SPOTI DOKTA: Osimhen chupuchupu afie uwanjani

KINDA wa soka kutoka nchini Nigeria anayekipiga katika klabu ya soka ya Napoli ya nchini Italia Victor Osimhen ameeleza kwa kina ajali ya mchezoni aliyoipata 21 Novemba 2021 chupuchupu imsababishie kifo.
Alikutana na ajali hiyo ya kugongana kimwili na Milan Skriniar katika mechi ya Ligi ya Serie A waliyopoteza 2-3 dhidi ya Inter Milan kwenye Uwanja wa Giuseppe Meazza.
Alisema ilikuwa chupuchupu kufariki kutokana na mivunjiko mingi ya mifupa ya uso iliyohusisha zaidi ya mmoja ambayo ni sehemu ya fuvu la kichwa.
Osimhen mwenye wa miaka 22 alieleza kuwa ajali hiyo wote wakiwa katika kasi alishtukia uso wake ukibamiza katika mwili wa Skriniar hatimaye alidondoka chini akiwa katika hali ya kuona wenge.
Ni kweli alifanikiwa kupata huduma ya kwanza pale uwanjani na aliweza kutoka mwenyewe nje ya uwanja pasipo msaada wa kutolewa na machela na watoa huduma ya kwanza.
Uwanjani hapo alidhaniwa kuwa pengine haikuwa ajali kubwa pengine angekuwa nje ya uwanja kwa muda mfupi lakini kumbe haikuwa jeraha dogo kwani lilimweka nje kwa muda wa miezi miwili.
Mara baada ya kufika hospitalini na kuchunguzwa, matokeo ya picha za mionzi yaliwafanya madaktari kushangaa kwani alikuwa na mivunjiko katika mfupa wa shavu la kushoto unaojulikana pia kama taya na eneo la juu la mfupa unaotengeneza pango la jicho.
Daktari nguli wa upasuaji wa mifupa na misuli ya kichwa anayejulikana kama Gianpaolo Tartaro ndiye aliyeongoza timu ya upasuaji huo uliofanikiwa lakini ulikuwa mgumu.
Dokta Gianpaolo anaeleza kuwa walishangazwa na ujasiri wa Osimhen wa kuweza kusimama mwenyewe huku akiwa na mivunjiko hiyo na kutoka nje ya uwanja pasipo msaada wa machela za watoa huduma.
Anasema hatua hiyo ilikuwa ya hatari kwani alikuwa na mivunjiko mibaya eneo la uso ambalo ni sehemu ya fuvu la kichwa inayolinda ubongo.
Kupata ajali katika maeneo hayo yangeliweza kujeruhi ubongo jambo ambalo lingelikuwa hatari zaidi ikiwamo kusababisha kifo.
Kwa mujibu wa daktari upasuaji wa kukarabati mivunjiko hiyo ya mifupa wa ya uso ilipelekea kutumia vifaa tiba aina ya vibaya chuma 6 na skrubu 18 ili kuunga vipande vya mifupa hiyo.
Ni upasuaji mgumu lakini ulikuwa na lengo la kuikarabati na kuiweka mifupa hiyo katika mkao wa asili wa kimwili kama awali. Wapasuaji wa mifupa hii na misuli ya kichwa ndio wanaitwa maxillofacial surgeons.
Wapasuaji hawa maalum ndio wamebobea katika eneo hilo, bila wao pengine angeliweza kupata ulemavu wa kudumu eneo la mbele ya kichwa.
Kwa upande wa jicho la kitabibu leo linatazama na kuwapa ufahamu wa boriti hizi au vishikizo ambazo hujulikana kama screw na vijisahani vya chuma hujulikana kama metal plates.
Vifaa Tiba hivi ndivyo vinavyowekwa ili kuiunganisha mifupa iweze kutulia sehemu na kuunga kirahisi kwa wakati.
Usiyojua kuhusu vifaa tiba vya kushikiza mifupa
Vifaa tiba vya kushikiza vipo vya aina mbalimbali ikiwamo vijisahani vyuma, boriti au skurubu, pini na vijipande bapa.
Vitu hivi vyote ni vifaa tiba ambavyo vinatumika katika upasuaji wa mifupa iliyovunjika. Lengo ni kuwezesha mifupa hiyo kuunganika huku ikitulia mahali pamoja.
Vifaa tiba hivyo ni kama kinga inayozuia eneo hili kutoachiana hata pale unapotokea mtikisiko kutoka nje ya mwili au pale mjeruhiwa anapoutembeza mwili wake.
Mifupa ambayo imevunjika na kupishana pande mbili au kutawanyika vijipande pande huwa inahitajika kuunganishwa kitaalam na madaktari wa tiba wa mifupa.
Vifaa hivi ni aina ya vipandikizi ambavyo vinaweza kuwekwa mwilini kwa muda au kwa kudumu. Vipo ambavyo vimetengenezwa kwa chuma, dongo ngumu au plastiki.
Ni kweli vinapandikizwa mwilini lakini ni kawaida pia kutokea kinga ya mwili ikakataa kukubaliana navyo hivyo kinga kujibu mapigo kwa kutiririsha askari mwili.
Kwa kawaida mifupa ambayo inavunjika ndani ya mwili huweza kujikarabati na kurudi katika hali yake kama hapo awali lakini njia kama hizi zinasaidia kuweza kuunga kwa usahihi na kwa wakati.
Ni kawaida pia katika mazuri yoyote ya kitiba kutokea madhara machache wakati wa uwekaji wa vifaa hivi katika mifupa ambayo imevunjika.
Moja ya madhara hayo ni pamoja na kupata uambukizi endapo vifaa hivyo vilishikamana na vimelea, kutokaa vyema katika mfupa hatimaye kutofanya kazi yake, kujeruhi tishu jirani, kuvuja damu nyingi, kinga ya mwili kukataana na vyuma hivyo.
Vile vile uwekaji na utoaji wa vifaa tiba hivyo huweza pia kumletea maumivu mgonjwa kwakuwa ni lazima ufanye upasuaji.
Vipandikizi hivi vinavyowekwa kwa muda ni kawaida kuhitajika kutolewa baada ya wiki 6-8 ingawa itategemeana na eneo la mvunjiko wa mfupa.
Habari nzuri kwa Osimhen upasuaji huo aliofanyiwa haukumletea madhari yoyote, zaidi ilikuwa ni maumivu ambayo yalidhibitiwa kwa dawa za maumivu.
Mafanikio ambayo yalipatikana katika upasuaji huo ndio yaliwezesha kufanikiwa kuunga vyema kwa mifupa hiyo kwa wakati hatimaye kuwa nje ya uwanja kwa miezi miwili.
Alirudi uwanjani tarehe 17 Januari 2022 akiingia katika dakika ya 71 katika mchezo wa ligi dhidi ya Bologna.
Hadi sasa amewekewa kifaa maalum anachovaa kwa nje kichwani wakati anacheza ambacho kinatoa msaada katika misuli na mifupa ya eneo la taya na mbele ya uso.
Ushauri, vizuri kila ajali ya uwanjani ikapewa kipaumbele katika uchunguzi na matibabu kwani si kila ajali ya uwanjani ni ndogo.