SPOTIDOKTA: Tatizo la mvutiko mkali wa misuli kwa wanasoka

HIVI sasa Ligi mbalimbali duniani zinaelekea kwisha na huku pia baadhi ya timu ziko katika hatua za fainali katika mashindano mengine.
Mfano kwa hapa Tanzania klabu ya Yanga iko katika fainali ya kombe la shirikisho la Afrika CAF na huku pia imetinga fainali ya kombe la Shirikisho Azam 2023.
Kimataifa klabu ya Soka ya Manchester City ikiwa imeishatawazwa kuwa mabingwa wa ligi kuu ya EPL lakini pia imetinga fainali ya kombe la FA na huku pia imetinga fainali ya ligi ya mabingwa Ulaya UEFA.
Wiki iliyopita tuliona kuwa moja ya nyenzo ya timu hizi kufika hatua hizi ni utimamu wa mwili wa wachezaji walionao.
Vile vile tuliona kuwa majeraha ni moja ya vitu vinavyochangia kuharibu utimamu wa mwili hivyo kucheza chini ya kiwango.
Mchezo wa soka ni moja ya mchezo unaohusisha kukumbana kimwili lakini eneo ambalo linaathirika zaidi ni eneo la miguu.
Mchezaji wa soka anatumia miguu kupiga, kukaba, kukimbia na kuruka hivyo kumfanya kuwa katika hatari ya kupata majeraha.
Katika miguu misuli ndio inawezesha mwanasoka kufanya kila kitu ndio maana maelfu ya wacheza wa soka duniani wanapata majeraha ya misuli.
Katika maisha ya mwanasoka ni kawaida kumwona ghafla akishika nyuma ya paja kama ishara ya kuhisi maumivu.
Baadaye ni kawaida pia kumwona mchezaji alikitoa ishara yakuhitaji kubadilishwa kutokana na hali hiyo ya maumivu.
Kitabibu huwa  ni sahihi kabisa kwa mchezaji kutoa ishara kwani kuendelea kukomaa kucheza ndio kunaongeza ukubwa wa jeraha.
Ni jambo ambalo wachezaji wengi wakulipwa wanalijua vyema pale wanaochezewa faulo au anapopata jeraha wakati wakucheza hushauriwa kutoa ishara ya kuomba kutolewa ili kujinusu kujijeruhi zaidi
Mara kwa mara tatizo wanalopata wachezaji hasa wale ambao wanatumika mara kwa mara katika mashindano tofauti tofauti huwa ni mvutiko mkali wa Misuli ya nyuma ya paja.
Kitabibu majeraha aina hii linajulikana kama overpulled muscle au Muscle strain. Ni aina ya majeraha ambayo mwanasoka hatakosa kuyapata katika maisha ya soka.
Ni hali inayoweza kumstua mtazamaji kumwona mchezaji anatoka akichechemea kidogo  lakini kwa jicho la kitabibu kumwona hivyo atembea mwenyewe kutoka nje ni ishara ya jeraha la kawaida ambayo ndio muscle strain.
Leo nitawapa ufahamu  jeraha la mvutiko mkali au kuvutika kwa msuli au kuchanika misuli ya paja ambalo ni tatizo la kawaida na huwapata sana wanasoka.

MAJERAHA YA NYAMA YA PAJA YALIVYO
Nyuma ya paja kuna misuli mikubwa mitatu inayoshirikiana kufanya kazi mbalimbali ikiwamo kurudisha paja nyuma na kupiga teke au kupiga mpira.
Misuli  inapotumika sana au kuzidiwa uwezo wake huweza kupata mchoko mkali na kuwa dhaifu.
Wakati wa kucheza nako kuna kuchezewa faulo ambazo mara nyingi husababisha majeraha madogo mpaka makubwa. Wachezaji wa soka wanakumbana na faulo nyingi hasa kwa viungo na washambuliaji.
Mambo yote haya huweza kuchangia kujijeruhi ndani kwa ndani kwa misuli na  nakurundika vijeraha vidogo vidogo na kuifanya misuli hii kuwa dhaifu.
Baadaye ghafla unapotumia nguvu kupita kiasi ikiwamo kutaka kuchomoka kasi misuli hii hupata shinikizo kubwa na huweza kusababisha kuchanika misuli hii.
Nyuzi nyuzi ndogo za misuli zilizo kama raba band huweza kukunjuka kupita kiwango chake hivyo kukatika.
Mchezaji anapokimbia kwa kasi mbio fupi kama vile za mita 100 misuli hii ndio inayoirudisha miguu nyuma huku akikanyagia na vidole gumba ili kuchochea kasi.
Wakati misuli hii ikifanya kazi hii hujikuta ikielemewa na uzito wote wa mwili, wakati huo huo huwa na kazi ya hujirefusha na kijifupisha ili kwenda kasi na hapo ndipo pia misuli hupata madhara.

