SPOTIDOKTA: Hatari ya dawa hizi kwa wanamichezo

KIUNGO wa Juventus ya Italia, Paul Pogba ameingia katika tuhuma za kutumia dawa za kusisimua misuli ambazo zilipigwa marufuku michezoni.
Katika taarifa iliyotolewa Jumatatu wiki hii ni kwamba, Pogba alichukuliwa vipimo vya awali ambavyo vilionyesha kuwa na kiwango kikubwa cha Testosterone.
Kinachosubiriwa sasa ni matokeo ya awamu ya pili ambavyo ni vipimo vya kina vitakavyothibitisha kuwa ametumia dawa hizo.
Endapo atabainika kuwa alitumia dawa hizo huenda akafungiwa kucheza kwa miaka minne.
Mara baada ya kufungiwa na Tume ya Taifa ya Kupambana na Kuzuia Matumizi ya Dawa za Kusisimua Misuli michezoni, msemaji wa Pogba, Rafaela Pimenta alieleza vyombo vya habari kuwa “hakuwahi kutaka kuvunja kanuni hizo.”
Alisema kuwa, “tunasubiri matokeo ya uchunguzi yakinifu, ila kwa sasa hakuna la kusema zaidi.”
Itakukumbukwa kuwa Pogba alikuwa ni majeruhi kwa muda mrefu mchezo aliocheza Agosti 20, 2023 dhidi ya Udinese ulikuwa ndio mchezo wake wa kwanza.
Majibu kuonekana ni chanya (positive) katika kipimo cha uchunguzi wa awali kama anatumia dawa za kusisimua misuli ambazo zimeharamishwa kutumika kwa wanamichezo ni pigo.
Dawa za kusisimua misuli zenye uasili wa ‘steroid’ ambazo mara kwa mara zimekuwa zikibainika kutumiwa na wanamichezo ni pamoja na Norandrosterone na Creatine.
Dawa zingine zenye majina ya kibiashara ambazo zipo mitandaoni kimagendo ni pamoja na Estoforce Edge, Muscle Ex Edge na Muscle Rip Edge.
Ipo jamii nyingine ya steriods zilizopigwa marufuku ziitwazo Steroid Precursors ambazo ni Adrostenedione (andro) na Dehydroepiandrosterone (DHEA) ambazo pia huongeza ukubwa na nguvu ya misuli.
Dawa hizi huwa zinaifanya misuli kuwa na nguvu kupita kiasi, huku pia zikiwa zinafanya kazi bila kuchoka kwa muda mrefu. Dawa hizo zimeainishwa kitaalamu kuwa zina uasili sawa kikemikali na kichochezi cha kiume cha Testosterones.
Kama ilivyo kwa dawa zingine zenye uasili wa kichochezi cha Steroids huwa na faida ya tiba ya kuondoa uvimbe na maumivu ya mwili, hutumika kurekebisha kudhoofika kwa mwili kunakosababishwa na magonjwa sugu kama vile Ukimwi.
Inaelezwa kuwa iwe ni kutumia dawa hizo kwa bahati mbaya au makusudi ni lazima sheria ichukue mkondo wake.
Dawa hizo husimamiwa uchunguzi wake na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Matumizi ya Dawa za Kusisimua Misuli Michezoni (Wada).
NAMNA WANAVYOGUNDUA
Kwa kawaida katika ligi kubwa huwapo na kamati maalumu ambayo kazi yake ni kupambana na watumiaji wa dawa za kuongeza nguvu au kusisimua misuli ili kuweza kuwa na nguvu zaidi.
Dawa hizo zimeharamishwa kutumiwa na wanamichezo, wataalamu wa tume hiyo huwa na kawaida ya kupima kwa kushtukiza wachezaji. Pale wanapoona au kuhisi huwastukiza na kuchukua sampuli ya mkojo papo kwa papo na kwenda maabara kuupima.
Huwa ni makosa pia kuwakwepa wataalamu hao. Mtakumbuka mchezaji wa soka beki wa kati wa Klabu ya Manchester United, Rio Ferdinand aliwahi kukumbwa na masahibu hayo pale alipowakwepa wataalamu hao, lakini hakuweza kukwepa adhabu ya kufungiwa.
KWANINI HAJA NDOGO?
