Prime
Simba ilete mashine hizi tu, isumbue zaidi msimu ujao

LIGI Kuu Bara imemalizika kwa Yanga kutetea ubingwa kwa mara nyingine tena ikiwa ni msimu wa nne mfululizo, huku watani wao wa jadi, Simba wakimaliza katika nafasi ya pili katika msimamo wa Ligi hiyo.
Yanga kuwa bingwa wala sio habari kubwa, kwa sababu hata kabla ya msimu kuanza wengi tuliamini wanaweza kuutetea bila shaka kwa kulinganisha timu waliyonayo na timu nyingine hasa wapinzani wao, Simba.
Habari kubwa ni Simba namna ilivyoweza kushindana na bingwa mtetezi hadi siku ya mwisho na kuangukia nafasi ya pili ambayo kwao ni mafanikio ukilinganisha na msimu uliopita wa 2023-2024 ambapo ilimaliza katika nafasi ya tatu nyuma ya Yanga na Azam.
Wakati Ligi inaanza, Azam ndio ilikuwa inaonekana mshindani mkubwa kwa Yanga kutokana na namna ilivyomaliza msimu wa 2023/24 na hata kufika kwao fainali ya Ngao ya Jamii na kuvaana na Yanga.
Pia ni kutokana na Simba kuamua kujenga kikosi chake kwa kuleta benchi jipya na asilimia kubwa ya wachezaji ambao wengi walikuwa vijana wadogo.

Kitu kizuri kwa Simba ni kwamba kwenye hatua za kutengeneza timu ya ushindani kuna vitu vingi chanya ambavyo vinatia matumaini ya kesho yao kama kutakuwa na utulivu kwenye tathmini ya msimu bila kuongozwa na hisia hasa kupoteza mechi dhidi ya Yanga ambayo ndio timu bora kwa sasa kwenye ligi yetu wanaweza kuangalia kikosi kilichopo na maboresho yanayohitajika.
Mfano kwa mchezaji mmoja mmoja wako waliojiinua na kuisaidia timu kufika fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika, nusu fainali ya Kombe la Shirikisho (FA) na nafasi ya pili ya Ligi Kuu. Moussa Camara langoni, Abdulrazack Hamza, Shomari Kapombe, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ katika eneo la ulinzi.
Katika eneo la kiungo kuna Yusuf Kagoma, Jean Charles Ahoua na Fabrice Ngoma, huku safu ya ushambuliaji ikiundwa na Kibu Denis, Ellie Mpanzu na Steven Mukwala wakijiinua kuliko wengi.
Sasa hapo Simba wanaweza kuwa na pa kuanzia hapo kwa kuwabakisha wachezaji hao kabla ya kufikiria wengine wapya wanaotoka nje ya timu hiyo, japo kutokana na uchache wa wachezaji wa daraja la hao niliowatumia kama mfano timu inahitaji kuongezewa rasilimali watu kwa kusajili wachezaji wenye daraja la juu kuliko walioko.

Langoni hakuna shaka wanahitajika makipa wa kumpa presha Camara, japo amekuwa mhimili kikosini kwa msimu huu ambao ni wa kwanza kwake, ila anahitajika kipa wa kuja kumuongezea njaa.
Kwa eneo la mabeki wa kati ni lazima apatikane kiongozi ambaye atakuja kutibu changamoto za msimu huu kukosa mbeba maono katika eneo hilo.

Hakuna ubishi kwa eneo la kiungo kulikuwa kunakosekana kiungo namba nane anayeweza kutumika katika nyakati kuu mbili za mchezo kwa maana kukaba na kushambulia kwa maana mwenye uwezo wa kutumia maboksi yote mawili la timu yake na la timu pinzani.
Kwa eneo hili la kiungo wanaweza kusajili viungo wawili mmoja anayeweza kucheza namba nane na namba sita mwingine anayeweza kucheza namba nane na namba kumi na kwa washambuliaji wa pembeni wanahitaji Mpanzu mwingine kuja kusaidiana na waliopo huku.

Kwa eneo la mshambuliaji kiongozi, kama ataongezewa nguvu kwa kusajili mshambuliaji atakayekuwa na uwezo wa kujitegemea hasa ukiangalia timu iko kwenye kujengwa.
Hivyo kuna wakati mshambuliaji atahitajika kujitegemea ili kupata nafasi ya kufunga kwa maingizo hayo huku wakiomba mbawa zao Kapombe na Tshabalala maumivu yawakalie mbali au watalazimika kuingia sokoni kusaka mabeki wengine wanaoweza kupandisha mashambulizi na kurudi kukaba.

Hayo yakifanyika timu ikiendelea kuwa na benchi lilelile ni wazi Simba ya msimu ujao inaweza kuwa tishio zaidi kuliko ilivyokuwa msimu huu ambao ilikuwa inajengwa, lakini ikaingia katika mafanikio makubwa kuliko hata msimu uliopita ilipomaliza nafasi ya tatu ikizidiwa hadi na Azam.