SPOTI DOKTA: Siri mabondia kuruka kamba

SPOTI DOKTA: Siri mabondia kuruka kamba

KWA wanamichezo ni kawaida kufanya mazoezi ya aina tofauti kwa lengo la kutengeneza utimamu wa miili kuwawezesha kutimiza majukumu kwa ufasaha. Kipaji cha kucheza bila mazoezi ni sawa na kufuli bila ufunguo. Vitu hivi vinategemeana ili kumfanya mwanamichezo kuwa mshindani.

Moja ya zoezi ambalo mabondia wengi duniani hulipenda ni kuruka kamba. Hulifanya kwa mtindo wa kuizungusha wakitumia mikono na kupita chini ya miguu na kichwani. Zoezi hili ni aina ya mazoezi mepesi yanayojulikana kama aerobics exercise na mara nyingi ukitazama mabondia hapa nchini na wa kimataifa utawaona wakilifanya.

Siri ya mabondia kupenda zoezi hili ni kutokana na faida lukuki zinazotokana na kulifanya zinazomfa mhusika kuruka mizunguko mingi kwa saa nyingi. Kutokana na mchezo wa ndondi kuhitaji wepesi na pumzi imara kuweza kustahimili kudumu pambano muda mrefu pasipo kuchoka ndiyo maana mabondia hupenda kufanya. Matokeo makubwa ya utimamu wa miili wanayopata mabondia ndiyo siri inayowafanya kulifanya kama sehemu ya mazoezi mepesi.

Habari nzuri ni kuwa halina gharama hata kwa mabondia au wanamichezo wengine wenye kipato cha chini kumudu kununua kamba. Zoezi hili ni moja ya mazoezi ambayo kipindi cha corona ilipokuwa juu kiasi cha watu kujifungia ndani lilikuwa likitumiwa na wanamichezo kulinda utimamu wa miili.

Ubora wa utimamu wa miili wa mabondia kama Mayweather Jr na Tyson Fury umechangiwa na kufanya zoezi hili mara kwa mara pamoja na kushikamana na mafunzo mengine. Hata mabondia nchini ambao wako katika viwango vizuri ikiwamo Hassan Mwakinyo na Twaha Kiduku pia ukifuatilia mazoezi utakuta zoezi la kuruka kamba wanalifanya mara kwa mara.


FAIDA ZAKE

Kuruka kamba ni njia ya kuupa mwili mazoezi mepesi ambayo ndiyo yanatupa utimamu wa miili na kuwa na afya njema. Zoezi hili ni rahisi linafahamika na idadi kubwa ya watu ambao wamewahi kupita shule za awali, linakuepusha kwenda kufanya mazoezi ya pamoja na halihitaji eneo kubwa.

Ingawa linaweza kuwa changamoto kwa wazee ambao tayari umri umesonga pamoja na wale ambao wana unene uliopitiliza, zoezi hili linawafaa sana wanamichezo vijana ambao wanahitaji kukabiliana na uzito mkubwa au unene.

Kuruka kamba ni moja ya zoezi la ambalo linaweza kutumika na kukupa faida nyingi kiafya ikiwamo kuufanya mwili kuepukana na unene uliokithiri. Faida kubwa ya zoezi hili ni kuchoma kiasi kikubwa cha mafuta mwilini kwa kuwa sehemu kubwa ya mwili hufanya kazi ikiwamo maeneo yenye mrundikano wa mafuta kama tumbo, makalio, mapaja, mikono, shingo na mashavu.

Hii ndiyo sababu wanasayansi wa mazoezi ya mwili wanalipendekeza kama ni moja ya zoezi linalopunguza uzito wa mwili kwa urahisi na vilevile kupunguza hatari ya unene. Zoezi hili ni rahisi lisilo na gharama kubwa kwani bei ya kamba kwa machinga huanzia Sh3,000-10,000 na ni rahisi kuibeba.

Zoezi hili ni vizuri kulifanya mwenyewe ukiwa ndani kwako kwa dakika 20-30 kwa siku katika siku tano za wiki. Kama ilivyo kwa mazoezi mengine humfanya mfanyaji kuhisi burudani huku akiwa na hisia ya furaha na hii ni kutokana na kuchochea kuzalishwa kwa ‘endorphins’ zinazoleta hisia chanya.

Tafiti za wanasayansi wa mazoezi zimebaini zoezi hili linapofanyika kwa dakika kumi ni sawa na dakika thelathini za kukimbia, hivyo mwili huchapa kazi zaidi kuliko kuogelea na kukimbia. Dakika 15-20 zinaweza kukata mzigo wa mafuta ambao ni sawa na kupoteza kalori 200-300 ambazo hii ni sawa na kutembea kilomita saba au saa nzima.

Hapa inatupa picha zaidi ya kwanini mabondia wanakuwa na mwonekano wa miili mikakamavu isiyo na mrundikano wa mafuta na hii ni kutokana na zoezi hili kuchoma mafuta mengi mwilini. Kabla ya kuanza zoezi ni vizuri kupasha mwili moto kwa mazoezi ya kunyoosha viungo ili kuandaa misuli na viungo vingine, kuwa na wepesi wa kufanya zoezi pasipo kujipa vijeraha vya ndani.

Pia hakikisha kuwa kamba unaitunza vizuri na kipindi hiki cha corona itumie wewe mwenyewe na ikitokea imetumiwa na mtu mwingine hakikisha unaitakasa kwanza. Faida hizi ndizo siri kubwa zinazowafanya mabondia na wanamichezo wengine kupenda kufanya zoezi hili mara kwa mara katika programu za mazoezi. Ni vizuri wanamichezo wakatumia zoezi hili kutengeneza utimamu wao wa miili ili kupata mafanikio makubwa ya michezo wanayoshiriki.