Kwa kawaida binadamu anapotumia dawa yoyote huingia mwilini katika mzunguko wa damu na kuvunjwa vunjwa na hapo baadaye inapomaliza kufanya kazi yake huwapo na mabaki taka mwilini.
Dawa nyingi mabaki yake yaliyopo katika damu hufika katika figo yakiwa na damu. Kazi ya figo huwa ni kuchuja kwa kuondoa vitu visivyotakiwa mwilini.
Mabaki ya dawa hizo pamoja na taka sumu nyingine za mwilini ikiwamo Urea na Creatinine hutolewa pamoja na mkojo.
Na mara nyingine kama mchezaji ametumia dawa hizo unaweza kumbaini pale tu anapotoka kucheza soka kwani zikishapita saa zaidi ya 24 inakuwa vigumu kwani mabaki hayo yanaweza kuwa tayari yamekwisha mwilini kwa njia ya kukojoa.
Katika upimaji huo wa kustukiza hufuatiwa na hatua B ambayo inahusisha sampuli za mkojo na damu, wataalamu hao huingia kwa kina kuchunguza sampuli hizo.
CHANGAMOTO YA VIPIMO
Moja ya changamoto ya vipimo hivyo ni pale wanapohitaji sampuli ya mkojo kwa mchezaji ambaye ametoka kucheza kwani unapocheza maji mengi mwilini hupotea kwa njia ya jasho.
Hivyo mara nyingi wanawakuta wachezaji wakiwa hawana hamu ya kwenda haja ndogo kwani maji mengi yamepotea kwa njia ya jasho.
Lakini, kitaalamu haikubaliki ni lazima katika kibofu kutakuwepo na kiasi cha mkojo hivyo ni lazima wapate sampuli ya mkojo.
Ndio maana unapokwepa hilo unakumbana na adhabu ya kufungiwa pia.
Sababu za kupigwa marufuku ni zipi?
Ni ukweli usiopingika kuwa dawa hizileti ushindani wa haki, kama wengine wanatumia na anacheza na wengine wasiotumia hazihalalishi ushindi au mafanikio halali ndio maana wanaziita dawa haramu.
Madhara makubwa ya kiafya ya dawa hizi ikiwamo athari katika moyo na damu ni sababu mojawapo ya kupigwa marufuku kutumika michezoni.
Steroids zilizopigwa marufuku na viambata vyake zina madhara makubwa kiafya na ya muda mrefu katika mwili. Kadiri mtu unavyotumia kwa wingi ndivyo madhara yanavyozidi kuongezeka.
Baadhi ya athari za dawa hizi zinaweza kudhibitiwa lakini nyingine zikiisha tokea ni vigumu kudhibiti.
Wanamichezo vijana wadogo walio katika umri wa balehe wakitumia dawa hizi wanapata tatizo la kutoongezeka urefu, kokwa au korodani kunyauka na kuota matiti.
Vile vile athari kama hii inapojitokezaa huambatana na uharibifu wa maumbile ya kiume, ukosefu wa nguvu za kiume na ugumba.
Kuota matiti kwa mwanamichezo wa kiume huambatana na matatizo ya kisaikolojia kama vile kukosa kujiamini, kujichukia, kujitenga, kuwa na msongo wa mawazo na kupata sonona (depression).
Vilevile kuota nywele katika uso na kupata chunusi nzito usoni. Kwa wanamichezo wakike madhara wanayopata ni kuwa na sauti nzito, kukomaa na kukamaa misuli kama mwanaume.
Madhara mengine kiujumla ni maumivu sugu ya maungio na kupata majeraha kirahisi ya nyuzi ngumu za miishilio ya misuli inayojipachika katika mfupa (tendon) na kuwa na kinga dhaifu.
Vile vile hupata matatizo ya ugandishaji damu pale unapopata jeraha, shinikizo la juu la damu, matatizo katika ini, figo kushindwa kufanya kazi, vifo vya ghafla, hasira zilizopitiliza na kuhisi uzito mwilini unaokufanya kuwa mvivu.
CHUKUA HII
Usitumie dawa yoyote bila kuandikiwa au kushauriwa na daktari, vile vile epuka dawa za kusisimua misuli au kuongeza ukubwa wa misuli au zakupunguza unene kwani nazo pia ni dawa zilizoharamishwa kutumiwa na wanamichezo.