Winga Pamba anaukubali mziki wa Chama

Muktasari:
- Winga huyo raia wa Uganda anaitumikia Pamba Jiji ya Mwanza ambayo alijiunga nayo Julai 7, 2024 akitokea Tabora United aliyodumu nayo kwa misimu miwili tangu mwaka 2022 ikiwa Ligi ya Championship.
BAADA ya kiungo wa zamani wa Simba, Thadeo Lwanga ‘Injinia’ aliyekuwa msomi wa chuo kikuu akiwa amehitimu Uhandisi wa Programu kutoka Chuo cha Makerere, winga John Nakibinge ni mchezaji mwingine msomi kutoka nchini Uganda anayekiwasha kwenye Ligi Kuu Bara.
Winga huyo raia wa Uganda anaitumikia Pamba Jiji ya Mwanza ambayo alijiunga nayo Julai 7, 2024 akitokea Tabora United aliyodumu nayo kwa misimu miwili tangu mwaka 2022 ikiwa Ligi ya Championship.
Nakibinge ambaye ni msomi wa Shahada ya Teknolojia ya Mawasiliano (IT) kutoka chuo kikuu cha Martyrs nchini Uganda, ni miongoni mwa mawinga wa kigeni wenye ufundi mwingi akisifika kwa kufunga mabao makali ya ‘kideoni’.
Kati ya mabao ya kukumbukwa msimu huu kutoka kwa nyota huyo ni lile la Septemba 21, 2024 alilolifunga dhidi ya Mashujaa FC dakika ya 39 akipiga ‘outer’ kutokea ya nje ya 18, katika mchezo huo uliomalizika kwa sare ya 2-2 kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza.
Pia, alifunga bao nje ya 18 kwa shuti kali dhidi ya Coastal Union Februari 15, 2025 katika mchezo wa Ligi Kuu uliochezwa kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza, huku Pamba Jiji ikishinda mabao 2-0.
Nakibinge anasema mazoea ya kufunga mabao kama hayo yanatokana na ubora wa ziada aliojaliwa na Mwenyezi Mungu.
“Nafikiri ni kujiamini, pia kama mchezaji unakuwa na ubora fulani wa ziada naamini nina ubora fulani, pia naweza kusema ni baraka za Mungu,” anasema.
Anasema soka lake la kulipwa na la ushindani limeanzia Tanzania kwani hakuwahi kucheza soka la ngazi ya juu nchini kwao Uganda zaidi ya kucheza mtaani, chuo kikuu na timu ya NEC FC iliyokuwa madaraja ya chini.

CHUO KIKUU NA SOKA
Akizungumzia safari yake ya soka anasema haikuwa rahisi kwani wazazi wake waliweka msisitizo zaidi kwenye masomo, hivyo ikabidi asome hadi chuo kikuu ambako ndiko soka lake lilikopata mwanga na kuonekana.
“Mungu ndiyo anajua kwa sababu baada ya kumaliza kidato cha sita nilikuwa nacheza mtaani tu kuna kocha mmoja alikuwa anafundisha chuo kikuu ndiyo akaniona akaja akaongea na mimi akasema anaweza kunipeleka chuo kikuu,” anasema Nakibinge.
Anaongeza kwamba; “Baada ya kuwaambia wazazi wangu naweza kwenda chuo kikuu nikasoma na nikawa nacheza mpira walifurahia na wakaniruhusu. Nilisoma Bachelor of Science and Information Technology (Shahada ya Sayansi ya Mawasiliano) katika Chuo cha Martyrs, Uganda.”
Winga huyo anasema ujio wake Tanzania ndio ulikuwa mwanzo wa safari ya kucheza soka la ushindani na kumfungulia milango ya kuonekana.
“Kwa kweli competition football (soka la ushindani) sijaianza wakati niko mdogo nimetumia muda mwingi kwenye masomo, wazazi wangu walikuwa wameniweka shule, nimekuja kuingia rasmi kwenye ushindani nikiwa chuo kikuu,” anasema Nakibinge.
Anaongeza; “Nilikuwa nacheza NEC FC wakati anasoma chuo kikuu mwaka 2020 nilipomaliza masomo ndiyo nikapata dili la kuja Tanzania kujiunga na Kitayose (sasa Tabora United) na sasa niko hapa Pamba Jiji.”

