SPOTI DOKTA: Simba vs Yanga, haya yanaweza kutokea DABI Mkapa

Muktasari:

  • Kama unavyofahamu mchezo huu unachezwa kwa mbinu nyingi za uwanjani na nje ya uwanja, kelele za mashabiki mitandaoni na uwanjani vinasababisha kuwapo kwa hamasa kubwa mchezoni.

Kesho ikiwa ni Sikukuu ya Nane Nane, pia kuna mpambano makali wa watani wa jadi, Simba na Yanga katika mchezo wa nusu fainali ya Ngao ya Jamii utakaochezwa kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam saa 1:00 usiku ukitanguliwa na nusu fainali nyingine kati ya Coastal Union na Azam FC itakayopigwa kule Zanzibar kwenye Uwanja wa New Amaan Complex kuanzia saa 10:00 jioni.

Kama unavyofahamu mchezo huu unachezwa kwa mbinu nyingi za uwanjani na nje ya uwanja, kelele za mashabiki mitandaoni na uwanjani vinasababisha kuwapo kwa hamasa kubwa mchezoni.

Mchezo huu unazikutanisha timu hizi ambazo wikiendi iliyopita zilikuwa zikiadhimisha siku zao ambazo zilitumika kutambulisha nyota wapya.

Katika mchezo huu wa leo jioni kuna mambo mbalimbali ambayo jicho la kitabibu linamulika kuwa huenda yakajitokeza kwa upande wa mashabiki na upande wa wachezaji.

Hivyo kwa wachezaji na mashabiki watapaswa kujipanga ili kuchukua tahadhari za kujikinga dhidi ya matatizo hayo ya kiafya ambayo si tishio kubwa kuwafanya wasiende kutazama.


YANAWEZA KUTOKA KWA MASHABIKI

Suala la mashabiki kuanguka na kupoteza fahamu huwa ni jambo la kawaida katika mchezo huu wa watani wa jadi. Kuzimia ni moja ya matukio ambayo yanatokea mara kwa mara katika mechi hizi.

Kutokana na mchezo huu kubeba hisia za mashabiki kuna mambo mengi ambayo yanaweza kuwapa mshtuko na kupoteza fahamu au kuzimia.

Ukiacha suala la hisia, hali ya hewa inatarajiwa kuwa na joto hivyo kuwaweka mashabiki katika hatari ya kupoteza maji mengi mwilini. Hii ikitokea ni moja ya sababu za kupoteza fahamu.

Uwapo katika msongamano mkubwa ambao katika mechi hizi za watani wa jadi huwa ni kawaida, unamweka shabiki katika hatari ya kukosa hewa hivyo kuwa katika hatari ya kujisikia kuchoka na kuzimia.

Kwa watu ambao wana umri mkubwa ni kawaida kujisikia uchovu au kuchoka kutokana na uwapo wa shinikizo la mwili linalotokana na kutumia muda mwingi kusimama na huku wakiwa katika jua kali muda mrefu.

Mashabiki huwa na tabia ya kuwahi kufika mapema zaidi ili kuwahi kuingia au kuwahi na kukaa maeneo ya jirani. Baadhi wanaowahi hukaa nje muda mrefu na kupata kinywaji kama vile pombe.

Hii inawaweka katika hatari ya kulewa mapema kutokana na mwili kukabiliwa na hali ngumu ya unywaji katika mazingira ambayo yanaupa mwili mchoko mkali kirahisi.


KWA WACHEZAJI

Ikumbukwe kuwa wachezaji wa timu zote mbili wana kiu kubwa ya kushinda mchezo huo, hivyo ni kawaida kutumia nguvu, kucheza kwa kasi na kucheza au kuchezewa faulo.

Kutokana na kukamiana huko haitashangaza kuona mchezaji akipata majeraha ya mapema na kutolewa. Hii ni kwasababu mchezo wa soka unahusisha kukumbana kimwili.

Mara nyingi katika dakika 15 za mwanzo ndio huwa shinikizo kubwa kutokana na maelekezo ya benchi huwa ni kutumia dakika hizo kupata ushindi wa mapema.

Washambuliaji, mawinga na viungo ndio huwa na kawaida ya kuanza mchezo kwa kasi ili kutafuta bao la mapema.

Hawa ndio huwa na kawaida kupata majeraha ya mapema ikiwamo kubanwa misuli.

Utakumbuka katika mchezo wa Aprili 20 mwaka huu, Yanga ilimpoteza beki wake wa kushoto, Joyce Lomalisa mwanzoni mwa mchezo na dakika 3 baadaye Simba nayo ilipata pigo baada ta beki wake wa kati Henock Inonga kuumia na nafasi ya kuchukuliwa na Hussein kazi.