MAMBO YANAYOMWEKA HATARINI
Mchezo wa soka na kupata majeraha ya misuli ya paja ni jambo ambalo ni gumu kulikwepa kwakuwa mchezo huu unatumia miguu kucheza.
Misuli iliyojibana iko katika hatari ya kupata tatizo hili, hii inawakumba wanamichezo wasiopasha kabla ya mazoezi au mechi.
Kama kundi la misuli litakuwa imara zaidi ya misuli pinzani (mfano misuli ya nyuma misuli inayopingana nayo huwa ni ya nyuma)  kutowina huku kunaweza kusababisha mchosho wa misuli, mara nyingi hutokea kwa misuli ya paja ya nyuma.
Misuli ya mbele ya paja huwa imara na nguvu zaidi, wakati wa  michezo inayohusisha kukimbia kasi misuli ya nyuma huchoshwa mapema na kutokuwa na nguvu kuliko misuli ya mbele. Mchoko huu huweza kuleta vijeraha katika misuli.
Kama misuli hii kiasili  itakuwa ni dhaifu basi nayo inakuwa haina uwezo wakuhimili mazoezi magumu hivyo inakuwa rahisi kujeruhi.
Uwepo wa Mchoko hupunguza uwezo wa misuli kupata nishati na kuwa na nguvu hivyo nayo hukuweka katika hatari ya majehi.
Wanamichezo ambao bado wanaendelea kukua kimwili wako katika hatari ya kuchanika kwa misuli kwani misuli yao na mifupa haikui katika uwiano sawa kwa muda na kasi.
Urukaji wa ghafla, kujinyoosha au mgongano wowote huweza kuivuta kupita kiwango chake na hivyo kuchana misuli iliyojipachika juu ya mfupi hiyo.
Dalili ya mara kwa mara ni pamoja na Mwanamichezo kujigundua kuwa na maumivu makali yanayochoma na kuuma nyuma ya paja hasa baada ya kuchoma kasi.
Hii itamfanya kusimama haraka na akiegemea mguu ulio mzima kiafya huku akishika nyuma ya paja baadaye maumivu yakizidi hukaa chini.
Ili kupunguza majeraha haya ya misuli ya paja ni vizuri wanasoka kuzingatia mazoezi mepesi ya viungo ikiwamo ya kunyoosha viungo vya mwili na kupasha moto mwili kabla na baada ya kushiriki michezo.
Vile vile wachezaji waepuke kucheza wakiwa wana mejaraha au kabla ya kupona vizuri. Tathmini ya kina ya kitabibu inahitajika kwa ajili wachezaji wanaopona baada ya kuwa majeruhi.
Benchi la ufundi linatakiwa kufanya kazi kwa kuzingatia weledi na ushauri wa wataalam wa mazoezi kwani sababu nyingine ya wachezaji kupata majeraha haya ni kufanyishwa mazoezi mazito kupita kiwango.
Majeraha aliyopata ni yakawaida ni ya mvutiko mkali wa misuli na ligamenti ambayo huchukua siku  2-5 kupona.

CHUKUA HII
Ili kuepukana na majeraha ya mvutiko mkali wa misuli ni vyema mchezaji akazingatia maelekezo ya wataala wa Tiba za michezo ikiwemo kufanya mazoezi lainishi ya viungo na ya kupasha mwili moto kabla ya kuingia au kuanza mazoezi mamakali.
Vile vile kufanya mazoezi ya viungo ya kupoza mwili mara baada ya mechi au mazoezi.