SPOTIDOKTA: Huenda hiki kilimsumbua Victor Osimhen

Mshambuliaji wa timu ya Taifa  ya Nigeria, Victor Osimhen alilazimika kuachwa jijini Abidjan Jumanne kuelekea mchezo wa jana wa nusu fainali dhidi ya Afrika ya Kusini kutokana na kuumwa tumbo.

Taarifa ya kuwekwa kando siku hiyo zilitangazwa jumanne asubuhi wakati timu hiyo ikiwa kwenye maandalizi ya mchezo huo na ilisema mshambuliaji huyo wa Napoli alibakishwa na kuwa katika uangalizi wa madaktari wa timu katika Jiji la Abidjan.


Taarifa hiyo iliwekwa wazi katika akaunti rasmi ya timu hiyo kabla ya kwenda jijini Bouake kwa ajili ya mchezo huo wa jana na ilielezwa wachezaji wote wataondoka isipokuwa Osimhen ambaye hali yake ya kiafya haikuwa vizuri kutokana na kuumwa tumbo.

Taarifa hiyo ilithibitishwa na daktari wa timu hiyo, akieleza mshambuliaji huyo amezuiwa kusafiri kwa ndege na atabaki na timu ya madaktari ili kuangalia hali ya afya yake kwanza.

Taarifa hizo zilizua gumzo kubwa mitandaoni hasa mashabiki wa nchi hiyo wakiwa na hofu na mshambuliaji wao tegemeo na hatari kwa wapinzani.

Hata hivyo, baadaye msemaji wa timu hiyo, Babafemi Raji alieleza mchezaji huyo bora wa mwaka Afrika aliungana na wenzake kwenda Bouake baada ya kupona tatizo hilo.


Kwa jicho la kitabibu, tatizo lililompata Osimhen ni kawaida kuwapata wageni wanaofika nchi ngeni, hasa wanaotegemea vyakula vya migahawa na hoteli.

Inawezekana Osimhen alikunywa maji au kula chakula ambacho si kizuri au chenye vimelea au uchafu, tatizo ambalo kitabibu linajulikana kama Food Poison.

Mchezaji huyu ambaye anavaa kifaa maalum usoni sio kama ni pambo bali ni kutokana na majeraha aliyoyapata na leo katika kona ya Spotidokta tutaona tatizo la tumbo na sababu ya kuvaa kifaa hicho usoni.


Tatizo la tumbo liko hivi

Kitabibu hujulikana pia kama foodborne illness na hutokana na uvamizi wa vimelea au shambulizi katika mfumo wa usagaji chakula unaoweza kuenea kwa kunywa maji au chukula.

Vimelea kama bakteria, virusi na parasaiti ndio vinara wanaosababisha usumu katika vyakula. Vile vile zipo baadhi yakemikali zinaweza kushikamana na vyakula au maji na kusababisha hali hiyo.

Ni tatizo linalowapata sana wasafiri wageni wanaotoka mazingira yao na kwenda mazingira mapya. Marekani pekee tatizo hili linawapata watu milioni 48 kila mwaka.

Dalili zake huwa ni maumivu makali ya tumbo, kuharisha, kutapika, kupata homa na kutetemeka. Tatizo hili huwa linaweza kuwa la wastani tu au likawa kali zaidi na kusababisha muathirika kulazwa hospitali.


Habari nzuri kuhusu tatizo hili, linatibika na mgonjwa akitibiwa kwa usahihi anapata nafuu haraka na kuendelea na majukumu yake.

Uamuzi wa kumzuia kwa muda na kuwa chini ya madaktari jijini Bouake ulikuwa ni uamuzi mzuri kwani inasaidia kutazama mwenendo wa tatizo kama linaongezeka au linapungua.

Tatizo hili linaweza kudhibitiwa na mwili wenyewe bila dawa yoyote na likaisha, kama ni matibabu dawa za matibabu na maji maalum ya ORS au dripu kwa wale waliotapika na kuharisha na kupoteza maji hutumika.

Tatizo kubwa na tishio ni endapo mgonjwa ataharisha na kutapika sana hatimaye kupata upungufu wa maji mwilini na kama hatua zisipochukuliwa mgonjwa anaweza kupoteza maisha.

Ni tatizo ambalo linampata mtu ghafla na huwa halidumu muda mrefu ukilinganisha na matatizo mengine ya tumbo. Kawaida huwa halizidi zaidi ya wiki.

Ni dhahiri Osimhen alipata tatizo la wastani na halikuwa kubwa ndio maana alijiunga na timu kuendelea na majukumu yake kama mshambuliaji kinara wa Super Eargle.


Sababu ya kuvaakifaa tiba usoni

Unaweza ukadhani amevaa kinyago usoni kama pambo. Hiki ni kifaa tiba maalum na alitakiwa kukivaa baada ya kupata majeraha mabaya ya kichwa eneo la usoni mwaka 2021.

Alilazimika kufanyiwa upasuaji wa uso baada ya kugongana na beki wa Inter Milan, Skriniari katika mchezo wa Ligi Kuu ya Italia, Serie A, Oktoba 2021 na baada ya kupona alishauriwa aendelee kukitumia ili kumkinga asipate jeraha eneo hilo.

Nyota huyu aliyeipa Napoli ubingwa wa Seria A msimu wa 2022/23, amekuwa akikivaa kifaa hicho (Face Msk) kwenye michezo yote ya ligi na timu ya taifa ikiwamo kwenye fainali hizo za Afcon 2023 na kimempa mwonekano wa kipekee na kujulikana haraka.

Licha ya kifaa hiki kutumika kama tiba, kimegeuka kuwa dili la kibiashara kwa mashabiki wa Napoli kununua na kampuni iliyokitengeneza kutoa mfanano wake na kuuza kwa mashabiki hao ambao wamempachika jina Osimhen ‘Masked-striker’ baada ya kuisadia timu hiyo kuweka historia iliyowahi kuwekwa na Maradona kwa kutwaa ubingwa wa ligi.