SPOTIDOKTA: Sababu za kuanguka na kufariki dunia ghafla

Muktasari:

  • Taarifa zinasema kwamba Maluu aliyekuwa akitokwa damu masikioni bada ya kuangukia uso na kushtua wanamuziki wenzake na mashabiki waliokuwa ukumbini akiburudika na kibao cha Hadija, alichokuwa akikiimba kisha kuwahishwa Hospitali ya Masana ilipobainika alishafariki na kutakiwa wapeleka mwili wake Hospitali ya Lugalo.

JANA Jumamosi kwenye ukumbi wa Target, uliopo Mbezi Beach jijini Dar es Salaam mwanamuziki mkongwe wa FM Academia, Maluu Stonch 'Nuhu' alianguka ghafla akiwa jukwaani akiimba kabla ya kukumbwa na mauti akiwahishwa hospitalini.

Taarifa zinasema kwamba Maluu aliyekuwa akitokwa damu masikioni bada ya kuangukia uso na kushtua wanamuziki wenzake na mashabiki waliokuwa ukumbini akiburudika na kibao cha Hadija, alichokuwa akikiimba kisha kuwahishwa Hospitali ya Masana ilipobainika alishafariki na kutakiwa wapeleka mwili wake Hospitali ya Lugalo.

Kifo cha mwanamuziki huyo wa zamani wa bendi ya Stono Musica, kimekuja siku chache baada ya kiungo wa zamani wa kimataifa wa Tanzania aliyetamba na timu za Simba na Nyota Nyekundu, Abbas Said Mhunzi 'Kuka' kuanguka msikitini wakati wa Swala ya Maagharibi na kuzikwa Magomeni jijini Dar.


Kadhalika kumekuwa na matukio yaliyoanza kuzoeleka kwa jamii na dunia kwa ujumla kwa wanamichezo na watu wengine kuanguka ghafla kabla ya kukumbwa na mauti na kuacha majonzi kwa famalia, ndugu, jamaa na rafiki wa wahusika.

Kibaya zaidi ni kwamba matukio hayo hutokea ghafla wakati mwingine wahusika waliofikwa na majanga hayo wakiwa na afya lete muda mchache kabla ya kukumbwa na jambo hilo na hapa chini ni sababu kinachochangia matatizo hayo na hatua za kuchukua mapema.

NINI TATIZO

Kupoteza fahamu inapotokea ghafla na aina ya uangukaji unaweza kuchangia kupata majeraha ya ubongo. Kuanguka na kichwa kutua katika sakafu ngumu kunaweza kuongeza ukubwa wa tatizo.

Eneo la kichwa ni eneo nyeti la mwili ambalo likapata jeraha kama lakupigwa na kitu kizito au kichwa kugonga sehemu ngumu inaweza kuambatana na majeraha mabaya ya ubongo ambayo yanaweza kusababisha kupoteza fahamu.

Binadamu kuzimia ghafla na kuanguka kunaweza kusababishwa na upungufu hewa yenye oksijeni katika ubongo, mfano katika magonjwa mfumo wa upumuaji na magonjwa ya moyo.

Upumuaji wakasi kutokana na uwepo wa tatizo lakiafya au kupata mshutuko wakisaikolojia na ushukaji mkali wa kiwango cha sukari katika damu vinaweza kumfanya mtu kuzimia na kuanguka.

Vile vile upungufu mkali wa maji mwilini, hofu au mstuko wa hisia, usumu katika mzunguko wa damu, dozi kubwa ya dawa za matibabu, kukosekana usawa wa tindikali, chumvi na madini katika damu. Ni kawaida pia sababu ya kuzimia ya moja kwa moja kutojulikana.

Ukiacha kuzimia ghafla, duniani matatizo ya mishipa ya mishipa ya damu ya moyo na magonjwa ya moyo ndio yanayoongoza kwakusababisha vifo vya ghafla ikiwamo kupata shambulizi la moyo

Shambulizi la moyo kitabibu Heart Attack ni moja ya matatizo ya kiafya yasiyoambukiza yanayosababisha mara kwa mara vifo vya ghafla kwa watu wazima wa miaka 45 kuendelea.

Ni kawaida ikatokea sababu ya kifo cha ghafla isijulikane moja kwa moja, lakini yapo matatizo ya kiafya yanayohusishwa na kifo cha ghafla ikiwamo vinavyotokea tukiwa usingizini.

Ukiacha matatizo ya moyo kwa ujumla, katika sehemu nyingine za mwili yaani ubongo na figo vinaweza kupata matatizo ya kiafya na kusababisha kifo cha ghafla.

Moyo ndio ogani kubwa inayohusika na usukumaji wa damu mwilini, magonjwa au matatizo yake huwa ni ya kimya kimya na ndiyo yanayoongoza kusababisha vifo vya ghafla duniani.

Maradhi ya moyo huwa yanapiga hatua kimya kimya pasipo kujijua kwa anayeugua, mara nyingi watu hugundulika wakiwa na matatizo ya moyo baada ya kufanyiwa uchunguzi wa jumla.

Mara nyingi kuharibika kwa mishipa ya damu katika moyo ni sababu kubwa inayosababisha matatizo mbalimbali ikiwamo mapigo ya moyo kwenda mrama, misuli ya moyo kufa na shambulizi la moyo.

Mishipa ya damu ya moyo ya Ateri ikiharibika husababisha misuli ya moyo kukosa damu kabisa au kupata kiasi kidogo sana. Uharibifu hutokana na mgando wa tando ya mafuta katika kuta za mishipa hii.

Hali hii husabisha misuli kushindwa kufanya kazi yakusukuma damu kwa ufanisi wakawaida, hupiga mapigo bila mpangilio na siku yoyote isiyojulikana ghafla moyo husimama.

Misuli ya moyo kututumka pia ni sababu mojawapo kwani husababisha vyumba vya moyo kuwa na nafasi ndogo yakupokea damu na pia kushindwa kusukuma vizuri damu.

Sababu nyingine ni pamoja na moyo kushindwa kufanya kazi, maumbile yasiyo yakawaida ya mishipa ya damu, hitilafu au uambukizi wa valve za moyo na kuzaliwa na moyo wenye hitilafu.

Vile vile uwepo wa matatizo ya mfumo wa umeme wa moyo, upungufu wa madini kama vile magnesium, kuzaliwa na moyo mkubwa, wingi wa mafuta mabaya mwilini na kuwa na hitilafu ya mapigo ya moyo.


Mambo mengine ambayo hayatokani na maradhi ya moyo ni kama vile sumu, mrundikano wa taka sumu, matatizo ya mfumo wa hewa, Kwame wa kitu njia ya hewa, kuvuta hewa chafu na ajali katika ogani.

Walio katika hatari ni wenye shinikizo la juu la damu, kiwango kikubwa cha lehemu, unene, kisukari, uvutaji tumbaku na kutofanya mazoezi, umri mkubwa 45+ na historia ya familia kupatwa na tatizo hili.

Inawezekana mtu ukawa na matatizo ya afya ya moyo lakini isijijue, ila pale inapotokea mstuko wowote ule ndipo unaweza kusababisha madhara.


USHAURI

Majukumu ya watoa burudani na wanamichezo yanatumia nguvu nyingi. Nikawaida kupata uchovu mkali, lakini pia kuna matatizo ya kiafya ambayo yanaweza kuwepo kimya kimya bila kuleta dalili.

Hivyo ni muhimu kujenga utamaduni wa kupima afya ya jumla angalau miezi sita mara moja. Vile vile vizuri kuwa na mienendo na mitindo bora ya kimaisha ili kujikinga na magonjwa yasiyombukiza.