SIO ZENGWE: Poulsen ameonyesha jambo kwa Lusajo, Novatus

Tuesday September 14 2021
posen pic
By Angetile Osiah

Zamani ilikuwa ni kawaida kusubiri vita kubwa ya viongozi wa klabu zetu mbili kubwa za Simba na Yanga kutokea kwenye kambi ya timu ya taifa, Taifa Stars.

Vita hiyo ilihusu usajili wa wachezaji nyota ambao makocha wa Stars wamewaona sehemu mbalimbali wakati ligi ikiendelea au michuano mingine kama Kombe la Taifa.

Mara nyingi vita hiyo haikusubiri mchezaji aliyeitwa timu ya taifa ang’are kwenye mechi kwanza, bali kuitwa tu kulitosha kuwahakikishia viongozi hao kuwa aliyeitwa ni mchezaji mzuri.

Hapo hukawii kusikia mfadhili wa Yanga au Simba ametinga kambini na baadaye kuwa na mazungumzo na mchezaji fulani na kesho yake unasikia amesajiliwa moja ya timu hizo. Na vita ikiwa kali zaidi, utasikia mchezaji huyo amesaini klabu zote mbili na hivyo kufungiwa.

Ipo mifano mingi ya wachezaji wa aina hiyo na waliotingisha vichwa vya habari vya magazeti mengi wakati wa usajili wao.

Hii ilikuwa inatokana na usajili kuwa unafanywa na watu ambao walikuwa hawaujui mpira, lakini wana imani kubwa na utaalamu wa makocha waliokuwa wanaajiriwa kuifundisha Stars.

Advertisement

Ni dhahiri kuwa ilikuwa ni lazima mpira kupitia hatua hizo kwa kuwa ndio mchakato wa mabadiliko. Lazima kutoka sehemu fulani duni kuja sehemu nyingine iliyoendelea kiasi na hatuwezi kuwalaumu viongozi wa wakati huo kwa vituko hivyo.

Lakini baadhi ya mambo yanavyoendelea ndio unaanza kuingiwa na shaka kwamba tumetoka kule tulikokuwa au tuko kule kule ila kwa staili nyingine?

Usajili wa mwaka huu wa klabu hizo mbili umekuwa na kelele huku mitandao ya kijamii na viongozi wakitaka kutuaminisha kuwa wamefanya usajili bora kuliko wengine.

Na wachezaji wote wanaozungumziwa katika majigambo hayo ni wa nje; Fiston Mayele, Peter Banda, Djuma Shabani, Pape Sakho na wengine wengi wa aina hiyo.

Yaani hakuna mchezaji mzawa anayesifika kuwa ni usajili bora kabisa. Hao ni ziada tu, labda wale ambao wameshajiimarisha kama Tshabalala, Fei Toto, Aishi Manula, Erasto Nyoni, Mwamnyeto, Job na wengine.

Ni kama vile hakuna wachezaji wazuri wazawa wanaoweza kusajiliwa kwa majigambo kama hoja nyingi zinavyotumika kusajili wachezaji wageni, ingawa wako wengi waliotushangaza hadi tukakumbuka vijana wetu.

Lakini kocha Kim Poulsen ametuonyesha kuwa wapo chipukizi wengi wazawa wanaoweza kusajiliwa kwa mbwembwe nyingi tu kama klabu hizo kubwa mbili zingekuwa na mfumo wa uhakika wa kufuatilia wachezaji.

Nilitweet katika akaunti yangu kuwa kama mashabiki wote nchini wangeambiwa wapange kikosi cha Taifa Stars kilichovaana na Madagascar, majina kama Reliant Lusajo Mwakasugule, Novatus Dismas na Nickson Kibabage yasingekuwemo kabisa, na inawezekana hata katika benchi wasingeweka majina hayo.

Lakini Poulsen aliwaamini, akawaanzisha Novatus na Lusajo katika kikosi kilichoanza dhidi ya timu ambayo ilifanya vizuri katika fainali zilizopita za Mataifa ya Afrika (Afcon 2018) nchini Misri.

Na bado katika benchi alikuwa na Kibabage na Israel Mwenda, ambaye baada ya kocha huyo Mdenishi kumuita ndipo klabu kubwa zilipomuonana kumgombea.

Inawezekana kabisa kuwa wachezaji wetu hawajakuzwa vizuri, yaani wanaanza kukutana na kocha mwenye elimu sahihi wakati wameshakuwa na umri mkubwa, lakini kuna wachezaji wazuri sana ambao wanahitaji jicho la ziada kuwabaini.

Kujua kusajili si kukimbilia nje bali kwanza kuangalia rasilimali za ndani katika umri mdogo na kuanza kuziwekea mazingira mazuri ya kukua kuliko kutumia mamilioni ya fedha kuleta wachezaji ambao hatuna uhakika wa kiwango chao.

Kupata wachezaji wazuri wa nje kunahitaji bahati fulani kwa kuwa uwezo wa kushindana kifedha na klabu kubwa ni mdogo. Tulibahatisha kwa Luis Miquissone kwa sababu alikuwa kwa mkopo Msumbiji lakini mazingira ya kumpata mchezaji wa aina yake ni magumu kujirudia.

Hivyo ni muhimu sana kuwa na jicho kali sana ndani ya nchi ili kupata vipaji bora na katika umri mdogo na baadaye kuwapa hao wageni wavinoe ili wanufaike viwango vya nyota kama Miquissone na Clatous Chama ili tuwauze kwa bei mbaya na baadaye waje wasaidie taifa letu.

Advertisement