje kwa michezo ya kimataifa.

Sasa ni miaka 14 tangu Kanu alipostaafu, lakini anaonekana kupata umaarufu zaidi na kupendwa na wananchi wa Nigeria, na nje kuliko alivyosakata kabumbu kwa karibu miaka 20 (1992-2012). Aliichezea timu ya taifa ya Nigeria (Super Eagles) kwa miaka 18 kati ya hiyo 16 akiwa nahodha na kuifungia mabao 133.

Vilevile alichezea klabu za Ajax ya Uholanzi, Inter Milan ya Italia na Arsenal, West Bromwich Albion na Portsmouth za England. Alisaidia Nigeria na klabu alizozichezea akiwa mfungaji wa kutegemewa na mara mbili alikuwa mchezaji bora wa kandanda Afrika miaka ya 1997 na 1999.

Alipokuwa anacheza alihesabika kuwa mmoja wa wachezaji warefu sana wa Afrika akiwa na futi 6 na inchi 6. Wakati huo  hadi sasa hakuna mchezaji aliyemkaribia kwa ukubwa wa kiatu alichovaa yaani namba namba 15 au 16.

Kwa sasa wachezaji wanaovaa viatu vikubwa ni Paul Bogba wa Ufaransa aliyekuwa Juventus ya Italia (10.5), Thibaut Courtois wa Ubelgiji anayeichezea Real Madrid (11) na Zlatan Ibrahimovich wa Sweden ambaye ni mshauri wa Inter Milan ya Italia. Wengine ni Manuel Neur wa Ujerumani anayechezea Bayern Munich (12.5), Harry Maguire wa England (Manchester United) 13 na Romelu Lukaku wa Ubelgiji anayeichezea Napoli ya Italia.

Kwa sasa anayevaa kiatu kikubwa sana duniani ni kijana wa miaka 28 wa Venezuela anayecheza mpira wa kikapu, Jeison Rodrigues Hernandez. Kijana huyo mwenye urefu wa futi 7 na inchi 3 anavaa kiatu namba 15.79 mguu wa kulia na 15.5 mguu wa kushoto. Kampuni ya Ujerumani, Georg Wessels ndio inayomtengenezea viatu na hivi karibuni ilimkabdhi jijini Caracas, Venezuela jozi 70 za viatu vya aina mbalimbali.

Tofauti na wachezaji wengi wa Afrika wanaokwenda kucheza Ulaya, Kanu aliporudi nyumbani akiwa na utajiri wa fedha na rasilimali za zaidi ya Dola 100 milioni hakuonyesha majivuno. Familia, marafiki, majirani zake na wachezaji wenzake wa zamani wanafaidika na utajiri wake.

Haikushangaza kuona watu wapatao 15,000 waliofika Uwanja wa Teslim Balogun, Lagos, walibubujikwa machozi Kanu alipozunguka na kuwaambia “kwaherini”. Hali hiyo ilimfanya Kanu kutokwa machozi na kusema: “Nawaaga kama mchezaji hapa uwanjani, lakini tutakuwa pamoja wakati wa furaha na dhiki. Naomba muniamini.”

Kanu ametimiza ahadi na kumfanya kupendwa na wadogo na wakubwa kuliko alipolikuwa akisakata kabumbu. Hii inatokana na kusaidia zaidi ya watu 700 wengi watoto waliosumbuliwa na ugonjwa wa moyo na kukata tamaa ya kupata ahueni.

Watoto walipatiwa matibabu Uingereza, India, Israel na Nigeria. Karibu kila siku vyombo vya habari vya Nigeria vina  habari za misaada anayotoa kwa watu wa makabila mbalimbali na rika tofauti. Vilevile anasaidia vijana waliokwama kuendelea na masomo kutokana na wazazi kuwa masikini, na amefungua hospitali, vituo vya afya, michezo na maktaba kila pembe ya Nigeria.

Watu wenye ulemavu zaidi ya 400 amewapatia vyombo vya kuwasaidia usafiri na huduma za kuwapunguzia shida za maisha.

