SPOTI DOKTA: Nyota wa EPL na tukio la kupatwa mshtuko wa moyo

Mchezo wa Ligi Kuu ya England (EPL) kati ya AFC Bournemouth na Luton Town Jumamosi iliyopita ulilazimika kuahirishwa mara baada ya nahodha wa Luton, Tom Lockyer kuanguka ghafla uwanjani akiwa anacheza mechi hiyo.

Mwanasoka huyo mwenye umri wa miaka 29 alikutana na hali hiyo dakika ya 59 kipindi cha pili akiwa ameudhibiti mpira akiwa pembeni mwa straika wa Bournemouth, Dominic Solanke.

Alilazimika kupatiwa huduma ya kwanza ya dharura ijulikanayo kitabibu kama Cardiopulmonary Resuscitation-CPR na madaktari wa pande zote mbili na watoa huduma ya kwanza kabla ya kutolewa na kuwahishwa katika hospitali ya rufaa.

Habari nzuri ni kuwa mara baada ya kuishiwa nguvu na kuanguka na mpaka anatolewa uwanjani kwa machela alikuwa ana fahamu hali ambayo ilikuwa ni kiashiria kizuri kitabibu.

Baadaye klabu hiyo ilitoa maelezo katika mtandao wake wa X kuwa mchezaji huyo alipatwa na tatizo la mstuko wa moyo au moyo kusimama ghafla kitabibu hujulikana kama Cardiac Arrest.

Mtakumbuka makala ya wiki iliyopita ilieleza tukio kama hili lililotokea kwa shabiki katika Ligi Kuu la Hispania (LaLiga) kati ya Granada na Athletic Club na kulazimika mchezo huo kuahirishwa mara baada ya kutaarifiwa shabiki huyo amefariki dunia.

Kwa Tom imekuwa ni bahati nzuri kwani aliweza kupata huduma akiwa uwanjani na baadaye ziliendelea katika ndani ya vyumba vya uwanjani kabla ya baadaye kuhamishiwa katika hospitali ya rufaa.

Taarifa ilitolewa na hospitali hiyo kuwa yuko imara kiafya na hali yake inaendelea vizuri ila yuko katika uchunguzi zaidi na uangalizi maalum akiwa ni siku yake ya 6 akiwa karibu na familia yake.

Mtakumbuka wiki iliyopita nilieleza tatizo la moyo kusimama ghafla au mstuko wa moyo vitu vinavyomweka mtu kupata tatizo hili mojawapo ni kuwahi kuugua magonjwa ya moyo.

Kwa mujibu wa kituo cha televisheni cha michezo ESPN, mwezi Mei mwaka 2022 mchezaji huyo alilazwa siku tano kwa ajili ya kutibiwa tatizo la moyo lijulikanalo kama Atrial Fibrillation.

Ambayo ni hali ya mapigo ya moyo yasiyo ya kawaida katika chemba za moyo za juu zijulikanazo kama Atrial, hali inayozaa mitetemo ya mapigo yasiyo na mpangilio hatimaye kuathiri utendaji kazi wa moyo.

Jicho la kitabibu siku ya leo linalitazama tukio hili katika upande wa huduma ya kwanza kama moja ya huduma muhimu hasa katika matukio ya mkusanyiko wa watu kama ilivyo katika viwanja vya soka.


UMUHIMU WA HUDUMA

YA KWANZA

Huduma ya kwanza ni moja ya nyenzo muhimu katika huduma za afya kwani ndio huokoa wagonjwa wenye matatizo ya dharura kupoteza maisha au kuzuia wasipate ulemavu wa kudumu.

Tatizo la moyo kusimama ghafla ni moja ya matatizo ya moyo ambayo kama hatua sahihi zisipochukuliwa katika huduma ya kwanza kifo cha mapema huweza kutokea.

Hii ni kwasababu moyo ndio kiungo nyeti mwilini ambacho kazi yake ni kusuma damu kwenda katika maeneo muhimu ikiwamo ubongo ambao ukikosa tu damu yenye oksjeni ndani ya dakika 5 kifo hutokea.

Uwepo wa huduma za kwanza uwanjani ni muhimu sana sio tu kwa ajili ya kukabiliana na matukio ya majeraha ya michezo bali pia kwa matatizo yoyote ya kiafya ya dharura kama la moyo kusimama ghafla.

Tatizo hili linaweza kukabiliwa vyema na kuwa na matokeo chanya endapo timu ya huduma ya kwanza na madaktari wa timu iliyopo uwanjani ina ujuzi na vifaa kukabiliana na matukio ya dharura.

Ujuzi huo ni pamoja na huduma ya usingaji wa moyo kwa tatizo la moyo kusimama ghafla ambayo ndio inayosaidia moyo kudunda na kupumua.

Ukiacha ujuzi huo ambao unatakiwa hata asiye mtoa huduma za afya angalau anatakiwa kuwa na elimu ya msingi ya kufanya usingaji wa moyo kwani ni matatizo ambayo bila huduma hiyo kifo hutokea.

Ukiacha ujuzi, lazima kuwepo na vifaa vya kisasa kwa ajili ya kutolea huduma ya dharura na mfumo kamili wa rufaa unaowezesha mgonjwa kufika kwa wakati katika huduma za afya za juu.

Ukiacha vifaa vingine, vifaa ambavyo ni muhimu kuwepo kwa watoa huduma ya kwanza ya kisasa viwajani ni pamoja na begi maalum la lenye vifaa kwa ajili ya huduma za usingaji wa moyo-CPR.

Begi hili huwa na puto la oskjeni, mashine ya kustua moyo AED, mashine ya mkono ya kufyonza ute ute au maji maji, barakoa ya kupitishia hewa, kituliza ulimi na pamoja na dawa za dharura.

Huduma za usingaji wa moyo huweza kufanywa kwa mikono na watoa huduma za afya kwa kuweka mikono kifuani mwa mgonjwa na kusaidia mapigo.

Habari nzuri ni kuwa hivi sasa kuna mashine ya kisasa ya kufanya usingaji ambayo ni rahisi kuibeba, kuitumia na inafanya kazi kwa ufanisi ukilinganisha na mikono.

Kwa aliyetazama tukio lile ni dhahiri kuwa suala la huduma za afya kwenye Uwanja wa Vitality zilikuwa timamu kwani Tom alipata huduma ya kwanza na kufikishwa kwa wakati katika hospitali kubwa.

Huduma walizotoa ndio zimechangia kuokoa maisha ya Tom ambaye alipata tatizo linaloweza kusababisha kifo cha mapema


KUAHIRISHWA

KWA MECHI

Tukio la kuangua ghafla na kupoteza fahamu ni matukio ambayo yanagusa hisia za watazamaji na wachezaji waliopo uwanjani, hali ambayo inasababisha kutokuwa sawa kiakili kumaliza mchezo.

Hali hiyo ya kupatwa na mstuko wa kiakili kutokana na tatizo hilo la dharura la kitabibu ni vigumu sana kwa timu zote na mashabiki waliokuwa wakiburudika na mchezo huo kustahimili.

Wasingeliweza kuendelea na mchezo huo kwani kila kitu na nguvu yote vilielekezwa kukabiliana na tukio hilo ambalo hakuna aliyekuwa anajua kama aliyeanguka amefariki au yuko hai.

Mashabiki hawakuwa nyuma kutoa faraja kwani walikuwa wakiimba jina la Tom la kumtakia kheri. Lakini taarifa njema zilikuja kwamba yuko salama.