Majeraha haya yalikuwa ya mapema sana kwa wachezaji hawa ambao walianza kucheza kikosi cha kwanza. Huwa ni kawaida kwa mechi kama hizi wachezaji kuwa na hamasa ya juu hatimaye kukamia mchezo.

Mchezo wa soka kama huu wenye upinzani mkali wachezaji wanatumia nguvu nyingi na kasi kubwa. Hata katika kukabana huko nako ni mapambano na hatimaye kukwatuliwa na kupata majeraha.

Kupata majeraha ya mapema kunaweza kuwa ni ishara ya wachezaji hawa kutumika sana mara kwa mara kutokana na umuhimu wao katika kuisaidia timu kupata mafanikio.

Mchezo wa soka huwa una mambo mengi uwanjani ikiwamo kutumia nguvu sana kucheza hivyo ni kawaida wachezaji kama hawa kupata mrundikano wa vijijeraha vya ndani kwa ndani.

Kitendo cha kutumika sana na nafasi wanazocheza ni kawaida kukumbana na majeraha ya aina ile kwani mabeki nao huweza kupanda na kushambulia.

Soka ni mchezo ambao unahusisha kukabana kimwili, pamoja na mbinu mbalimbali zinatumika kupunguza majeraha lakini ni kawaida kutokea majeraha.

Ili kuepuka majeraha ya mapema wachezaji wanahitajika kupasha mwili moto kwa mazoezi mepesi na mazoezi ya viungo kabla ya kuingia katika mechi.

Mchezaji anaweza kupata majeraha yatokanayo na mchezo katika eneo la miguu yanaweza kutokea kutokana na kukimbia kasi, kugongwa, kujipinda vibaya hasa maeneo ya maungio kama goti na kifundo na kutua vibaya wakati wa kuruka.

Inawezekana kupata majeraha ya maungio na misuli inapofanya kazi ikiwamo kukakamaa, kupata mkazo, kuchanika au kuvutika kupita kiasi.

Katika mchezo huu unakuwa na hamasa kubwa kwa wachezaji ni kawaida pia kwa mchezaji pinzani kutumia nguvu kubwa kumkaba mwingine hatimaye kuweza kumjeruhi.

Mchezaji kucheza akiwa bado hajapona vizuri, hii inaweza kuwa moja ya sababu kwani kama jeraha halijapona vizuri ni rahisi kupata majeraha tena kwani eneo hili linakuwa sio timamu.

Wakati wa kucheza mchezaji mwenyewe anaweza kutumia nguvu sana wakati wa kucheza au kukaba, hii inaweza kuchangia kujijeruhi mwenyewe pasipo kuchezewa faulo ikiwamo kujipinda uelekeo hasi.

Kutokana na mchezo wenyewe kuwa na upinzani mkali, ni kawaida kufanyiwa faulo mbaya na kupata majeraha.

Mwanasoka anapokuwa anategemewa katika timu anaweza kuamua kudanganya kuwa hana maumivu ya mwili na kucheza au akalazimishwa kucheza akiwa ametumia dawa za maumivu.

Mchezaji anaweza kushawishika au kudanganya ili tu apangwe kucheza katika kikosi cha kwanza jambo ambalo humpatia bonasi ikiwamo ile anayopewa endapo atafunga au kuibuka na ushindi.

Huwa ni kawaida majeraha kutokea katika mechi hii bila sababu ya msingi hii ni kutokana na miili ya wachezaji kushindwa kustahimili kucheza kama mechi itakuwa ngumu.

Ikumbukwe kuwa wachezaji wanaocheza mchezo wa leo wametoka pia kucheza mechi katika kuadhimisha sikukuu za timu hizo. Ni kawaida kukumbana na hali ya uchovu hatimaye kucheza chini ya kiwango.

Mchezaji mwenye upungufu wa maji mwili yuko katika hatari ya kupata tatizo la kubanwa msuli.

Mchezaji asiyepata muda wa kutosha wa kupumzika na kulala kwa muda wa saa 8 kwa usiku mmoja leo anaweza kucheza chini ya kiwango kutokana na mwili kuharibiwa utimamu wake.


USHAURI

Ili kuepukana na matatizo ya kiafya yanayoweza kujitokeza, mashabiki wanatakiwa kunywa maji ya kutosha, kulala na kupumzika kabla, kutumia vikinga jua na kuvaa nguo rafiki kwa joto kali.