LIGI YA BONGO
Baada ya kukaa na kucheza soka kwa misimu mitatu nchini Tanzania, Nakibinge ameukubali mziki na kusema limepiga hatua na linaendelea kuvutia mastaa wengi kutoka mataifa mbalimbali.
“Kwa kweli mpira wa Tanzania kila mwaka unakua hata ukiangalia zile klabu ambazo zinawakilisha Tanzania kwenye mashindano ya kimataifa unaona zinafanya vizuri,” anasema Nakibinge.
Anaongeza kuwa; “Hata ukiangalia ubora wa wachezaji wa kigeni ambao wako kwenye ligi unaona ligi ni bora kweli kweli, naona kila mwaka mpira unaongezeka kukua.”
OKWI, MUKWALA WAMPA HASIRA
Mastaa kutoka nchini Uganda walikuja wakafanya vizuri na kuacha alama kwenye Ligi Kuu Bara akiwamo Emmanuel Okwi (Simba na Yanga), Khalid Aucho (Yanga), Thadeo Lwanga (Simba) na sasa Steven Mukwala (Simba).
“Mimi mwenyewe natamani kufikia kiwango walichoonyesha wachezaji wenzangu nina malengo makubwa nataka nicheze Ligi ya Mabingwa Afrika,” anasema Nakibinge na kuongeza;
“Nataka nicheze klabu kubwa siyo Tanzania tu hata Afrika mimi mwenyewe nawaangalia kama kielelezo kwangu wananishawishi ninatamani kuwa kama wao au zaidi.”
Nakibinge anasema kilichofanywa na kinachoendelea kuonyeshwa na wachezaji hao ni alama kwa wachezaji wengi chipukizi nchini Uganda ambao wanatamani kufikia ngazi ya juu.
“Okwi, Aucho na hata Mukwala ukimuona sasa hivi jinsi anavyofanya pale Simba kweli wanakushawishi na wewe uendelee kupambana uone kwamba inawezekana kufika pale,” anasema winga huyo.

CHAMA NI BALAA
Winga huyo amemwagia sifa kiungo mshambuliaji wa Zambia ambaye amepata sifa kubwa nchini baada ya kuonyesha uwezo mkubwa akiwa na Simba na sasa Yanga, Nakibinge anaamini nyota huyo ana uwezo mkubwa wa akili ya kusoma mchezo.
“Kwa hapa Tanzania kwenye ligi mimi nampenda Chama (Clatous) anajua sana mpira jamaa ana akili sana yule, mimi napenda sana mchezaji anayetumia akili lazima uusome mchezo,” anasema Nakibinge.
Anaongeza nje ya Tanzania anamkubali winga wa zamani wa Manchester United raia wa Ureno, Luis Nani ambaye alikuwa anamtazama wakati anakua.
“Nilikuwa nampenda sana Luis Nani kipindi nilikuwa mtoto ndiyo maana hata sasa hivi navaa jezi namba 17, alikuwa anafanya sana mambo mazuri ambayo nilikuwa natamani sana na mimi niyafanye.”
UGANDA CRANES
Licha ya kucheza soka la ushindani nje ya nchi yake, Nakibinge bado hajabahatika kuitwa katika timu ya taifa ya Uganda (The Cranes), jambo ambalo bado halijamkatisha tamaa kwani anaamini siku moja ndoto hiyo itatimia.
“Nafikiri ni ndoto ya mchezaji yeyote yule kuiwakilisha nchi yake kwenye mashindano makubwa, mimi mwenyewe natamani, napambana siku moja niitwe timu ya taifa,” anasema.

KIDOLE CHAMTIBULIA
Anasema kati ya changamoto zilizomsumbua ni kupata majeraha ya kidole gumba ambacho kilimuweka nje ya uwanja kwa miezi minne na kurudisha nyuma kiwango chake na kukosa uhakika wa namba kikosini.
“Msimu huu sijacheza sana nilipata majeraha nikakaa miezi minne bila kucheza niliporudi nimekuwa na ingia toka kikosini sikuwa na muendelezo mzuri ila mambo yanakuwa mazuri,” anasema.