Prime
Siri iliyomo kwenye vibegi wanavyobeba wachezaji

Muktasari:
- Kuanzia kwenye mazoezi hadi katika siku za mechi, mastaa wa soka kubeba vibegi sio ishu tu ya mitindo na fasheni, bali vina umuhimu mkubwa kwa ajili ya mahitaji yao muhimu.
LONDON, ENGLAND: HIVI ushawahi kujiuliza kuhusu vibegi wanavyobeba wanasoka huwa ndani kunakuwa na nini?
Unatamani kujua? Tulia hivyo hivyo.
Kuanzia kwenye mazoezi hadi katika siku za mechi, mastaa wa soka kubeba vibegi sio ishu tu ya mitindo na fasheni, bali vina umuhimu mkubwa kwa ajili ya mahitaji yao muhimu.

Lakini, swali linaloulizwa mara nyingi, kwenye hivyo vibegi kumewekwa nini na vingi kiasi gani?
1. Ndani ya vibegi vidogo vya mastaa
Mara nyingi umekuwa ukiwashuhudia wanasoka, hasa kwenye zile mechi zinazoonyeshwa moja kwa moja kupitia televisheni, kipindi wanaposhuka kwenye mabasi ya timu zao, wanakuwa wamebeba vibegi vidogo. Unaweza kujiuliza kwenye vibegi hivyo vidogo kuna kitu gani cha maana kimewekwa na kubebwa?

Wanasoka wanabeba sana vibegi vidogo wanapokwenda au kutoka kwenye mechi. Lakini, cha kujiuliza, wameweka nini?
Kwa kawaida, jezi, soksi, viatu vya kuchezea, kitambaa cha unahodha na vitu vingine muhimu kwa ajili ya mambo ya ndani ya uwanja huwa vinawekwa kwenye vyumba vya kubadilishia, pamoja na vifaa vingine kama slipa na taulo.

Hivyo, mchezaji anachotakiwa ni kubeba vitu vyake binafsi kwenye vyuma vya kubadilishia. Na vitu hivyo, ndivyo vinavyowekwa kwenye vile vibegi vidogo, ambavyo watahitaji kuvitumia kabla ya baada ya mechi. Mfano wa vitu vinavyowekwa kwenye vibegi vidogo ni sabuni, shampuu, mafuta na wengine wamekuwa wakibeba mashine za kunyoa nywele.
2. Nini kinabebwa kwenye begi kubwa?
Katika nyakati nyingine, wanasoka wamekuwa wakipendelea kubeba mabegi ya mgongoni au mabegi makubwa. Hiyo ina wasaidia kubeba vitu vingi zaidi wanavyovihitaji, kama vile nguo za kubadilisha baada ya mechi, jozi za viatu, kompyuta mpakato au vifaa vingine kama vile chupa za chai, huku pia wakibeba viatu vya kuchezea kwenye hali ya hewa tofauti ili inapohitajika isiwe shida.

3. Jinsi wanasoka wanavyopanga vitu kwenye mabegi
Kwanza wanaandaa vifaa vyao vya mazoezi na mechi usiku mmoja kabla ya mechi au saa moja kabla ya kwenda kwenye mechi.
Kama mechi inachezwa kwenye mazingira ya baridi, basi lazima nguo za joto, tracksuit, viatu, shin guard na soksi. Baada ya kuandaliwa, kazi ya kuanza kuvipanga kwenye begi inaanza.

-Kwanza nguo zinakunjwa vizuri na kupangwa kwenye begi. Kisha viatu vinawekwa kwenye eneo lake, huku ikizingatia vitu vikavu vinakaa upande tofauti na vitu vya maji. Vifaa vya mazoezi na mechi haviruhusiwi kuchanganyika na nguo binafsi. Hata baada ya kufanya mazoezi, viatu na jezi zilizotumika, bila shaka zitakuwa zimeloa, hivyo vinapaswa kupangwa kivyake.

Kitu kingine kinachobebwa kwenye begi hasa lile kubwa la mchezaji ni maji au juisi ya matunda kwa ajili ya kuupa mwili nguvu kabla na baada ya mazoezi au mechi.