SIO ZENGWE: Super League inakuwaje nzuri Afrika, mbaya Ulaya

MWAKA 1998, kampuni ya habari nchini Italia, Media Partners, ilifika ofisi za makao makuu ya Chama cha Soka cha Ulaya (Uefa) kuonana na rais wa wakati huo, Lennart Johasson. Viongozi wa kampuni hiyo, hawakuwa na lolote jingine, bali pendekezo la kuanzishwa kwa ligi mpya ya Ulaya.

Wakati huo, Ulaya yote ilikuwa imeelekeza macho jijini Milan ambako Real Madrid walikuwa wakipambana na Atletico Madrid katika fainali ya Ligi ya Mabingwa. Uefa haikukubaliana na wazo hilo, lakini pengine ilijifunza mengi katika pendekezo hilo, ambalo kama lilivyoibuka mwaka huu, lingehusisha klabu 14 kubwa barani Ulaya wakati huo.

Wazo hilo liliibuka tena mwaka huu na klabu kubwa kama Real Madrid, Barcelona, Atletico Madrid, Manchester United, Arsenal, Liverpool, Juventus na Milan zilishakubaliana na mpango huo, ambao ungeziwezesha kupata tiketi ya kushiriki michuano hiyo bila ya kupambania nafasi ndani ya nchi zao, huku timu nyingine zingefanya kazi nzito ya kufuzu kwa nafasi chache ambazo zingesalia.

Vyama vya soka vya nchi, serikali na mashabiki wa nchi tofauti walipinga vikali mpango huo, huku Uefa ikitishia kuzichukulia hatua kali klabu ambazo zingeshiriki. Wazo hilo limekufa, ingawa Real Madrid bado inaeleza kuwa mpango huo unaendelea na huenda Super League ikawepo mwakani.

Wapinzani wa wazo hilo walisema kitendo cha baadhi ya timu kufuzu moja kwa moja bila ya kupambania nafasi kinaondoa asili ya michezo ya kushindana ili kupata kitu fulani.

Pia wengine waliona ingechosha kwa klabu kubwa kukutana kila mara kwenye ligi moja.

Mashabiki walisema matajiri waliokubaliana na mpango huo walikuwa wabinafsi na walifikiria fedha zaidi badala ya mashabiki na hivyo kuandamana na hata kusababisha mchezo wa Manchester United kuahirishwa. Wengine, hasa wa klabu zinazoonekana kuwa ndogo, waliona uwezekano tena kwa timu zao kukutana na klabu kama Barcelona, Real Madrid, Manchester United na Juventus, ungekuwa mdogo kutokana na muundo wa ligi hiyo.

Shirikisho la Kimataifa la Soka (Fifa) lilitishia kuwazuia wachezaji wote ambao wangeshiriki ligi hiyo kucheza fainali zijazo za Kombe la Dunia na hata klabu shiriki kuzuiwa katika michuano inayoandaliwa na Fifa au vyama wanachama.

Fifa ilisema kanuni zinazotumika kote duniani za kupata nafasi kutokana na kushindana kimichezo, mshikamano, kupanda na kushuka daraja ndio msingi wa mpira wa miguu na ndizo zinahakikisha mafanikio duniani na zimeelezwa katika katiba za Fifa na mashirikisho yaliyo chini yake na hivyo haikubaliana na muundo huo wa Super League wa klabu kupata nafasi bila ya kushindana.

Hiyo ilikuwa ni mara ya pili kwa jaribio hilo la kuanzisha ligi mpya kufeli. Wazo hilo lina asili ya Marekani ambako Ligi ya Taifa ya Mpira wa Miguu wa Kimarekani (NFL) haina kushuka wala kupanda daraja na haikuwa ajabu kwa benki ya Kimarekani, JP Morgan kuwa tayari kumwaga mabilioni ya dola kuidhamini.

Wakati wazo hilo likifa kwa nguvu za Fifa, Uefa na vyama wanachama, wasimamizi hao wa soka ulimwenguni sasa wanaona wazo hilo ni bora barani Afrika na rais wake, Gianni Infantino yuko nyuma ya mpango huo, akisema utasaidia kuinua soka barani Afrika.

Inakuwaje mpango huo uwe mzuri Afrika na mbaya Ulaya? Hapa Afrika ndiko kanuni hizo za Fifa za kupata wawakilishi uwanjani hazitumiki? Ni mazingira gani tuliyo nayo Afrika yanafanya Super League iwe nzuri, lakini Ulaya iwe inakinzana na misingi ya mpira wa miguu yaliyowekwa katika katiba za Fifa, Uefa, CAF, Concacaf na vyama wanachama wa mashirikisho hayo?