SPOTI DOKTA: De Bryune kama vile hakuwa majeruhi

KIUNGO wa Manchester City, Kevin De Bruyne ‘KDB’ amerudi kutoka kwenhye majeraha akiwa na makali yake kama awali kabla ya kuwa nje kwa miezi mitano baada ya kuumia misuli ya paja Agosti mwaka janma. Makali yake  yalionekana Jumamosi katika mechi ya Ligi Kuu EPL baada ya  kuisaidia timu yake kupata ushindi wa mabao 3-2 dhidi ya Newcastle katika Uwanja wa St James Park.

Katika mchezo huo Man City ilimiliki mpira kwa asilimia 73% huku KDB aliyeingia kipindi cha pili alionyesha kiwango bora kwa kucheza dakika 21, kufunga bao moja na kusaidia lingine pia alipiga mashuti mawili langoni.

KDB alifunga bao la kuisawizishia timu yake iliyokuwa nyuma kwa bao 2-1 dakika ya 74 . Baadaye aliweza kutoa krosi ndefu ya mita 30 ambayo ilizaa goli la ushindi dakika ya 90+1 dakika za majeruhi.

Katika dakika chache alizocheza aliweza kudhihirisha kuwa amerudi na makali yake kama vile hakuwa majeruhi ambayo yalimweka nje kwa muda wa miezi 5.

Huu ilikuwa ni mchezo wake wa pili tangu apone majeraha hayo ambayo aliyapata mwanzoni mwa msimu Agosti 2023, hivyo kumlazimu kuwa nje.

Alianza kuujaribu utimamu wake wa mwili katika mchezo wa Kombe la FA dhidi ya Huddersfield Town Jumapili wiki iliyopita kwa kuingizwa dakika za mwisho katika mchezo walioshinda mabao 5-1.

Katika mchezo dhidi ya Newcastle aliibeba timu yake iliyokuwa nyuma 2-1 hivyo kudhihirisha utimamu wake na kiwango chake.

Katika mchezo huo alicheza kwa tahadhari akitumia muda mwingi kujitenga na kuomba mipira na kutoa zaidi pasi kuliko kushambulia akikwepa kukumbana kimwili.

Kwa namna alivyoonyesha kiwango chake kwa dakika chache kinatoa picha kama vile hakuwa majeruhi kwa muda mrefu. Ni kawaida kwa mchezaji aliyekuwa majeruhi kucheza chini ya kiwango.

Katika mchezo wa kwanza kuanza alicheza dakika zisizozidi dakika 30 ili kuujaribu mwili wake mara baada ya mechi hiyo alieleza kwa kwa sasa anaweza kuanza na kucheza dakika 90.

Awali ilisemwa angeweza kucheza dakika 20-25 akiwa katika utayari wa juu lakini si kwa dakika 90, hii ni kutokana na majeraha aliyoyapata yalikuwa makubwa lazima arudi kucheza kwa tahadhari.

Jicho la kitabibu linamtazama kiungo huyo mwenye umri wa miaka 32 ambaye ni mmoja kati ya wachezaji bora kabisa kama moja ya mfano mzuri kwa mchezaji aliyetoka majeruhi akichezeshwa kwa tahadhari.

Mtakumbuka katika mchezo wa ufunguzi wa Ligi Kuu dhidi ya Burnley alipata majeraha haya mabaya ya kuchanika misuli ya paja yajulikanayo kitabibu kama Amstring Injury.

Majeraha hayo ndio yalimfanya kuwa nje ya uwanja na kukosa mechi 18 za msimu huu. Lakini utaratibu uliomwandaa na kumfanya kurudi uwanjani ndio sahihi kwa mchezaji ambaye ndiye ametoka kupona majeraha.


ALIANDALIWA KURUDI MCHEZONI KAMA HIVI

Jeraha alilopata lilikuwa kubwa. Misuli ya paja inahusisha kuchanika nyama za paja daraja la tatu ambalo linahitaji uangalizi wa kitabibu wa kiwango cha juu.

Kuna matibabu yanayoweza kutibiwa katika ngazi ya klabu lakini kwa jeraha alilopata ilikuwa ni lazima kupata matabibu ya kibingwa katika hospitali ya juu kwa madaktari maalumu.

Katika vituo hivyo vya juu mchezaji huchunguzwa kwa kina na kupata matibabu na huku akiendelea kuwa chini ya uangalizi na kuhudhuria kliniki maalumu ya matibabu na ufuatiliaji.

Anapopona hupewa programu nzima ya uuguzi wa jeraha na anatakiwa kuizingatia na huku akishikamana na miiko yote na masharti yote yakitabibu.

Anapopona kabisa ndipo huamishiwa kwa wataalamu wa mazoezi tiba ya viungo ambao huwa na programu yao ya mazoezi ya uponyaji ili kulainisha, kunyoosha na kuimarisha misuli iliyopata majeraha.

Baada ya kufanya majaribio yao na kuona kama amepona timu wataalamu hushirikiana na wale walimu wa timu katika kumtathimini kama anaweza kuanza mazoezi ya awali.

Ikiwamo kuchezeshwa mazoezi ya peke yake, baadaye huchezeshwa kwa tahadhari timu B ili kuona kama hana shida yoyote hapo ndio huanza mazoezi ya pamoja na kikosi cha kwanza.

Kwa mchezaji kama KDB jeraha alilopata ni kubwa na limemuweka nje miezi mitano lazima umpange kwa tahadhari ili asije akapata jeraha lingine mapema.

Ndio maana walilifahamu hilo akaingizwa katika mchezo wake wa kwanza na wapili  kipindi cha pili akacheza kwa dakika zisizozidi 25 kitu ambacho ni sahihi.

Kocha Pep Guardiola ameleza kwa uwazi wanalitambua vyema kuwa jeraha alilopata lilikuwa kubwa hivyo wanamtumia kwa tahadhari ili jeraha  lisijirudie.

Moja ya hatua wanayoichukua ni kumwanzishia mazoezi ya pamoja kwa wiki kadha kwa kumjumuisha katika vipindi visivyozidi vitano hadi sita vya mazoezi. Na pia wanazingatia ushauri wa wataalamu wa viungo.

Guardiola alisema hawawezi kumpa dakika 80 au 90 kutokana na aina ya jeraha alilopata. Bado anahitaji wiki na dakika zaidi za mazoezi ili kuwa timamu.

Kutokana na umri wake ni rahisi kupata majeraha ya mara kwa mara kama ushauri wa madaktari hayatazingatiwa.


HATARI YA KUPATA MAGONJWA YA AKILI

Mchezaji mwenye majeraha si tu anapata athari katika mwili, bali pia kiakili. Hivyo matibabu ni lazima yawe ya pande mbili ili kumwezesha kuwa timamu. Matatizo ya akili yanayoweza kumkabili ni pamoja na hofu, mfadhaiko, msongo wa mawazo na sonona (depression).

Hivyo, madaktari wanapokabiliana na majeraha ya michezo kwa upande mwingine humpa pia ushauri tiba ili kumwepusha na matatizo ya afya ya akili. 

Tatizo la kiakili linaweza pia kuepukwa endapo mchezaji anapata faraja kutoka kwa klabu na mashabiki. KDB alipata hamasa kubwa pale aliposhangiliwa wakati anaingia katika mchezo wa kwanza. Hii inamfanya mchezaji kujiamini na kucheza kwa ari na hamasa ya hali ya juu.  KDB ameonekana kama vile hakuwa majeraha  alivyoupiga mwingi katika mechi mbili alizocheza.