Kanu ambaye amejenga nyumba nyingi Lagos katika eneo la Victoria Island na kuzikodisha, hoteli ya kitalii na kumiliki mashamba mengi siyo mtu mwenye mbwembe wala dharau.

Alizaliwa siku inayoitwa Nkwo (gulio) kwa lugha ya watu wa kabila la Igbo wanaoishi Kusini-mashariki mwa Nigeria. Mwaka 1996 alipata ugonjwa wa moyo na kufanyiwa upasuaji, na wengi waliamini huo ulikuwa ndio mwisho wake kucheza kandanda.

Lakini, alirudi uwanjani na nguvu mpya akacheza vizuri zaidi na baada ya kupona alianzisha taasisi ya moyo inayosaidia watoto wenye ugonjwa huo.

Mwaka 2012 alifungua kituo cha michezo alichokipa jina lake na hapo vijana wanajifunza kandanda na mpira wa kikapu.

Amekuwa akiwaalika wachezaji mashuhuri wa Afrika, Ulaya na Marekani kutoa mafunzo kwa vijana waliojiunga na kituo hicho.

Vilevile amefungua kituo cha sanaa kinachopiga picha, kurekodi nyimbo, michezo ya kuigiza na sinema ambacho hutoza ada nafuu ukilinganisha na vituo vingine.

Pia Kanu anamiliki shule ya kandanda nchini Canada na hupeleka watoto wa Nigeria wa umri wa chini ya miaka 17, na wengi wao baada ya kumaliza mafunzo wamekuwa wachezaji wa kutegemewa wa klabu za Ngeria, Ulaya na timu ya taifa ya Nigeria.

Vilevile anatoa mafunzo kwa waamuzi wa michezo mbalimbali na ni mdhamini wa timu ya kijijini kwao alikozaliwa inayoitwa

Papilo FC. Mara nyingi timu hiyo ikicheza huingia uwanjani na kucheza na vijana kwa dakika chache. Miaka saba iliyopita aliandaa maonyesho ya michezo sehemu nyingi za Nigeria na kuwaalika wachezaji 46 waliowika Afrika, Ulaya na kwingineko.

Hawa ni marafiki zake ambao walifika Abedi Pele, Sammy Kuffour na Tony Baffoe (Ghana). Wengine ni Patrick Mboma wa Cameroon, Anthony Baffoe (Ghana), Kalusha Bwalya (Zambia), Didier Drogba (Ivory Coast), Samuel Eto’o (Cameroon), El-Hadji Diouf (Senegal), Frederic Kanoute (Mali) na Benni McCarthy, Lucas Radebe, Mark Fish na Phil Masinga wa Afrika Kusini. Pia wengine ni Austin Jay Jay Okocha, Daniel Amokachi, Celestine Babayaro, Garba Lawal, Victor Ikpeba, Taribo West, Uche Okechukwu, Peter Rufai, Emmanuel Amuneke na Samson Siasia wa Nigeria.

Fedha zilizopatikana katika michezo hiyo iliyovutia maelfu ya watazamaji na wadhamini wa kampuni mbalimbali zilisaidia kuwatibu watoto wenye maradhi ya moyo. Hivi karibuni alijenga hospitali ya kisasa katika Jiji la Abuja, makao makuu ya Nigeria na anakusudia kujenga zingine nne katika nchi za Kiafrika – Kaskazini, Kusini, Mashariki na Magharibi.

Kanu katika mipango yake anawashirikisha wachezaji mashuhuri waliokuwa bora wa mwaka wa Afrika kina Roger Milla wa Cameroon na George Weah wa Liberia. Pia anazisaidia kimyakimya familia za wachezaji wenzake ambao hawana maisha mazuri baada ya kustaaafu.

Katika miradi yake amewaajiri watoto na wanafamiia wa wachezaji wa zamani wa Nigeria. Anachofanya Kanu ambaye sasa ana miaka 48 ni mfano wa kuigwa na wanamichezo wengine wa Afrika wanaofanya vizuri wanapochezea klabu kubwa duniani.