Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

SPOTI DOKTA: Hivi ndivyo ilivyo saratani iliyomuua Eriksson

Muktasari:

  • Kocha huyo aliyekuwa raia wa kwanza wa kigeni kuifundisha England alifikwa na mauti juzi, Jumatatu, asubuhi nyumbani kwake akiwa amezungukwa na familia yake.

KOCHA wa zamani wa timu ya Taifa ta England, toka nchini Sweden Sven-Goran Eriksson amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 76 baada ya kuugua saratani ya kongosho kwa muda mrefu.

Kocha huyo aliyekuwa raia wa kwanza wa kigeni kuifundisha England alifikwa na mauti juzi, Jumatatu, asubuhi nyumbani kwake akiwa amezungukwa na familia yake.

Taarifa ya kifo chake ilithibitishwa na wakala wa kocha huyo wa zamani wa Lazio nchini Sweden anayejulikana kwa jina la Gustavsson.

Januari mwaka huu aligundulika kuugua saratani ya kongosho ambayo ilikuwa katika hatua za mbali, jambo ambalo lilisababisha kuacha majukumu yake na kupigania afya yake.


Itakumbukwa kazi yake ya mwisho alikuwa ni mkurugenzi wa michezo wa Karlstad ambayo ndiyo timu ya eneo analotoka  nchini Sweden.

Kitu kikubwa kilichoondoa uhai wa Eriksson au kuchangia kifo chake ni madhara makubwa ya saratani inapokuwa katika hatua za juu ambayo huwa ni hatua ya tatu au nne.

Kongosho kwa kitabibu hujulikana kama Pancreatic, ni moja ya ogani za ndani ya mwili ambayo ni kiwanda cha kuzalisha vimeng’enya vya kusaga chakula na kichochezi cha insulini ambacho ndicho kinachodhibiti sukari ya mwili.

Tatizo la saratani ya kongosho huwa ni mara chache kuweza kubainika katika hatua za awali na hii ni kwa sababu hainyeshi dalili zozote kwenye hatua hiyo.

Mara kwa mara dalili na viashiria huweza kujitokeza pale saratani inapokuwa katika hatua za juu. Itakumbukwa kuwa saratani inaweza kutibika ikiwa katika hatua za awali.

Inapokuwa imepiga hatua za juu huwa na dalili kama vile kuumwa tumbo. Maumivu hayo yanaweza kuenea au kusambaa eneo la mgongo, kukosa hamu ya kula na uzito wa mwili kupungua.

Vilevile mabadiliko ya ngozi na tando nyeupe ya macho kuwa manjano, kupata haja kubwa tepetepe na yenye rangi ya kufifia, mkojo wenye rangu ya kahawia au nyeusi, kuwashwa, uchovu na kukosa nguvu.

Inapotokea mtu ana saratani hiyo mwili wake unakosa uwezo wa kudhibiti sukari kwa sababu ogani iliyoathiriwa na saratani ndiyo inayozalisha kichochezi kinachodhibiti sukari.

Madhara ya saratani ambayo hujitokeza ikiwa imeanza kuvamia maeneo mengine ya mwili ni pamoja na upungufu wa damu, kinga ya mwili kuwa chini, kukosa nguvu na kukonda.

Saratani inapovamia ogani nyingine za mwili huathiri utendaji wa ogani hizo na hatimaye kuleta dalili mbalimbali ikiwamo kukosa nguvu pamoja na uchovu na maumivu.


INASABABISHWA NA NINI?

Mpaka sasa haieleweki kwa kina kisabaishi cha saratani ya kongosho. Wataalamu wamebaini vitu vinavyoweza kuchangia kujitokeza ikiwamo matumizi ya tumbaku na kuzaliwa katika familia yenye historia ya kuugua saratani ya kongosho.

Vihatarishi vingine ni pamoja na shambulizi sugu au uambukizi wa mara kwa mara katika kongosho, unene uliokithiri, umri mkubwa wa miaka 65+ na unywaji pombe kupitiliza

Saratani hiyo inatokea mara baada ya seli za kongosho chembe za urithi (vinasaba) yaani DNA kubadilika. Itakumbukwa kuwa DNA ndiyo imebeba maelekezo yanayoielekeza seli kitu gani cha kufanya katika majukumu mbalimbali ya mwili. Kwa seli zenye afya zinaelekezwa kukua na kuongezeka kwa usahihi na kufa katika muda uliopangwa.


Wakati katika seli zenye saratani zenyewe hupata maelekezo tofauti hatimaye kukua na kugawanyika ili kuongezeka kiholela. Seli hizo hizo zinaweza kukua haraka pasipo mpangilio.

Seli hizo zinaweza kuzaliana, kukua na kutengeneza uvimbe ambao huweza kuathiri tishu au ogani zingine za mwili ambazo zina afya njema.

Pale zinapopiga hatua zaidi huweza kuvamia katika maeneo mbalimbali ya mwili na hatimaye kuleta madhara mbalimbali ambayo nimeyataja katika dalili.


JE INATIBIKA?

Saratani hiyo inaweza kutibiwa katika hatua za awali kwa njia ya upasuaji na dawa. Katika hatua za mbali ambazo ni ngumu kutibika mgonjwa hupewa matibabu ya kufifisha dalili mbaya ikiwamo dawa za maumivu, lishe maalumu na kuongezewa damu.

Vilevile mgonjwa hupewa ushauri nasaha wa namna ya kuishi na tatizo hilo endapo lipo katika hatua za mbali.


NAMNA YA KUJIKINGA

Ili kupunguza hatari ya kupata saratani ni kuwa na mwenendo na mitindo bora ya kimaisha ikiwamo kuepuka matumizi ya tumbaku na bidhaa zake pamoja na kufanya mazoezi ili kudhibiti uzito wa mwili.

Vilevile punguza matumizi ya nyama nyekundu na kula zaidi vyakula vya asili hasa mbogamboga na matunda. Epuka vyakula vya kusindika na unywaji pombe kupita kiasi.

Kinga ni bora kuliko tiba, saratani haichagui masikini wala tajiri. Ishi katika mienendo na mitindo bora kimaisha na jenga tabia ya kupima afya ya jumla angalau kwa mwaka mara moja.


CHUKUA HII

Pamoja na umaarufu mkubwa na kuwa na pesa nyingi kwa Eriksson anatarajiwa kuzikwa katika eneo la siri na watu wachache katika familia yake.